NDUGAI, UPINZANI WAPIMANA UBAVU BUNGENI

0
933

Na ESTHER MBUSSI, DODOMAMkutano wa 12 wa Bunge umeanza kwa wabunge wa upinzani kuvutana na Spika Job Ndugai, wakati wa kujadili muswada wa kulitangaza Jiji la Dodoma kuwa makao makuu ya nchi.

Mvutano huo ulianza baada ya Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni kuwasilisha maoni yake yaliyosomwa na Mbunge wa Viti Maalumu, Sophia Mwakagenda (Chadema).

Mbunge huyo alianza kwa kuzungumzia namna viongozi wa Serikali wanavyowanunua wabunge wa upinzani na kusema mswada uliokuwa unajadiliwa ni wa kutamka Dodoma kuwa jiji badala ya Jiji la Dodoma kuwa makao makuu ya nchi.

Hatua hiyo ilimwibua mara kwa mara Spika wa Bunge, Ndugai, ambaye alikuwa akimwongoza Mwakagenda kutamka Dodoma kuwa makao makuu ya nchi badala ya Dodoma kuwa jiji.

Naye Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu, Bunge, Sera, Uratibu, Ajira, Kazi na Watu Wenye Ulemavu, Jenista Mhagama, alimtaka Mwakagenda kuendana na hoja iliyopo mezani na kuondoa maneno ya viongozi wa Serikali kununua wabunge wa upinzani.

HALI ILIVYOKUWA

Katika hotuba yake, Mwakagenda alianza kusoma kwa kumshukuru Mungu kwa kuendelea kuwajalia (upinzani) moyo wa ujasiri na uvumilivu kwa kipindi hiki wanapopita kwenye majaribu.

“Nimelazimika kuanza kwa maneno hayo kwa kuwa vitendo vya hila vinavyofanywa sasa hivi vya kurubuni na kuwanunua viongozi wa vyama vya upinzani na kuuhadaa umma kwamba viongozi hao wamefurahishwa na utendaji kazi wa Serikali na kulisababishia taifa hasara ya kurudi kwenye uchaguzi zisizo za lazima,” alisema Mwakagenda.

Baada ya maneno hayo, Jenista alimkatisha akiomba utaratibu wa Spika kwa kanuni kuhusu mtu anayelidanganya Bunge na kujadili suala ambalo halijaletwa mezani kama suala la mjadala na kuzungumzia jambo ambalo lilikwama kuamuliwa na mikutano ya Bunge iliyopita.

“Baada ya kusema hayo, nakuomba unisaidie ni utaratibu gani unavunjwa na jambo gani linaweza likafanywa, katika suala lake ambalo ameanza kulisema kutuhumu Serikali na viongozi kwamba wamekuwa wakifanya biashara ya kuwanunua viongozi, suala hilo hilo linajirudia katika ukurasa wa tatu wa hotuba yake na linajirudia kwenye ‘paragrafu’ ya kwanza ukurasa wa tatu.

“Katika mtazamo wangu na mtazamo wa Serikali, toka chaguzi hizi ndogo zimeanza, si msemaji wa taarifa, wala chama chake, wala mtu yeyote aliyewahi kufungua shtaka lolote katika mahakama yoyote akimtuhumu kiongozi yeyote aliyeondoka upinzani kuwa amenunuliwa.

“Kwahiyo kulileta hili jambo bungeni ni kukiuka kanuni yetu ya 64 (1), jambo hili ni uongo uliokithiri na ambao hauwezi kuvumilika, kanuni ndogo ya (b) inasema ni lazima jambo linaloendelea bungeni liwe linahusu mjadala uliopo, mjadala huu ni Sheria inayohusu kulitangaza Jiji la Dodoma kuwa makao makuu ya nchi, si shughuli za uchaguzi zinazoendelea ndani ya nchi yetu, kwahiyo Spika ni kukiuka kanuni.

“Nikirudi katika kanuni ya 64 (b), hoja hii inayozungumzwa hapa ni tamko la Dodoma kuwa makao makuu na si tamko la kuwa jiji, kwahiyo hii pia ni uvunjifu wa kanuni.

“Jambo hili la Dodoma kuwa jiji lilishatolewa maelezo katika mkutano uliopita, kwahiyo kulirudisha leo ni ukiukwaji wa kanuni,” alisema.

Wakati Jenista akiendelea kutoa utaratibu huo, Mbunge wa Tarime Mjini, Ester Matiko (Chadema), alimtaka kuacha kuchambua hotuba hiyo kwani hawajaisikiliza.

Baada ya kumaliza kutoa hoja hizo, Ndugai alimtaka Mwakagenda kuendelea huku akijaribu kuendana na mambo ambayo ameambiwa; “Natumai umesikia yote uliyoambiwa, unasemaje kuhusu hayo uliyoambiwa, karibu…”

Mwakagenda alisema; “hotuba hii ni ya Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni na si ya CCM, nitajiendeleza kujikita na hotuba yetu.”

Ndugai aliingilia kati tena na kusema; “hii hotuba ni ya msemaji mkuu, na kwa maana hiyo msemaji mkuu ni wewe, si ya kambi. Sasa mambo yaliyozungumzwa hapa ni ya msingi, hatuwezi kuyadharau kwamba inatakiwa kwa kweli tujielekeze kwa kilichoko mezani, kilichoko mezani si uchaguzi, sijui nani kanunuliwa, sijui kamnunua nani, je tukisema twende maadili (Kamati ya Maadili), ukathibitishe nani alitoa shilingi ngapi.

“Lakini itakuwa hatujitendei haki, kwahiyo tutakuwa tumefungua pandora na kwenda kwenye ‘untouched waters’ na hiyo kwa kweli ni ngumu kuitafsiri, hivyo huko mbele sijui utasema ni kitu gani ambacho hutakitoa, yaani ambacho kitapita salama, yaani sioni, labda twende tuone ili uweze kujithibitishia mwenyewe, twende…

“Naomba ujikite kwenye mambo yaliyopo mezani, yaliyopo nje ya kanuni ujaribu kuyaruka, habari ya nani kamnunua nani labda kama una ushahidi endelea nayo, na mimi baada ya kumaliza hii shughuli tutakupeleka kwa wenzako kule.”

Baada ya Spika kusema hayo, Mwakagenda alisema huo ulikuwa ni utangulizi wake kama ambavyo wengine wanampongeza Mbunge wa Jimbo la Buyungu, Christopher Chiza, ambaye aliapishwa jana.

“Kwa bahati mbaya sana Manispaa ya Dodoma haikidhi vigezo vya sheria hiyo,” alisema Mwakagenda kabla Spika hajaingilia kati na kusema; “Mheshimiwa Sophia naomba uheshimu kiti, unafahamu ninavyokuelekeza ni kitu cha msingi kabisa, kwamba jielekeze kwenye sheria iliyoko hapa, sheria hii haizungumzii Manispaa ya Dodoma kuwa jiji.”

Baada ya Spika kusema hayo, alimruhusu Mbunge wa Iringa Mjini, Mchungaji Peter Msigwa (Chadema) kutoa taarifa.

Mchungaji Msigwa alisema; “naomba tupate maelekezo kwani sheria tuliyoletewa hapa inasema ‘a Dodoma Capital City declaration Act 2018’, inazungumzia utawala wa Capital City, tunawezaje kukwepa hayo yote tunapojadili hili la Capital City, labda tupate ufafanuzi kuhusu hili.”

Akijibu hilo Spika alisema ‘capital city’ na ‘city’ ni vitu viwili tofauti.

“Arusha is a city, Arusha is not a capital city, Mwanza is a city, Mwanza is not a capital city, tunazungumza habari ya mji mkuu siyo jiji, majiji yako mengi tu, kama umemaliza Sophia basi tuendelee,” alisema Ndugai.

Mwakagenda akihitimisha mjadala huo, alisema kwa mara nyingi wakileta maoni ya kambi rasmi ya upinzani kumekuwa na utaratibu wa kuwazuia, kwa maana hiyo anaomba hotuba yao ipokewe na iingie kwenye kumbukumbu za Bunge (hansard) ili waonyeshe kama walitoa maoni yao kama wapinzani na Serikali ichukue itakayoona yanafaa.

Akichangia mjadala huo, Mbunge wa Kawe, Halima Mdee (Chadema), alisema amekuwa mbunge kwa vipindi vitatu sasa, lakini hajawahi kuona Bunge linalopelekwa na Serikali kama hili.

“Ni lini Bunge hili lilifanya kazi kwa mujibu wa sheria, Serikali imechomeka suala la makao makuu na hivyo kuhalalisha Bunge kupokonywa mamlaka yake kisheria, hili suala la makao makuu si jipya, lakini pia hakuna anayepinga Dodoma kuwa jiji wala Serikali kuhamia. Lakini hoja ni kwamba utaratibu wa kisheria umekiukwa na pia mipango ya taifa haijatekelezwa kama katiba inavyotaka.

“Mnasema mmehamia Dodoma mmejaza ofisi za Serikali pale Chuo Kikuu cha Dodoma (Udom), mnataka watoto wetu wapate mimba zisizotarajiwa, na hii isije ikajengwa na propaganda kwamba kuna mtu anapinga Dodoma kuwa makao makuu, maana sasa hivi siasa zetu zimetoka katika hoja na kwenda katika vihoja,” alisema Mdee.

Alisema Sheria ya Mipango Miji ya mwaka 2008 inasema vigezo vya jiji ni pamoja na mamlaka ya kutangazwa kwa eneo kuwa jiji ni ya Bunge, lakini hakuna muswada ulioletwa ambao uliinyanyua Dodoma kuwa jiji zaidi ya Rais John Magufuli ambaye kisheria hana mamlaka ya kulitangaza Dodoma kuwa jiji,

Mdee alisema rais anaweza kusema, lakini mamlaka ya Bunge kulipa uhalali ya kuwa jiji lazima yatekelezwe.

Baada ya Mdee kusema hayo, Spika Ndugai alimuuliza Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Dk. Adelardus Kilangi kama ana lolote la kusema juu ya hilo.

Dk. Kilangi alijibu kwa kusema wabunge wengi waliosema kuwa Rais alikosea kulitangaza Dodoma kuwa jiji walitumia Sheria ya Mipango Miji ambayo ni kwa ajili ya kuweka mipango mizuri ya matumizi ya ardhi katika maeneo ya mijini ambayo si sahihi kuitumia katika suala hilo lililopo mezani.

Mbunge wa Malindi, Ally Saleh (CUF), alisema alitarajia kungekuwa na demokrasia katika suala hilo, kwamba pande zote za muungano zingeulizwa kuhusu kuhamishwa makao makuu ya nchi, lakini hilo halikufanyika.

“Wakati Afro Shirazi Party na Tanu zinaungana, pamoja na udogo wangu nilikuwapo kushuhudia, katika hili pia Zanzibar tungehusishwa, waziri aliulizwa hakuna jawabu, sasa unahamishaje wakati hatukuhusishwa,” alisema.

Kwa upande wake, Mbunge wa Iringa Mjini (Chadema) Msigwa alisema hatua ya kuhamia Dodoma si kipaumbele cha taifa na wala haipo kwenye Mpango wa Taifa wa Maendeleo wa miaka mitano.

“Inaweza kuwa jambo zuri lakini lisiwe sahihi, sisi kama wabunge ni wajibu wetu kusimamia kodi za Serikali kwa hiyo masuala mengi tunayoletewa na Serikali ni wajibu wetu kutafakari kwa pamoja kama taifa, kwamba hili suala tunalokwenda kulifanya ‘is it economical’,” alisema.

Mbunge wa Chilonwa, Joel Mwakanyaga (CCM), alisema kwa kiasi kikubwa kutungwa kwa sheria hiyo kutafanya jambo la kuchezewa chezewa kwa makao makuu kusifanyike tena.

Mbunge wa Mtwara Mjini, Maftaha Nachuma (CUF), alipongeza jambo hilo huku akishauri kuwa ni vyema kabila la Wagogo wakapewa elimu ya namna ya kutumia barabara kutokana na ongezeko la matumizi yake hali inayochangia baadhi yao kuwa na tabia ya kuvuka hovyo kwenye ‘zebra’ kama wanaingia ndani ya nyumba.

 

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here