26.2 C
Dar es Salaam
Thursday, April 25, 2024

Contact us: [email protected]

NDUGAI: MSIJALI MANENO YA MAKONDA

ELIZABETH HOMBO Na ASHA BANI-DAR ES SALAAM

SIKU moja baada ya Spika wa Bunge, Job Ndugai, kutakiwa kutimiza ahadi yake ya kuweka vifaa vya kupima wabunge kama wametumia kilevi ama dawa za kulevya kabla ya kuingia Ukumbi wa Bunge,  amesema Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda ni mtani wake, hivyo watu wasijali maneno yake.

Juzi Makonda alimwomba Spika Ndugai kuweka kipimo hicho ili kabla wabunge hawajasimama kuchangia hoja wabainike kama wanatumia dawa za kulevya au la.

“Kaka yangu Ndugai alisema ana nia ya kuweka kifaa maalumu kuwapima wabunge kama wanatumia dawa za kulevya au la, hivyo atimize nia yake hiyo ili kama na huko wapo tuwanyofoe,” alisema Makonda.

Akizungumza jana na MTANZANIA kwa simu,  Ndugai alisema: “Makonda ni mtani wangu, mimi ni Mgogo yeye ni Msukuma, kwahiyo tunataniana… msijali maneno yake, alikuwa ananichapa tu kidogo.”

Wakati wa mkutano wa tatu wa Bunge la 11 Mei mwaka jana, Spika Ndugai alipata kulieleza Bunge kuwa anafikiria kuweka vifaa maalumu vya kupima ulevi kwa wabunge.

Ndugai alitoa kauli hiyo siku chache baada ya Rais Dk. John Magufuli kutengua uteuzi wa aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Ndani, Charles Kitwanga baada ya kuingia bungeni akiwa amelewa.

Alisema kuwa kuna wabunge kadhaa huingia bungeni wakiwa wametumia vilevi vikali.

“Tunajaribu ku-identify (kuwatambua) watu maalumu wanaoweza kutusaidia kuzungumza na hawa watu ili waondokane na matatizo yale ambayo tutaweza kuyagundua.

“Lakini wale wanaofanya kwa kificho itakuwa tabu kidogo. Lakini huko mbele tutakwenda kwenye vifaa, maana si ulevi tu, kuna sigara kubwa (bangi), unga (dawa za kulevya)… watu wanapiga konyagi hadi mchana, kimsingi mambo ni mengi.

“Simaanishi wabunge wote, maana mtu anaweza kufikiri ni wote, hapana. Hili ni kundi dogo mno la wabunge na hawajai hata mkononi. Lakini wabunge walio wengi ni wazuri sana, hawanywi pombe wala nini. Kikundi hiki kinahitaji msaada wa ushauri,” alisema Ndugai.

MAONI YA WABUNGE

Kauli ya Makonda ya kuwataka wabunge kupimwa akili ili kubaini kama wanatumia aina yoyote ya dawa za kulevya au la, imepokewa tofauti na baadhi ya wabunge.

Akitoa maoni jana kwa simu, Mbunge wa Ubungo Saed Kubenea (Chadema), alisema wabunge tayari   wameshapimwa akili na wananchi wao na ndio maana wakapewa ridhaa ya kuwaongoza.

Alisema kulikuwa na michakato mingi hadi wao kuchaguliwa, ikiwa ni pamoja na ya ndani ya chama, majimboni na hata kwenye Tume ya Uchaguzi ya Taifa (NEC), hivyo wao wako safi hadi wakapitishwa na wananchi wao.

“Anayetakiwa kupimwa akili kama anatumia dawa au la au kama aliugua au la ni mtu ambaye aliwahi kumfunga viatu mtoto wa rais, kulala kwenye sebule ya Sitta, na hata kumpiga mzee Warioba na kutukana waliomzidi umri bila sababu,” alisema Kubenea.

Aliongeza kuwa anaamini kwa wasiopimwa sehemu yoyote akiwemo Mkuu wa Mkoa na wateule wengine wa rais ndio ambao wanatakiwa kupimwa.

Mbunge wa Mbeya Mjini, Joseph Mbilinyi, maarufu kwa jina la Sugu, alisema Bunge ni mhimili mwingine, hivyo Makonda hana nguvu ya kuwataka wao kupima. 

Alisema kama ni mawazo ya kutakiwa kupima au kutopimwa, anayetakiwa kusema hiyo ni Spika wa Bunge Ndugai na kama yeye ataafiki wao watakubali kupimwa.

“Sisi mhimili wetu unasimamiwa na Spika ndiye mkuu wetu, lakini alishawahi kusema hilo siku nyingi  kwamba mhimili wake usiingiliwe hovyo hovyo, lakini mtu mmoja mdogo sana anajiongelesha, ambaye hana hata mamlaka,” alisema Sugu.

Alisema yeye mwenyewe Makonda ana matatizo yake na kama akihitaji wao wapimwe, watatakiwa kwenda wote.

Hata hivyo, Sugu ambaye ni Waziri Kivuli wa Habari Utamaduni na Sanaa, aliwalalamikia waandishi wa habari kwa kumpa nafasi Makonda na kuacha kuandika maoni wanayotoa wao kama wazo lake alilotoa bungeni siku ya kufunga Bunge.

Mbunge huyo alisema anatamani siku moja Makonda apelekwe Mkoa wa Mbeya na akawaongoze kwa miezi sita tu aone na si kukaa Dar es Salaam peke yake huku akiingilia kazi za Spika.

Sugu alisema Serikali ya awamu ya tano inaonyesha wazi kwamba inalichukia Bunge kutokana na matamshi mbalimbali yanayotolewa.

Alisema kama angekuwa yeye badala ya kushauri Bunge kwenda kupima, basi anashauri viongozi wote kupimwa wakiwamo wakuu wa wilaya, mikoa na wengine wa Serikali ili nchi iwe salama kwa kila mtu.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles