25.2 C
Dar es Salaam
Thursday, April 25, 2024

Contact us: [email protected]

NDOTO TANGA KUWA BANDARI KUU YA UGANDA YAFUFULIWA

  • Bandari ya Tanga ilianzishwa na Wareno miaka ya 1500
  • Kwa mwaka inahudumia tani 700,000 za mizigo
  • Miaka ya 1960 Milton Obote alimuomba Mwalimu Nyerere kuikodisha bandari ya Tanga

KAMPALA, UGANDA

BOMBA la kusafirisha mafuta lenye urefu wa kilomita 1,400, litaanzia Wilaya ya Hoima kupitia Masaka na Mutukula nchini Uganda hadi Bukoba, Biharamulo, Shinyanga na kuishia Bandari ya Tanga nchini Tanzania.

Bandari ya Tanga ambayo ndiyo itakayotumika kusafirisha mafuta hayo kwenda nje ya nchi kusafishwa, ndiyo kongwe zaidi Afrika Mashariki. Ilianzishwa  na wafanyabiashara wa Kireno miaka ya 1500.

Lengo la kuanzishwa kwake ilikuwa ni kusafirisha pembe na watumwa.

Usafirishaji wa mafuta hayo sasa unatarajiwa kufufua jina la bandari hiyo, ambayo ilipotea katika ramani za kibiashara kwenye ukanda huu, baada ya kuanzishwa Bandari ya Mombasa nchini Kenya na ile ya Dar es Salaam.

Tanga ni bandari ya pili kwa ukubwa nchini Tanzania, ikihudumia tani 700,000 za mizigo kwa mwaka.

Kwa mujibu wa Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA), bandari ya kwanza kwa ukubwa ni Dar es Salaam.

Bandari ya Tanga pia inatarajiwa kuongeza uhusiano wa Tanzania na Uganda, nchi ambayo haina bahari.

Kwa sasa, Uganda inategemea Bandari ya Mombasa kwa zaidi ya asilimia 90 kupitisha mizigo yake inayotoka na kuingia.

Mizigo ya Uganda, hutumia barabara kuingia Mombasa na kutoka. Hii ni kwa sababu ya kutokuwapo reli.

Ujenzi wa reli ya kisasa ya kiwango cha standard gauge katika njia kongwe ya miaka ya 1892, kutoka Mombasa kupitia Nairobi, Kisumu hadi Tororo na Kampala haujakamilika.

Hivyo sasa, mbali na bomba la mafuta, Bandari ya Tanga inafungua fursa nyingine ya Tanzania na Uganda endapo mpango wa kujenga reli utakamilika kwa wakati.

MPANGO WA ZAMANI, HITAJI JIPYA

Miaka ya 1960, Rais wa kwanza wa Uganda, Milton Obote, alimwomba Mwalimu Julius Nyerere, kuikodi Bandari ya Tanga ili iwe kituo cha nchi yake kuifikia bahari kama mbadala wa Mombasa.

Wakati huo Tanga ilikuwa imeanza kupitwa kiukuaji na Dar es Salaam, pia usafirishaji wa mkonge ulikuwa umeshuka jambo lililoififisha Bandari ya Tanga.

Tanzania ilitaka kuwapo matumizi mapya ya bandari ambayo yataleta mapato na kuchochea ukuaji wa jiji.

Hata hivyo mpango huo ulikufa baada ya kupinduliwa kwa Obote mwaka 1971 na kuibuka kwa Idi Amin.

Baada ya Amin naye kupinduliwa mwaka 1979, wazo hilo liliendelea kutotekelezwa.

Badala yake, nguvu ziliwekwa kutumia njia za reli za Tanzania kama mbadala wa kuagiza na kusafirisha bidhaa za Uganda.

Njia hiyo iliibuka baada ya ujenzi wa reli ya kati kutoka Bandari ya Dar es Salaam kupitia Dodoma, Tabora na kuishia bandari ya Mwanza, kisha kusafirishwa na meli ndani ya Ziwa Victoria hadi Jinja au Port Bell nchini Uganda.

Kukamilisha njia ya usafiri wa reli na majini nchini Uganda mwaka 1983, kukaanzisha vivuko vikubwa vitatu vya kufanya safari ziwani kutoka Mwanza (Tanzania) hadi Jinja na Port Bell.

 KUIFANYA TANGA KUWA BANDARI YA UGANDA

Uwezekano wa Tanga kuwa bandari kuu ya Uganda umefufuliwa na bomba la mafuta.

Tanga inatoa faida nyingi kwa Uganda. Haina msongamano na itabakia hivyo kwa miaka mingi kwa sababu ya uwapo wa Bandari ya Dar es Salaam na Mtwara ambazo tayari zinahudumia mizigo ya nchi nyingine zisizo na bahari, zikiwamo Malawi na Zambia.

Hivyo Uganda itakuwa mtumiaji huru wa Bandari ya Tanga ambayo pia itanufaisha nchi nyingine za Rwanda na Sudan Kusini.

Linapokuja suala la umbali, Tanga na Mombasa zina umbali karibu sawa kutoka zilipo hadi Kampala.

Ni kilomita 945 kutoka Tanga hadi Musoma katika Ziwa Victoria na karibu kilomita 300 kutoka Musoma hadi Port Bell au Jinja.

Hivyo kutoka Tanga hadi Port Bell, Kampala ni kilomita 1,245 na Mombasa hadi Kampala ni kilomita 1,165 kwa barabara ikiwa tofauti ya kilomita 100.

Kinachoifanya njia ya Tanga iwe maridhawa zaidi ni kwa sababu inatoa fursa ya unafuu wa gharama na rafiki zaidi kwa mazingira duniani za  reli na majini.

Bahati mbaya kwa sasa Uganda hakuna vivuko vinavyofanya kazi katika njia hizo. Shughuli za majini zilihamishwa kwa Shirika la Reli la Rift Valley wakati Shirika la Reli Uganda likiendelea kuwa msimamizi mkuu.

Hivyo ili kuifanya ndoto ya Tanga kuwa kweli, mataifa yote ya Uganda na Tanzania yatapaswa kuwekeza katika uboreshaji na uanzishaji wa miundombinu katika njia hiyo kwa kuanzia reli ya kisasa.

Kwa sasa kuna njia nyembamba ya reli inayotoka Bandari ya Tanga hadi Moshi ikiwa na matawi katika njia ya Mombasa-Kampala katika Voi na vilima vya Taveta nchini Kenya.

Njia hiyo inapaswa kuboreshwa kuwa katika kiwango cha standard gauge na kurefushwa hadi Arusha na Musoma katika pwani ya Ziwa Victoria, ambako vyombo vya majini vinaweza kusafirisha makontena katika Port Bell/Bukasa, Bukakata na Majanji nchini Uganda.

Mizigo ya kuelekea Uganda itashushwa Port Bell na Jinja wakati mizigo kuelekea Sudan Kusini itashushwa katika bandari ya Majanji mashariki mwa Uganda, ambako reli ya urefu wa kilomita 52 itaiunganisha na Tororo na kisha kusafirishwa kwenda Pakwach of Gulu, kwa barabara kupitia mipaka ya Nimule au Oraba.

Mizigo ya kuelekea Rwanda itashushwa Bukakata na kusafirishwsa kwa barabara kupitia Masaka, Mbarara na Katuna au vilima Mirama.

Kuifanya ndoto hii kuwa kweli, nchi inahitaji vyombo vikubwa vya majini vinavyoweza kubeba makontena na mizigo ya wazi kama magari katika  Ziwa  Victoria na vilevile kufufua MV Pamba na MV Kaawa vilivyosimamishwa.

Bandari mpya pia zinapaswa kujengwa Bukakata na Majanji, huku zile kongwe katika Jinja na Port Bell zikiboreshwa kuweza kuhudumia mizigo mikubwa zaidi.

Hali kadhalika, hatua za kiusalama za majini zinapaswa kuzingatiwa.

NDOTO YA UGANDA KWA BANDARI YA TANGA

Kamishna wa Forodha katika Mamlaka ya Mapato Uganda (URA), Dicksons Kateshumbwa, alisema mwaka 2013, URA na Wizara ya Biashara vilifanya utafiti wa kuangalia iwapo inawezekana kuiongeza Tanga katika utekelezaji wa Himaya Moja ya Forodha (SCT) wakati Tanzania itakapokuwa tayari.

SCT ni hatua ya kufikia umoja kamili wa forodha unaofikiwa kwa kuondoa vikwazo vya  kibiashara, ikiwamo  kupunguza udhibiti kwenye mipaka ya ndani, ambayo ilipitishwa karibuni na wakuu wa nchi za Afrika Mashariki (EAC).

Tanzania ilikuwa tayari kwa mpango huo mwanzoni mwa mwaka 2014.

Hata hivyo, tathmini ilibaini kuwa Bandari ya Tanga haikuwa fanisi kama njia bora kwa mizigo inayoelekea Uganda.

Moja ya sababu ni changamoto zilizopo kwa sasa za kusafirisha mizigo kupitia Tanzania kutokana na uwapo wa mfumo mbovu wa usafirishaji wa ardhini.

Mizigo yote ikiwamo mafuta husafirishwa kwa barabara na tathmini inasema kuwa Tanga imekosa uwezo wa kuhudumia meli kubwa zaidi na hivyo inahitaji uwekaji wa vifaa vya kisasa.

“Ni kweli kupitia Bandari ya Tanga kutakuwa na manufaa makubwa kwa sababu inatoa njia fupi hadi bandari ya Mwanza katika Ziwa Victoria kuunganisha na Port Bell na Jinja iwapo usafirishaji ziwani utaimarishwa. Pia inatoa umbali mfupi wa kusini magharibi mwa Uganda kupitia Mutukula na Kikagati,” anasema Kateshumbwa.

Kwa mujibu wa Wizara ya Biashara, sehemu ya mpango wa kuwezesha uboreshaji wa biashara kuunganisha Uganda na njia mbadala, ni pamoja na kukamilika kwa Bandari ya Bukasa. Serikali hivi karibuni iliamua kukopa fedha kutoka China kuboresha bandari hiyo.

Taarifa kutoka wizara hiyo hata hivyo iligusia kwamba ufanisi wa matumizi ya bandari za ndani ya Uganda utategemeana na kuboreshwa kwa miundombinu nchini Tanzania kama vile reli na Bandari ya Tanga.
Ofisa mmoja mwandamizi wa uchukuzi katika Wizara ya Ujenzi, Henry Ategeka, alisema mwaka 2009 viongozi wa Uganda na Tanzania walisaini hati makubaliano (MoU) kufufua mtandao wa reli na bandari katika Ziwa Victoria, ambao unahitaji uwekezaji mkubwa wa fedha.
Lakini pia maofisa wa Wizara ya Ujenzi ya Uganda walikiri kuwa Tanzania inaonekana ‘kutotaka mchezo’ katika mikakati hiyo, wakati upande wa Uganda haujafanya vya kutosha.”

Timu ya pamoja kutoka nchi zote mbili imeanzishwa na kwa sasa sekretariati ya ukanda wa kusini ipo Tanzania.

“Kipindi cha miezi 2-3 ijayo tutakuwa na muswada ambao Baraza la Mawaziri utaupitia na baada ya hapo tutakuwa tayari kuendelea na hatua nyingine,” alisema Ategeka.

Waagizaji na wasafirishaji wa bidhaa wa Uganda watakuwa wakisubiri kwa hamu kubwa wakitumaini kuwa bomba la mafuta ni moja tu ya fursa wanayoisubiri kwani kuna njia nyingine mbadala na ya gharama nafuu ya kuifikia bahari wanayoitazamia.

 

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles