33.2 C
Dar es Salaam
Friday, March 29, 2024

Contact us: [email protected]

NDOA BORA HUJENGWA KWA KUTANGULIZA MAHITAJI YA MWENZA

Na CHRISTIAN BWAYA


BINADAMU tunazaliwa na hulka ya ubinafsi ndani yetu. Ubinafsi ni ile tabia ya kuweka mahitaji yetu mbele ya mahitaji ya wenzetu. Ni hulka ya kutafuta utoshelevu binafsi kwanza kabla ya kufikiri namna ya kumsaidia mwingine kupata mahitaji yake.

 

Tabia hii ina umuhimu wake kwa mwanadamu. Kwanza, ni mbinu ya asili ya kutetea usalama wa mtu binafsi. Dunia yetu ina mengi yanayotishia usalama wetu. Mwenyezi Mungu, kwa kutambua hilo, alituumba na hulka ya ubinafsi ili iwe rahisi kwetu kupambana kuwa salama.

 

Fikiria unapokutana na adui anayetishia uhai wako. Mchanganyiko wa wasiwasi na hasira unaweza kukufanya ufikiri mbinu za dharura ili kujiokoa na hata ikibidi kumwangamiza adui. Katika mazingira kama haya, ubinafsi unakuwa na nafasi ya kukuwezesha kutetea usalama wako. Vivyo hivyo unapojikuta katika mazingira ya ajali. Kwa kuhisi maisha yako yako hatarini, ubinafsi utakufanya utafute namna ya kujiokoa mwenyewe kabla hujafikiria usalama wa jirani yako.

 

Lakini pia, mbali na usalama wa kimwili, binadamu anahitaji kulinda usalama wake wa kisaikolojia. Hapa tunazungumzia hadhi ya mtu kwa maana ya taswira ya jumla anayojijengea kama binadamu anayestahili heshima mbele ya macho ya jamii. Ubinafsi tulioumbiwa unafanya kazi ya kumsaidia binadamu kutetea hadhi hii ambayo ndiyo msingi wa furaha ya mwanadamu.

 

Fikiria, kwa mfano, umesikia maneno yanayochafua heshima yako mbele ya jamii yanaenea. Katika mazingira kama haya, ule ubinafsi unaoishi ndani yako unaweza kukusukuma kuchukua hatua za dharura zinazolenga kupambana na tishio hilo la kuchafuliwa na mtu anayeonekana kuwa na nia ovu na wewe. Mbali na kukabiliana na mtu huyo, pia unaweza kujitetea kwa kutoa ufafanuzi unaolenga kusafisha hali ya hewa katika jitihada za kulinda hadhi yako.

 

Kwa ujumla tunaweza kusema, ubinafsi ndani ya mwanadamu ni masalia ya hatua ya awali ya ukuaji inayolenga kuhakikisha tunapata na kulinda mahitaji yetu ya msingi. Hatua hii ni muhimu kwa sababu bila mahitaji haya kukamilika, ni vigumu mtu kujali mahitaji ya wengine.

 

Ubinafsi unaathiri uhusiano

 

Hata hivyo, ubinafsi usipodhibitiwa unaweza kuathiri ustawi wa watu wengine katika jamii. Matatizo mengi tunayoyaona katika jamii, kwa mfano, yanaanza na tabia ya watu kutanguliza maslahi yao mbele yaw engine. Mapambano ya watu binafsi kujilinda, mathalani, yanaweza kuleta hasara kubwa kwa watu wengine.

 

Fikiria marafiki ambao kila mmoja anapambana kivyake kulinda usalama wake wa kisaikolojia bila kujali mwenzake anaathirika vipi. Ikitokea, kwa mfano, watu hawa wakagombana itakuwa vigumu kupata suluhu kwa sababu kila mmoja anapambana kulinda usalama wake. Katika mazingira haya, hakuna atakayekuwa tayari kumwomba msamaha mwenzake kwa sababu kufanya hivyo kutaonekana si tu kumkweza mwenzake bali kuhatarisha heshima yake.

 

Kwa msingi huo, kisaikolojia, ukomavu katika maisha yetu hupimwa kwa namna mtu anavyoweza kudhibiti ubinafsi huo unaoishi ndani yake. Mtu aliyekomaa kisaikolojia, ni yule mwenye uwezo wa kumtanguliza mwenzake kwa maana ya kujali mahitaji ya mwenzake kama anavyoweza kujali mahitaji yake binafsi. Mtu mkomavu ni yule anayeweza kuvaa viatu vya mwenzake na kuyafanya mahitaji ya mwenzake kuwa mmoja wapo ya vipaumbele vyake.

 

 

Ubinafsi na ndoa

 

 

Haiwezekani urafiki mzuri ustawi katika mazingira ambayo kila mmoja anapigania maslahi yake wenyewe bila kujali maslahi ya mwenzake. Urafiki wowote wa karibu unajengwa kwenye msingi wa watu wawili kuwa tayari kuvuka handaki la ubinafsi.

 

Inapotokea watu wawili wasioweza kudhibiti ubinafsi wao wanaamua kuishi pamoja, upo uwezekano mkubwa wa kutokea mifarakano. Mmoja anapotanguliza mahitaji yake, mwingine hujisikia kutumika na wakati mwingine kunyanyasika. Hapa ndipo matatizo yanapoanzia.

 

Ndio kusema ndoa bora hujengwa wawili wanapofanikiwa kupambana na ubinafsi wao. Bila ubinafsi, kwa mfano, ni rahisi mtu kujali hisia za mwenzake hata kama na yeye anazo hisia zake. Bila ubinafsi inawezekana kuvumilia tofauti ya mawazo kati ya watu wawili wanaotofautiana kimtazamo. Bila ubinafsi, watu wawili wanaweza kusameheana.

 

 

Ushauri

 

Kwa kijana anayefikiria kuingia kwenye ndoa, ni vyema kuanza maandalizi kwa kupambana na hulka ya kutanguliza mahitaji yake mbele ya mahitaji ya mwenzake. Ukiweza kudhibiti ubinafsi wako utaweza kujitoa kwa mwenzako kwa kiwango kinachostahili. Ukiweza kudhibiti ubinafsi utakuwa kwenye nafasi nzuri zaidi ya kufanya juhudi za kutambua na kuelewa tafuta mahitaji ya mwenzako. Lazima kuanza kujifunza namna ya kujali hisia za wengine kuliko kusubiri mtu mwingine wa kujali hisia zako.

 

INAENDELEA

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles