24.2 C
Dar es Salaam
Thursday, April 18, 2024

Contact us: [email protected]

Ndanda waipigia magoti Yanga

NA MICHAEL MAURUS, MTWARA

LIGI Kuu ya Tanzania Bara msimu wa 2014/2015 inamalizika leo kwa timu 14 za ligi hiyo zitakapokuwa katika viwanjani tofauti, huku mabingwa wa ligi hiyo, timu ya Yanga wakiwa wenyeji wa Ndanda FC ya Mtwara.

Yanga, walioondoka Dar es Salaam juzi, tayari wamewasili mkoani humo kuwavaa Ndanda katika Uwanja wa Nangwanda Sijaona, huku wenyeji hao wakiomba ishinde mchezo huo ili isalie kwenye ligi hiyo inayodhaminiwa na Vodacom msimu ujao.
Ndanda, walio na pointi 28, ipo katika hatari ya kushuka daraja kutokana na kuwiana pointi na timu nyingine za Stand United ya Shinyanga, Mgambo JKT ya Tanga na Tanzania Prisons ya Mbeya.

Yanga wamefikia katika hoteli ya Veta mjini hapa na leo jioni watafanya mazoezi ya mwisho katika Uwanja wa Nangwanda Sijaona, kabla ya kushuka dimbani kuwavaa Ndanda FC.
Meneja wa timu ya Yanga, Hafidh Saleh, alisema mjini hapa kuwa wanataka kuweka heshima kwa kumaliza ligi kwa kishindo wakiwa na ubingwa wao waliokabidhiwa Jumatano katika Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, licha ya kufungwa mabao 2-1 na Azam FC.
“Wachezaji wote wako fiti kwa mchezo wetu na Ndanda na hatutaremba, bali ni kutoa kipigo tu ili kumaliza ligi kwa kishindo,” alisema.
Hata hivyo, mashabiki wa timu ya Ndanda wameonekana kubeba mabango ya kuitaka Yanga kuibeba timu yao ili isishuke daraja, huku wakiahidi kulipa fadhila msimu ujao.

Mechi nyingine zitakazochezwa leo, JKT Ruvu itacheza dhidi ya Simba katika Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, huku makamu bingwa wa ligi hiyo, timu ya Azam FC wakiikaribisha Mgambo Shooting katika Uwanja wa Azam Complex, Dar es Salaam.

Wenyeji Stand United wataikaribisha Ruvu Shooting katika Uwanja wa Kambarage, Shinyanga, huku Kagera Sugar wakiialika Tanzania Prisons katika Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza.

Mbeya City watakuwa katika Uwanja wa Sokoine, mjini Mbeya kuialika Polisi Morogoro, huku Mtibwa Sugar na Coastal Union zikichuana katika Uwanja wa Manungu, Morogoro.

Wakati huo huo, Rais wa Shirikisho la mpira wa miguu nchini, Jamal Malinzi, amewaagiza wasimamizi wa vituo vya ligi hiyo kuhakikisha sheria na taratibu zote za mechi zinafuatwa.

Malinzi ameagiza hivyo kutokana na kuwepo kwa dalili za upangaji wa matokeo katika mechi za mwisho za ligi hiyo, inayohitimishwa leo katika viwanja mbalimbali nchini.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles