30.2 C
Dar es Salaam
Friday, March 29, 2024

Contact us: [email protected]

Nassari avuliwa ubunge akiwa kazini

Na MWANDISHI WETU-DAR ES SALAAM

MBUNGE wa Arumeru Mashariki, Joshua Nassari (Chadema), amevuliwa ubunge kutokana na kutohudhuria mikutano mitatu ya Bunge mfululizo, huku mwenyewe akisema amepokea taarifa hiyo akiwa kwenye kazi za kibunge mkoani Kilimanjaro na Kamati ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii.

Kuvuliwa ubunge wa Nassari kunafanya Chadema kupoteza wabunge nane tangu Uchaguzi Mkuu wa 2015, ambapo kati yao saba walijiuzulu uanachama wa chama hicho na baadaye kuteuliwa tena kuwania nafasi zao kupitia CCM.

Jana Spika wa wa Bunge, Job Ndugai, alimwandikia barua Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi (NEC), Jaji Semistocles Kaijage, kumtaarifu kuwa Jimbo la Arumeru Mashariki lipo wazi.

Taarifa hiyo ilieleza sababu za Nassari kuvuliwa ubunge kuwa ni kutohudhuria mikutano ya Bunge mitatu mfululizo.

Taarifa hiyo ilitaja mikutano hiyo kuwa ni mkutano wa 12  wa Septemba 4 hadi 14, 2018), mkutano wa 13 wa Novemba 6 hadi 16, 2018 na ule wa 14 wa Januari 29 hadi Februari 9 mwaka huu.

Taarifa hiyo ilisema. “Uamuzi huo wa Spika umezingatia masharti ya Katiba ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Ibara ya 71(1) (c). Ibara hiyo inaeleza kuwa ‘Mbunge atakoma kuwa mbunge na ataacha kiti chake katika Bunge ikiwa atakosa kuhudhuria vikao vya mikutano ya Bunge mitatu mfululizo bila ya ruhusa ya Spika.

“Ibara hiyo pia imefafanuliwa katika kanuni ya 146 (1) na (2) ya kanuni za kudumu za Bunge toleo la Januari 2016, kuwa ‘kuhudhuria vikao vya Bunge na kamati zake ni wajibu wa kwanza wa mbunge, mbunge yeyote atakayeshindwa kuhudhuria mikutano ya Bunge mitatu mfululizo bila ruhusa ya Spika iliyotolewa kwa maandishi, atapoteza ubunge wake na Spika ataitaarifu Tume ya Taifa ya Uchaguzi”.

Taarifa hiyo ilisema “Tume ya Taifa ya Uchaguzi inaweza kuendelea na mchakato wa kumpata Mbunge wa kujaza nafasi hiyo iliyo wazi ya Jimbo la Arumeru Mashariki”.

KAULI YA NASSARI

Akizungumzia taarifa hiyo, Nassari alisema ni kweli kuwa hakuhudhuria mikutano hiyo lakini kuhusu mkutano wa Januari aliiandikia Ofisi ya Bunge barua ya kuomba ruhusa kuwa hataweza kuhudhuria mkutano huo kwa kuwa alikuwa anamuguza mkewe.

“Mke wangu alikuwa anaumwa na nilikuwa namuuguza nje ya nchi na baadaye alijifungua salama, lakini wakati mkutano huo wa Januari unaanza niliomba ruhusa nikaiandikia Ofisi ya Bunge email.

“Wakati huu ninavyoongea na wewe niko na kamati yangu ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii kwa hiyo bado sielewi chochote ngoja nifuatilie kwanza,”alisema Nassari.

Alisema jana yeye na kamati yake walifanya ziara katika chuo cha wanyamapori Mwika.

Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Ardhi na Maliasili, Shabani Shekilindi, alisema Nassari alikuwa kwenye kamati hiyo tangu juzi.

Shekilindi ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Lushoto (CCM), alisema kamati hiyo ilianza kazi Machi 11.

Hadi gazeti hili linamtafuta mwenyekiti huyo, kujua kama kweli Nassari yupo kwenye ziara ya kamati, alisema alikuwa hana taarifa za Mbunge huyo wa Arumeru Mashariki kuvuliwa ubunge wake.

BARUA YA NASSARI KWA SPIKA

Barua ya Nassari ya Januari 29 mwaka huu aliyoielekeza kwa Spika wa Bunge, ilieleza kuwa hataweza kuhudhuria mkutano huo kutokana na sababu zilizo nje ya uwezo wake.

“Kwa muda sasa nimekuwa nikifuatilia matibabu ya mwenza wangu anayetibiwa nje ya nchi na taarifa njema ni kwamba amejifungua mtoto wa kike siku mbili zilizopita.

“Hata hivyo madaktari wake wameshauri wanatakiwa wawe naye katika uangalizi wa karibu, nimeliandika hili ili ofisi yako ijue na ninasikitika kuwa nitashindwa kuhudhuria wiki hizi kabla hatujarudi nchini.

“Naahidi kuhudhuria vikao vinavyokuja baada ya kurudi kwangu nchini,”ilisema barua hiyo.

Watoro bungeni

Novemba 15, mwaka jana Spika Ndugai, alitaja orodha ya wabunge na mawaziri watoro lakini jina la Nassari halikuwepo.

Katika orodha hiyo aliwataja Mbuge wa Arusha Mjini, Godbless Lema (Chadema) na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Augustine Mahiga, ndio vinara wa utoro kwenye vikao vya Bunge.

Ndugai alisema mahudhurio ya wabunge hao yamechukuliwa kutoka kwenye vikao vya kamati za Bunge 33 ambavyo vilikaa Machi, Agosti na Oktoba na vikao 61 vya mkutano wa 11 wa Bunge la bajeti na tisa vya Bunge la 12.

Alisema taarifa hiyo aliyoitoa bungeni jana, siyo ya kisiasa kwasababu mahudhurio hayo ni kwa mujibu wa usajili ambao wabunge hufanya kwa njia ya kielektroniki mara waingiapo kwenye vikao.

MAWAZIRI WATORO

Ndugai aliwataja mawaziri waliopata alama chache katika mahudhurio hayo na asilimia zao katika mabano kuwa ni Waziri wa Mifugo na Uvuvi Luhaga Mpina (45), Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Kazi William Lukuvi (41).

Wengine ni Waziri wa Katiba na Sheria Profesa Palamagamba Kabudi wakati huo, Waziri wa Nchi katika Ofisi ya Makamu wa Rais, January Makamba na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Augustine Mahiga wakati huo.

“Mahudhurio yao si mazuri lakini waziri ambaye ana mahuzurio mazuri amepata asilimia 90 ambaye ni Jenista Mhagama (Waziri wa Nchi katika Ofisi ya Waziri Mku Sera, Bunge, Kazi, Ajira na Wenye Ulemavu), wengine wote wanasuasua tu,” alisema Ndugai.

Alisema suala la utoro si zuri na mawaziri wakati wa Bunge wanapaswa kuhudhuria vikao na kama hawapo watoe taarifa.

MANAIBU WAZIRI WAHUDHURIAJI

Alisema kwa upande wa manaibu waziri, mwenye mahudhurio mazuri zaidi ni Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Ashatu Kijaji, ambaye amehudhuria vikao vyote vya kamati pamoja na vya Bunge.

Wanaomfuata ni Hamad Masauni (Wizara ya  Mambo ya Ndani) Antony Mavunde ( Ofisi ya waziri Mkuu Sera, Bunge, kazi, Ajira, Vijana na wenye Ulemavu) Mussa Sima (Ofisi ya Makamo wa Rais Mazingira na Muungano).

Wengine ni Abdalah Ulega (Wizara ya Mifugo na uvuvi), John Kuandikwa (Wizara ya Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi) Atashasta Nditiye (Wizara ya Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi).

WABUNGE WATORO

Ndugai aliwataja wabunge  wenye mahudhurio mabaya kabisa kuwa ni  Salim Hamis Salim (Meatu-CCM), Abdul Azizi (Morogoro-CCM) Hussen Nassoro Amar (Nyangwale-CCM), Mbaraka Bawazir (Kilosa-CCM), Dk. Mathayo David Mathayo (Same Magharibi-CCM).

Wengine John Mnyika (Kibamba-Chadema), Salim Hassan Turky (Mpendae-CCM), Suleiman Nchambi (Kishapu-CCM) na kwamba mbunge wa Arusha Mjini (Chadema) ndio mbunge anayeongoza kwa utoro ambapo kwa vikao vya kamati na Bunge amehudhuria kwa asilimia 7.8 tu.

“Na hii sio habari njema kwa wapiga kura wenu ambao mnategemea kusimama tena kuwaongoza wakati mahudhurio yenu ni haya. Na pia mahudhurio yenu haya nayapeleka kwenye vyama vyenu nao wajue maana tumeshasema sana,”alisema.

Alitaja wabunge waliohudhuria vikao vyote kwa asilimia 100 ambao wote ni wa CCM Justin Monko (Singida Kaskazini), Felister Bura (Viti Maalum) na Omary Kigua (Kilindi).

Wanaofuatia kwa uhudhuriaji mzuri ni Joel Mwaka (Chilonwaa), Halima Bulembo (Viti Maalum-CCM) Mbarock Salum (Wete) Hawa Mchafu, Allan Kiula (Iramba Mashariki-CCM), Rashid Shangazi (Lushoto-CCM), Mendrad Kigola (Mufindi Kusini-CCM).

Wengine ni Augustine Masele (Mbogwe-CCM), Innocent Bashungwa (Kerwa-CCM) na Juma Hamad Omary (Ole-CUF).

Chadema yapoteza mbunge wa nane

Baada ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015, idadi kadhaa ya madiwani wa vyama vya upinzani walianza kujiuzulu na baadaye kujiunga na chama tawala CCM.

Mbali na madiwani, baadaye baadhi ya wabunge wa vyama hivyo vya upinzani nao walianza kujiuzulu na kujiunga na CCM.

Wabunge wa upinzani waliojiuzulu na baadaye kujiunga na CCM ni pamoja na Dk. Godwin Mollel (Siha-Chadema), Mwita Waitara (Ukonga-Chadema), Julius Kalanga (Monduli-Chadema).

Wengine ni Maulid Mtulia (Kinondoni-CUF),Zuberi Kuchauka (Liwale-CUF), Pauline Gekul (Babati Mjini-Chadema), James Ole Millya (Simanjiro-Chadema), Chacha Marwa (Serengeti-Chadema), Joseph Mkundi (Ukerewe-Chadema).

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles