22.8 C
Dar es Salaam
Thursday, April 18, 2024

Contact us: [email protected]

Nani kumrithi Bouteflika baada ya damu kumwagika?

HASSAN DAUDI NA MITANDAO

BAADA ya wiki kadhaa za maandamano yaliyokwenda sambamba na umwagaji damu, hatimaye Rais wa Algeria, Abdelaziz Bouteflika, alikubali kujiuzulu, hatua ambayo imewakuna wengi ndani na nje ya Taifa hilo la Kaskazini mwa Afrika.

Bouteflika alikuwa chanzo cha vurugu zilizogharimu maisha ya maelfu ya wananchi kwa uamuzi wake wa kutaka kugombea kiti cha urais kwa mara ya tano, katika Uchaguzi Mkuu uliokuwa unatarajiwa kufanyika Machi 11, mwaka huu.

Wananchi walioingia mitaani kupinga uamuzi wake huo walitilia shaka umri (miaka 82) na afya yake iliyodhoofishwa na ugonjwa hatari wa kiharusi, wakiamini asingeweza kutekeleza majukumu yake ipasavyo.

Kuthibitisha hilo, siku chache baada ya kung’atuka, imeripotiwa kuwa anajiandaa na safari ya kwenda Qatar au Uswis kwa matibabu.

Baada ya kujiuzulu sasa, wafuatiliaji wa siasa za nchi hiyo wanasubiri kusikia tarehe mpya ya uchaguzi huo ingawa sasa ni Abdelkader Bensalah ndiye anayeushikilia wadhifa wa urais kwa kipindi ambacho hakitakiwi kuzidi siku 90.

Bensalah anatambuliwa kuwa ni swahiba mkubwa wa Bouteflika, ikikumbukwa kuwa alikuwa akishirikiana naye katika majukumu mbalimbali ya urais, hasa kipindi ambacho kiongozi huyo alikuwa akisumbuliwa na maradhi.

Pia, ni mapema mno kusahau kuwa Bensalah alikuwa mstari wa mbele kuunga mkono juhudi za bosi wake huyo kuitaka awamu ya tano madarakani.

Mbali ya siku ya uchaguzi, shauku nyingine ya walio wengi ni mvutano unachoendelea kati ya wanaopewa nafasi ya kuingia Ikulu kukikalia kiti cha Bouteflika aliyeachia ngazi akiwa na umri wa miaka 82, ambaye aliingia madarakani mwaka 1999.

Wapo wanaomtazama Ofisa Mwandamizi wa Jeshi la Wananchi, Ahmed Gaid Salah, kuwa ndiye mwenye nafasi ya kuchukua kijiti, ikiwa haijasahaulika kuwa alikuwa mstari wa mbele kutaka wananchi wakatae kitendo cha Bouteflika kugombea tena katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu.

Nguvu kubwa aliyonayo naibu waziri wa ulinzi huyo ni sifa ambazo amekuwa akipewa kutokana na kufanikiwa kwa mikakati yake ya kudhibiti ugaidi, licha ya bajeti ndogo aliyotumia.

Juu ya kugombea nafasi ya kumrithi Bouteflika, ripoti ya Bunge la Ufaransa imeweka wazi kuwa Gaid Salah, anajiona kuwa mwanasiasa mwenye sifa ya kuwa Rais wa Algeria mara tu Uchaguzi Mkuu utakapomalizika.

Mbali na huyo, wapo wachambuzi wanaoamini kuwa kigogo huyo atakumbana na upinzani mkali na hata kuzidiwa kete na Said Bouteflika, mdogo wa rais aliyejiuzulu.

Ni kwa muda mrefu sasa, wafuatiliaji wa siasa za Algeria wamekuwa wakimtaja Said kuwa na nia ya kuingia Ikulu, wakiamini huu ni wakati mwafaka kwake kutimiza hilo.

Mhadhiri huyo wa zamani wa masomo ya fizikia aliingia serikalini mara tu kaka yake, Bouteflika, alipotinga Ikulu mwaka 1999, akimteua kuwa mshahuri wake.

Hata Bouteflika alipopata maradhi ya kupooza mwaka 2013, mdogo wake huyo, Said, ndiye aliyesafiri naye hadi Ufaransa kusimamia matibabu yake. Wanaomjua, wanamtambua kuwa ndiye mtu wa karibu zaidi kuliko ndugu zake wengine, akitumia kila njia kulinda masilahi yake.

Sasa, inaweza kutabirika kirahisi kuwa huenda ndoto yake ya kuingia madarakani isitimie, kwani alikuwa bega kwa bega na Bouteflika wakati wananchi wasio na hatia wakipoteza maisha katika maandamano ya hivi karibuni. 

Endapo atafanikiwa, basi atakuwa ametumia nguvu kubwa kuwashawishi wapiga kura.

Lipo pia jina la aliyewahi kuwa Waziri Mkuu, Ali Benflis, ambaye hii itakuwa ni mara ya tatu kugombea urais, ukiacha awamu mbili zilizopita (2004 na 2014) alizoambulia patupu mbele ya Bouteflika.

Benflis aliyekuwa Katibu Mkuu wa chama tawala, National Liberation Front (FLN), ameweza kujijengea umaarufu mkubwa katika ulingo wa siasa tangu alipopokonywa wadhifa huo mwaka 2003.

Huku naye akionyesha nia ya kuutaka urais wa Algeria, akisema yeye ndiye mtu anayepaswa kuongoza mabadiliko, mataifa ya Magharibi yanamuona kuwa ndiye mtu sahihi kuchukua nafasi iliyoachwa wazi na Bouteflika.

Je, vipi kuhusu Lakhdar Brahimi, mwanadiplomasia mkongwe na mwenye heshima kubwa nchini humo? Kukubalika kwake katika siasa za nchi hiyo kunatokana na kazi nzuri aliyoifanya akiwa waziri wa mambo ya nje. 

Kama hiyo haitoshi, kuingia katika Sekretarieti Kuu ya Umoja wa Mataifa (UN) kunamwongezea sifa mbele ya macho ya wanaomtazama kuwa anafaa kuiongoza Algeria. “Ni mmoja kati ya wanadiplomasia makini zaidi duniani,” aliwahi kusema Katibu Mkuu wa zamani wa UN, Ban Ki-moon.

Vilevile, joto la Uchaguzi Mkuu huo halijawaacha kando wafanyabiashara wenye majina makubwa nchini humo. Inaeleweka kuwa kwa kipindi chote cha utawala wa Bouteflika, tabaka la wafanyabiashara lilionekana kuwa na nguvu, hata kupelekea baadhi ya viongozi wa serikali kupoteza nyadhifa zao pale walipoonekana kuwawekea vizingiti.

Hivyo basi, orodha ya wafanyabiashara wanaopewa nafasi ya kuleta upinzani mkali katika mbio za urais mwaka huu ina jina la bilionea Issad Rebrab na tayari ameelezea kiu yake ya kuitwa rais wa Algeria.

Licha ya ‘ubize’ wake katika biashara, ambapo mbali ya miradi mingine pia ni mmiliki wa vituo vya televisheni, Rebrab amekuwa akionesha hisia zake katika ulingo wa siasa, mfano mzuri ukiwa ni kitendo chake cha kumpinga Bouteflika katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2014.

Ukilieka kando jina la Rebrab, mfanyabishara tajiri mwingine anayepewa nafasi ya kwenda Ikulu kukalia kiti cha Bouteflika ni Ali Haddad. Akiwa mmiliki wa vyombo vya habari, hakuwa na maelewano mazuri na Bouteflika na serikali yake.

Kutokana na hilo, haikushangaza vyombo vyake vya habari kuzipa muda mwingi wa hewani taarifa zilizokuwa zikimshinikiza Bouteflika kujiuzulu.

Akihojiwa na tovuti ya TSA mwaka 2017, Haddad, ambaye pia anamiliki kampuni za ujenzi na klabu ya soka, hakuficha bali aliweka wazi kuwa anakaribia kuingia madarakani, akijitaja kuwa ni mzalendo wa Algeria.

Wakati huo huo, licha ya kukosa umoja, kwa maana ya kusimamisha mgombea mmoja, vyama vya upinzani navyo vinapewa nafasi yake katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu.

Vikiwa ndivyo vyama vikuu vya upinzani, Socialist Forces Front (FFS) na Rally for Culture and Democracy (RND), ndivyo vilivyoanza kukataa Bouteflika asigombee kwa awamu ya tano, kabla ya wananchi wa Algeria kushawishika kuingia mitaani.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles