24.2 C
Dar es Salaam
Wednesday, April 17, 2024

Contact us: [email protected]

Nangole aomba arudishiwe ubunge

nangolepicNa ELIYA MBONEA, ARUSHA

ALIYEKUWA Mbunge wa Longido, Onesmo ole Nangole (Chadema), amewasilisha hoja sita mbele ya jopo la majaji watatu wa Mahakama ya Rufaa ya Tanzania akipinga hukumu ya kutengua ubunge wake.

Katika hoja hizo, Nangole kupitia kwa Wakili Method Kimomogolo, anapinga uamuzi wa Mahakama Kuu, uliotolewa na Jaji Sivangilwa Mwangesi, aliyemvua ubunge kutokana na kesi aliyokuwa amefunguliwa.

Akiwasilisha hoja mbele ya jopo hilo la majaji linaloundwa na Jaji Sanda Mjasiri, Jaji Mussa Kipenka na Jaji Profesa Juma Ibrahim, Wakili Komomogolo alidai Jaji Mwangesi hakuainisha kilichotokea katika chumba cha majumuisho kilikuwa ni vurugu au mzozo wa maneno.

Wakili Kimomogolo alidai kwamba, katika hukumu yake, Jaji Mwangesi pia aliongeza neno ambalo halikuwa katika kuelezea kilichotokea ndani, lakini pia alijielekeza katika ushahidi wa shahidi wa tano ambaye ni Mkuu wa Polisi Wilaya ya Longido.

“Katika ushahidi wao, hapakuwa na ushahidi wa kufanyika vurugu, lakini pia kinachoitwa vurugu bado kisingeweza kusababisha matokeo kushindwa kutangazwa,” alidai Wakili Kimomogolo.

Akifafanua hoja nyingine, Wakili Kimomogolo alidai kwamba, Jaji Mwangesi katika uamuzi wake hakufafanua ni kwa vipi mazingira ya chumba cha majumuisho yaliathiri ujumuishaji wa matokeo.

Alidai kwamba, kutokana na hoja zilizowasilishwa mbele ya jopo hilo, ni maoni yake Jaji Mwangesi hakujielekeza vema na ipasavyo kwenye misingi ya kisheria.

Kutokana na sababu hizo, aliliomba jopo hilo la majaji watengue uamuzi wa Jaji Mwangesi na watamke kuwa, muomba rufaa ambaye ni Nangole, alichaguliwa kihalali na arejeshewe ubunge wake.

“Tunaiomba pia mahakama hii kufuta taarifa ya kutangaza Jimbo la Longido lipo wazi iliyopelekwa kwa Mkurugenzi wa Halmashauri ya Longido. Lakini pia wajibu rufaa walipe gharama za kesi,” alidai Wakili Kimomogolo.

Baada ya kusikilizwa hoja hizo, mahakama hiyo iliahirishwa kwa muda wa dakika 45 ili kutoa fursa ya kuendelea kusikiliza hoja za mjibu rufaa ambaye ni Dk. Steven Kiruswa, anayewakilishwa na Wakili Dk. Masumbuko Lamwai.

Awali katika shauri hilo, Dk. Lamwai aliwasilisha pingamizi akiomba rufaa hiyo itupiliwe mbali, kutokana na kufunguliwa kimakosa kwa kushindwa kumjumuisha Mwanasheria Mkuu wa Serikali pamoja na msimamizi wa uchaguzi.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles