28.6 C
Dar es Salaam
Tuesday, March 19, 2024

Contact us: [email protected]

Namna ya kuwafanya watu wafurahie mafanikio yako

Na CHRISTIAN BWAYA

BINADAMU kwa hulka yake anapenda kufanikiwa. Tangu enzi na enzi, mwanadamu, tofauti na viumbe wengine, ana ndoto na matamanio anayojitahidi kuyafikia. Matamanio hayo yanapofikiwa, huyahesabu kama mafanikio.

Ingawa tunatofautiana vile tunavyoyachukulia mafanikio, ni wazi kila mtu ana ndoto na matamanio yanayomhamasisha kufanya kazi kwa bidii.

Kuna wengine wanachukulia wingi wa mali zinazowawezesha kuishi aina fulani ya maisha kuwa ndio mafanikio; wengine umaarufu katika jamii; wengine madaraka ya kuwaongoza watu; wengine nguvu walizonazo katika jamii; wengine uimara wa familia zao. Vyovyote iwavyo, kila mtu kwa namna yake, ana namna anavyoyatazama mafanikio. 

Kwa kawaida, unapofanikiwa, unapata aina fulani ya utoshelevu. Unajisikia vizuri kuvuka vihunzi vingi katika maisha na kufikia pale ulikotaka kupafikia.

Kijana aliyehitimu masomo kwenye chuo maarufu, kwa mfano, anajisikia utoshelevu kuwa baada ya jitihada za muda mrefu, hatimaye amefikia ndoto zake;

Ndivyo ilivyo kwa mwanafunzi aliyepata alama nyingi kwenye mtihani mgumu; kijana aliyepata kazi yenye heshima wakati wenzake wanahangaika kupata kazi; kujenga nyumba nzuri; kununua gari la kisasa; kusafiri kwenda mahali wanakotamani kwenda watu wengine na hata kukutana na watu fulani maarufu.

Katika mazingira ambayo ulitia bidii na kuona matunda, lazima utajisikia vizuri. 

Upande wa pili wa utoshelevu huo ni ile hali ya kujiona umewazidi wengine; kuwafanya wengine wajisikie kuzidiwa; waone tumefanya kazi kwa bidii zaidi, tumejituma zaidi kuliko wao.

Ingawa si kila aliyefanikiwa anakuwa na hali hii, lakini kuna kiwango fulani cha ukweli kuwa kwa wengine wetu, tunapima thamani ya kile tulichonacho kwa kuangalia vile tunavyowazidi watu wengine.

Ndani yetu unakuwapo msukumo wa kutamani wengine waone tulivyo bora kuliko wao. Unapokuwa na kazi ambayo si watu wengi wanayo, kwa mfano, unajisikia kufanikiwa zaidi kuliko unapofanya kazi ambayo watu wengi wanaifanya.

Maana yake kuna kaukweli kuwa binadamu tunapenda kushindana kwa kujilinganisha na wenzetu iwe wazi wazi au kwa mbinu za kichini chini. 

Hii inaweza kuwa ndiyo sababu inayoeleza kwanini watu hutumia nguvu nyingi kujigeuza kwua wahamasishaji wa mafaniki. Uhamasishaji huu, mara nyingi unafanyika kwa kuwananga watu, kuwafanya wajione ni wavivu, wasiojituma, wasioelewa maana ya mafanikio na wakati mwingine kuwakejeli wanapooneka wanategemea kuajiriwa.

Saa nyingine mtu anapofanikiwa hushindwa kuvumilia mafanikio yake yajitangaze yenyewe. Ile shauku ya kuonekana amefanikiwa ikamsukuma kutumia nguvu nyingi kutangaza kile kilichotokea.

Pengine umewahi kujiuliza inakuwaje unakutana na mtu hamjazungumza hata dakika mbili ukashangaa anaeleza mambo mengi ambayo kwa hali ya kawaida hayakuwa na ulazima wa kuyasema? Kwa nini inakuwa hivyo?

Kwa nini mtu anayepata mafanikio anatamani kila mtu asikie lakini anapofanya vibaya anatamani isifahamike?

Ingawa ni kweli kwa kusema mafanikio yetu tunajisikia vizuri zaidi lakini matokeo yake yanaweza kuwa hasi.

Badala ya watu wanaotusikia tukijisifia mafanikio kufurahia mafanikio yetu, wanajisikia vibaya. Je tatizo ni roho mbaya na chuki ya watu au sisi wenyewe kukosa busara? Nitaeleza.

Binadamu (kwa asili yake) ni mtu wa mashindano. Kimya kimya, tunashindana sisi kwa sisi. Nani ana nini na mimi nina nini. Tunajilinganisha. Ukiwa na kizuri wasichonacho wengine, unajihesabu umefanikiwa.

Lakini ukikosa kizuri walichonacho wengine, unajisikia kunyong’onyea. Unakosa amani hata kama ni katika hali halisi uko vizuri na huna sababu yoyote ya kuwa vile alivyo mwingine.  

Hulka hii ya kushindana wakati mwingine hutufanya tuwaonee wivu (na hata ikibidi kuwachukia) wale wanaoonekana kutuzidi. Unapotamani mafanikio yako yafahamike na wengine, usilisahau hilo. Kwamba unapomwambia mwenzako kile ulichonacho ni rahisi kwake kutafsiri mafanikio hayo kama udhaifu wake.

Kwamba kwa kujilinganisha na wewe atajiona yuko nyuma na hatakubali ajione ni dhaifu. Na ili asijione ni dhaifu, uwezekano ni mkubwa ‘atapambana’ na wewe kwa ama kukuchukia, kukudhalilisha.

Kwa nini? Hulka ya kushindana.

Tunachokiona hapa ni kwamba kile unachofikiri kinaweza kupandisha heshima yako machoni pa watu kisipofanyika kwa makini kinaweza kukushushia heshima yako.

Maana yake ni kwamba kabla hujawaambia watu mafanikio yako jiulize, ‘Hivi ni lazima wajue? Wakijua watanufaika? Kama ni muhimu wajue, je siwezi kuwaacha wakajua wenyewe? Hadhi yangu inategemea namna watu wanavyoniona?’

Hoja yangu ni umuhimu wa kujifunza kumudu mafanikio. Kama si lazima, usiwaumize watu kwa kuwaonesha kile unachojua hawana.

Waache waone wenyewe na ikibidi waambiane wenyewe.

Unapotumia mikakati kuwajulisha, kuwatambia, inakuwa kama mtu anayekwenda kula keki katikati ya watu wenye njaa.

Hawa wanaoshuhudia ukila keki mbele yao, wakikuchukia usiwalaumu kwa sababu umewachokoza mwenyewe.

Maana yangu ni kwamba jifunze kuwa mwangalifu unapopanda ngazi katika maisha. Unapokuwa na elimu kuliko wengine, kuwa mnyenyekevu kwa kuwaheshimu uliowazidi.

Lugha yako isioneshe kuwa unajihesabu kuwa mtu wa maana kuliko wao. Unapokuwa na madaraka na cheo, heshimu wasio na nafasi uliyonayo. Lugha na matendo yako yaheshimu hisia zao.

Unapokuwa na uwezo wa kifedha, jitahidi kuwa mnyenyekevu kwa lugha na matendo. Usiwafanye maskini wajione kama wao ndio wavivu wasiojua namna ya kutafuta fedha. Ukifanya hivyo, watu watafurahia mafanikio yako.  

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
584,000SubscribersSubscribe

Latest Articles