27.5 C
Dar es Salaam
Thursday, March 28, 2024

Contact us: [email protected]

NAMNA YA KUMLINDA KIJANA NA TABIA HATARISHI  

 

Na CHRISTIAN BWAYA


IDADI ya vijana wanaotumia vilevi na dawa za kulevya inazidi kuongezeka. Ingawa hatuna takwimu rasmi lakini hali halisi inaonesha kuwa tatizo hili ni kubwa. Tembelea vituo vya usafiri mijini, vijiwe vya vijana, utakutana na vijana wengi wenye nguvu wanaoonesha dhahiri ni walevi na wanatumia dawa za kulevya.

Sambamba na ulevi, kuna tatizo la vijana wadogo kujiingiza katika uhusiano wa kimapenzi. Tafiti mbalimbali zilizofanyika kwenye maeneo tofauti hapa nchini, zinaonesha kuwa vijana wengi wanaanza kushiriki ngono katika umri wa kati ya miaka 14 na 17. Ngono katika umri mdogo huchangia kuzorotesha maendeleo yao na wakati mwingine huchochea ongezeko la mimba za utotoni sambamba na ndoa katika umri mdogo.

Pamoja na hali kuwa hivi, ukweli wa mambo ni kwamba wazazi wengi wanatamani kuona watoto wao wanajiepusha na tabia kama hizi. Hakuna mzazi, kwa mfano, anayefurahia kuona mwanawe anayesoma shule akijihusisha na mapenzi shuleni.

“Wakati mimi ninakua, ilikuwa mwiko kabisa kwa kijana kuwa na uhusiano wa kimapenzi kabla ya ndoa,” aliniambia mzazi mmoja na kuendelea, “Tulioa tukiwa wadogo kweli, lakini hatukujiingiza kwenye mapenzi kabla ya ndoa. Tendo la ndoa lilikuwa ni zawadi ya fungate. Siku hizi mambo yamekuwa tofauti. Kijana anakujia na girlfriend nyumbani bila wasiwasi. Ngono imekuwa jambo la kawaida kabisa na vijana hawajali hata ikifahamika kwa wazazi.”

Mawazo ya mzazi huyu kimsingi hayatofautiani na mitazamo ya wazazi wengine ambao ni wazi hawatamani kuona vijana ama wanaanza kutumia madawa ya kulevya au wanajiingiza kwenye vitendo  visivyo vya kimaadili kama uasherati. Swali, hata hivyo, ni kitu gani hasa huchangia vijana kuwa na tabia hizi?

Ili kupata mwangaza wa vichocheo vya tabia hizi, ni muhimu kuelewa mahitaji makubwa ya vijana chipukizi. Kama tulivyogusia katika makala zilizopita, vijana wa umri huu wanahitaji kubwa la kujisikia ‘utu uzima’ ndani yao. Shauku ya kujiona wana hadhi sawa na watu wazima wengine, huwafanya vijana watumie nguvu nyingi kujaribu kutengeneza utambulisho unaowaweka kwenye mizania ya ‘utu uzima.’ Hitaji la hadhi ya utu uzima linakwenda sambamba na mihemuko ya mwili inayochochewa na ongezeko la homoni za uzazi. Mihemuko hii, kama tunavyofahamu, nayo ina nafasi kubwa katika kuumba utambulisho wa kijana.

Namna gani kijana huyu anakidhi matarajio ya watu anaowaona kuwa muhimu kwake na hivyo kujitambulisha nao, inachangia kwa kiasi kikubwa kuamua atakuwa mtu wa aina gani. Bahati mbaya, hata hivyo, watu ambao kijana huyu anawathamini na kujitambulisha nao, wanaweza kuwa ni wale ambao wakati mwingine mienendo yao inakwenda kinyume na matarajio ya wazazi. Katika mazingira ambayo wazazi na watu wengine hawajaweza kugusa moyo wa kijana huyu, inakuwa rahisi kijana huyu kujenga utambulisho wa hatari unaokidhi matarajio ya watu waliopotoka kimaadili.

Maana yake kuwa vijana chipukizi hujiingiza katika tabia mbovu kama ulevi na uasherati kwa sababu ndani yao kunaishi ombwe la kutafuta kutambulika, ombwe ambalo kwa bahati mbaya hakuna anayelijaza isipokuwa watu wasiojulikana. Ndio kusema, ikiwa mzazi anahitaji kumsaidia kijana wake, kazi kubwa anayohitaji kuifanya mapema ni kuweka mazingira yatakayokuwa msingi wa kujaza ombwe la kutambulika alilonalo kijana. Tutaanzia hapo katika makala inayofuata panapo uzima.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles