29.2 C
Dar es Salaam
Wednesday, April 24, 2024

Contact us: [email protected]

NAMNA YA KUJIFUNZA KUBADILI TABIA

Na CHRISTIAN BWAYA



KUJIFUNZA tabia mpya kunaweza kuwa kazi ngumu kama ilivyo kujaribu kuacha tabia usiyoipenda. Sababu ni kwamba mwili, kama ulivyo ufahamu wa mtu, unapenda kufanya kilichozoeleka. Nakumbuka nilipoazimia kuanza kufanya mazoezi kila siku alfajiri nilipata shida kuzoea. Ilinichukua muda mrefu kidogo mazoezi kuwa sehemu ya maisha yangu ya kila siku.

Kila nilipojaribu kuamka alfajiri, nilikabiliana na mpambano mkali na mwili usiotaka kuamka. Japo nilikuwa na nia ya dhati ya kufanya mazoezi, bado kiuhalisia haikuwa rahisi. Nilijikuta nikijipa sababu za kutosha kuahirisha kwenda kwenye mazoezi kwa matumaini kuwa ningeendelea kesho yake. Wakati mwingine hiyo kesho ilifika baada ya wiki moja au zaidi.

Baada ya muda mrefu wa kupambana na upinzani wa ndani kwa ndani, niliamua kuweka malengo mahususi yatakayonisukuma kujenga tabia mpya ya mazoezi. Kwa hiyo, pamoja na ugumu wake, niliazimia mazoezi yatakuwa sehemu ya ratiba yangu ya kila siku. Kwamba ikipita siku sijafanya mazoezi, basi hiyo itamaanisha ninaelekea kushindwa.

Watu wengi hushindwa kujenga tabia mpya wanazozihitaji kwa sababu hawazifanyi tabia hizo kuwa sehemu ya mambo wanayoyafanya kila siku. Wanafikiri kutamani tu kujenga mazoea mapya kunakuja bila jitihada zozote. Matokeo yake, wanaendelea kuwa na tabia zile zile miaka nenda – rudi.

Ikiwa unataka kuanza kusoma vitabu, kwa mfano, hakikisha usomaji unakuwa sehemu ya ratiba yako ya kila siku. Siku isipite hujasoma. Kwa kawaida, mwanzoni akili na mwili vitakupa upinzani mkali kwa sababu havijazoea tabia hiyo mpya. Siri hapa ni kuendelea kufanya kile kile unachotaka kukifanya bila kujali unajisikiaje.

Lakini pia, kuna tatizo la kuanza tabia mpya kwa ‘fujo.’ Nakumbuka siku ya kwanza tu nilikimbia kwa kasi kubwa utafikiri nilikuwa kwenye mashindano ya mita 400. Kitu ambacho sikukifahamu ni kwamba kwa kufanya hivyo niliuchosha mwili kwa kuulazimisha kufanya kitu ambacho hakijazoeleka. Siku ya pili ilikuwa vigumu kuamka.

Mwili wote ulikuwa unauma. Nilikuja kujifunza baadae kwamba sikuwa na sababu ya kukimbia kwa kasi kubwa. Nilihitaji kukimbia kwa mwendo mdogo usiochosha na kwa umbali mdogo. Kwa kufanya hivyo, niliuwezesha mwili kuzoea tabia mpya.

Unapambana kuanzisha tabia ipi mpya? Huenda unajaribu kujenga desturi ya maombi kila unapoamka; kufanya sala kabla hujala chakula; kukamilisha kazi ndani ya muda uliopangwa; kujibu ujumbe unaotumiwa kwa wakati. Mahali pa kuanzia ni kujipa muda wa kuanza kidogo kidogo. Usitake kufanya kwa ukamilifu ndani ya muda mfupi. Jiruhusu kupata mafanikio hatua kwa hatua.

Wakati mwingine tunajikuta ‘tunaishangaza’ akili kwa sababu tunataka badiliko liwe kubwa ndani ya muda mfupi. Tunapoona tabia mpya haionekani kuleta matunda kwa wakati tunataka tamaa. Tunataka ‘matokeo makubwa sasa.’ Tunasahau waswahili walisema, ‘Haraka haraka haina baraka.’ Mambo mazuri hayahitaji haraka. Kujifunza kuzizoesha fahamu zetu kuzoea tabia mpya hatua kwa hatua ni jambo la msingi.

Hapa ndipo tunapohitaji kujifunza jambo la tatu. Unapoanzisha tabia mpya lazima kujiwekea mfumo mzuri wa motisha. Tabia mpya isipokupa motisha itakuwa vigumu kwako kuendelea nayo. Kuna namna mbili za kujipa motisha. Mosi, kuyaona matokeo ya kile unachojaribu kujifunza. Jiulize kwa nini unajaribu kujenga tabia mpya? Kilichonihamasisha kufanya mazoezi ni matokeo. Nilijiona nikidhibiti uzito wa mwili. Hiyo ilikuwa hamasa tosha.

Lakini pili, weka utaratibu wa kujikumbusha kile unachojaribu kujifunza. Fahamu zetu zina tabia ya kupuuza jambo tusilolipa uzito. Namna nzuri ya kujikumbusha ni kujisemea maneno yanayosisitiza mpango ulionao. Andika maneno yatakayokukusha mazoea mapya mahali pa kuonekana. Bandika vikatarasi kwenye kioo cha kabati lako; mlango wa jokofu lako; kwenye dashboard ya gari yako. Kokote unakoweza kuona maneno hayo, bandika. Kwa namna hii utajikumbusha kwa urahisi.

Pia, unaweza kuwachagua watu makini unaowaamini ukawaambia unachojaribu kukijenga. Mimi nilimwambia mke wangu. Ingawa na yeye alilazimika kuungana nami kufanya mazoezi, kumwambia kunisaidia kuwajibika zaidi kuliko kama ningekuwa najifanyia mazoezi kwa siri. Mshirikishe rafiki yako au mtu unayemini atakayekuwa hakimu pale utakapojisahau.

Baada ya muda, utashangaa unaifanya tabia mpya bila kufikiri. Inakuwa sehemu ya maisha yako.
Christian Bwaya ni mnasihi na mhadhiri wa Saikolojia Chuo Kikuu cha Kikatoliki Mwenge (MWECAU). Unaweza kuwasiliana naye kwa simu 0754870815 au barua pepe [email protected] kwa msaada zaidi.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles