27.2 C
Dar es Salaam
Tuesday, April 16, 2024

Contact us: [email protected]

Naibu Spika amwita mbunge bwege bungeni

tulia-acksonNA BAKARI KIMWANGA, DODOMA

NAIBU Spika wa Bunge, Dk. Tulia Ackson, jana amezua sintofahamu bungeni baada ya kumwita bwege Mbunge wa Kilwa Kusini, Seleman Bungara (CUF).

Dk. Tulia alimwita bwege mbunge huyo wakati wa kuchangia mjadala wa hotuba za bajeti za Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) pamoja na Utawala Bora.

Kilichomponza mbunge huyo ni hatua yake ya kusimama na kuhoji Bunge kutorushwa moja kwa moja kwenye runinga wakati Naibu Spika akitoa ufafanuzi kwa wabunge kuhusu mjadala uliokuwa ukiendelea.

“Bwege acha ubwege wako hapa… Bwege acha ubwege,” alisema Dk. Tulia huku akionya hatua ya kuzomea ndani ya Bunge.

Baada ya Dk. Tulia kutoa kauli hiyo, mbunge huyo alimjibu kwa kusema si ajabu kumwita bwege kwa sababu hilo pia ni jina lake.

“Bwege ndiyo jina langu, kwani kuna ajabu gani, kwani wewe mwanamume? Ukiitwa mwanamume utajisikiaje?” alisema mbunge huyo ambaye ni maarufu kwa jina la ‘Bwege’.

Hivi karibuni, mkazi wa Mtaa wa Olasit jijini Arusha, Isaac Habakuk Emily, alifunguliwa mashtaka na Jamhuri akidaiwa kuweka kwenye ukurasa wake wa Facebook ujumbe ulioonyesha kumdhihaki Rais John Magufuli kwa kumwita bwege, huku akijua kufanya hivyo ni kosa kisheria.

Ujumbe huo ulisomeka: “Hizi siasa za maigizo, halafu mnamfananisha huyu bwege na Nyerere wapi buana”.

 

NAIBU SPIKA ALIPULIWA

Awali Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema (Chadema), alimlipua Naibu Spika huyo akidai kwamba amejipa mamlaka ya Spika wa Bunge, Job Ndugai kinyume cha utaratibu.

Lema alisema kiongozi huyo amekuwa akifanya mambo yenye kuhitaji mamlaka ya Spika ikiwamo kwenda Ikulu kwa Rais Dk. John Magufuli, kupeleka Sh bilioni 6 za Bunge hali ya kuwa hakuna kikao cha Kamisheni ya Utumishi ya Bunge kilichopitisha suala hilo.

“Inashangaza sana mmetoa hela za Bunge hapa, mnaita utawala bora, mmeutoa wapi? Mmekwenda kukabidhi fedha za Bunge kwa Rais (Dk. Magufuli), Spika hajui. Spika naye anasoma kwenye WhatsApp. Spika anaangalia mko Ikulu, yuko anaumwa, anasoma kwenye WhatsApp.

“Mmefanya maamuzi ya fedha za Bunge bila kuishirikisha Kamisheni ya Bunge, mnasema utawala bora, uko wapi?”

Mbunge huyo wa Arusha Mjini, alikwenda mbali zaidi akimtuhumu Naibu Spika huyo kutwaa madaraka ya Spika wa Bunge, huku akikosoa kitendo cha Serikali ya Awamu ya Tano chini ya Rais Magufuli kuongozwa bila mwongozo wa utekelezaji majukumu ya mawaziri (Instrument).

“Na wewe siku hizi unajifanya wewe ndio Spika, Serikali haifuati misingi ya utawala bora. (Sospeter) Muhongo alikwenda Bandari, akamwambia yule mama afungue koki za mafuta, mnafukuza aliyeagizwa badala ya kumchukulia hatua aliyemwagiza,” alisema Lema.

Akijibu makombora ya Lema wakati akiahirisha mkutano wa Bunge jana, Dk. Tulia alisema: “Wabunge tusitafute maneno ya kumwekea Spika mdomoni, tusigombanishe viongozi bila sababu.”

 

Mchungaji Msigwa

Naye Mbunge wa Iringa Mjini, Mchungaji Peter Msigwa (Chadema), akichangia bajeti hizo za TAMISEMI na Utawala Bora, alidai kuwa amewarekodi mawaziri wa Rais Magufuli kwenye mgahawa wa Bunge, wakilalamikia utendaji wa Serikali ya awamu ya tano.

Alisema kuwa suala la utawala wa sheria kuanzia na bajeti si la msingi wala takwa la kisheria.

“Tangu Serikali hii imeingia madarakani, kuna mambo ambayo imeyakanyaga, halafu leo zinaombwa fedha zaidi ya bilioni 800 za utawala bora ambao haupo, Serikali hii imeanza kufanya kazi kienyeji, mawaziri wote hawa wanafanya kazi kienyeji bila kufuata mwongozo, ni kukanyaga sheria, kwahiyo hawa mawaziri hawa ni mawaziri kivuli kwa sababu walikuwa wanatoa maagizo bila kufuata sheria na huo si utawala bora,” alisema.

Alisema hivi sasa mawaziri hao ndio wamekuwa wakilalamika kila kona jambo ambalo inaonyesha kwamba Serikali imeshindwa kazi.

“Hawa mawaziri wamekuwa wakija kwetu kwenye chai na kulalamika kuhusu utendaji wa Serikali, na ushahidi upo tumewarekodi, na wakitaka ushahidi upo, hata kwa majina tunaweza kuwataja humu ndani mmoja baada ya mwingine, sasa tumekuwa na Serikali ambayo watu wake wamekuwa ni wanafiki,” alisema Msigwa.

Wakati mbunge huyo akiendelea kuchangia, alisimama Naibu Waziri wa Afya, Ustawi wa Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dk. Hamis Kigwangalla, ambaye aliomba mwongozo wa Naibu Spika kuhusu kauli hiyo dhidi ya mawaziri wanaolalamikia utendaji wa Serikali.

“Mhemishiwa Naibu Spika ninasimama hapa kwa Kanuni ya 68 (7) za Bunge, ninaomba mbunge anayeendelea kuzungumza athibitishe kauli yake kwamba kuna baadhi ya mawaziri wanapingana na Serikali, sasa awataje hapa ili tuwajue wanafiki,” alisema Dk. Kigwangalla.

Kutokana na mwongozo huo wa Naibu Waziri huyo, vijembe vilitawala kati ya upande wa upinzani na ule wa chama tawala CCM, ambapo Naibu Spika wa Bunge, Dk. Tulia, alisema kwamba angeutoa mwongozo huo kwa mujibu wa kanuni ya 63 kifungu cha 4 wakati mwingine na kuruhusu mjadala kuendelea.

Akiendelea na mjadala huo, Mchungaji Msigwa alisema kwamba tangu Bunge la tisa chini ya Spika wa Bunge mstaafu, Samuel Sitta, suala la utawala bora lilikuwa likitiwa uzito ikiwemo Bunge kuonyeshwa moja kwa moja kwa sababu ni chombo cha wananchi.

“Ninashangaa Bunge ni mali ya wananchi inakuaje Serikali inaweka usiri hali ya kuwa huu si mkutano wa unyago, ukiona Serikali inajivuna kwa uwazi halafu inakwenda kinyume hiyo ni Serikali oga na inaficha madudu.

“Leo hata Magufuli (Rais Dk. John) akidondosha kijiko mnabaki mnapiga makofi na kuufyata,” alisema.

 

NAPE

Baada ya Msigwa kumaliza kuchangia, alisimama Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Nape Nnauye, na kuomba mwongozo kuhusu kauli ya Msigwa kuwa Serikali imedhibiti Bunge na suala la matangazo ya moja kwa moja.

“Mheshimiwa Naibu Spika, nasimama hapa kwa kanuni ya 68 (8), maneno yaliyosemwa na mbunge ni ya uongo,” alisema Nape huku wabunge wa upinzani wakimzomea.

Alisema si kwamba Bunge limewazuia waandishi wa habari ila wapo wanaripoti matukio yote yanayoendelea ndani na nje ya Bunge.

 

Mbunge arusha kijembe

Licha ya maelekezo kadhaa ya Naibu Spika, alisimama Mbunge wa Konde, Khatib Said Haji (CUF), alisema kwamba anashangazwa na taarifa za Waziri wa Habari Nape Nnauye.

“Najua ni Ukawa mwenzangu anayechangia ila aliyechukua uamuzi wa kushauri Rais ni huyo Vuvuzela Nape,” alisema Khatibu.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles