31.2 C
Dar es Salaam
Friday, March 29, 2024

Contact us: [email protected]

Nafasi ya Mbowe huru

LEONARD MANG’OHA -DAR ES SALAAM

NAFASI ya Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Freeman Mbowe iko huru.

Hatua hiyo, inatokana na chama hicho kutangaza rasmi kuanza mchakato wa uchaguzi wa viongozi wakuu ngazi ya taifa unaotarajia kufanyika Desemba 18.

Uchaguzi huo utahusisha nafasi ya mwenyekiti wa chama ngazi ya taifa, makamu mwenyekiti Tanzania Bara, makamu mwenyekiti Zanzibar na wajumbe wanane wa Kamati Kuu, wakiwamo sita kutoka Tanzania Bara na wawili kutoka Zanzibar.

Nafasi nyingine zitakazowaniwa ni wajumbe wanane wa Kamati Kuu ya chama ambapo upande wa Tanzania Bara, utakuwa na wajumbe sita wakiwamo wanaume watatu na wanawake watatu, huku upande wa Zanzibar ukiwa na mwanamume mmoja na mwanamke mmoja.

Akizungumza na waandishi wa habari makao makuu ya chama hicho Dar es Salaam jana, Katibu Mkuu wa Chadema, Dk. Vicent Mashinji, alisema uchukuaji na urejeshaji fomu za kugombea nafasi mbalimbali ulianza jana na utafikia ukomo Novemba 30.

Dk. Mashinji alisema katika Baraza la Wazee, nafasi zitakazoshindaniwa ni pamoja na mwenyekiti, makamu wenyeviti wawili – mmoja kutoka Tanzania Bara na mmoja Zanzibar, katibu, naibu katibu (Bara), naibu katibu (Zanzibar), mweka hazina, wajumbe watano watakaowakilisha katika Baraza Kuu la chama ambapo wanne watatoka Tanzania Bara na mmoja Zanzibar.

Alisema nafasi nyingine itakayowaniwa katika baraza hilo ni wajumbe 20 wawakilishi wa mkutano mkuu wa chama taifa ambao 15 watatoka Tanzania Bara na watano Zanzibar.

“Katika Baraza la Wanawake (Bawacha) nafasi zitakazowaniwa ni mwenyekiti taifa, makamu mwenyekiti Tanzania Bara, makamu mwenyekiti Tanzania Zanzibar, katibu taifa, naibu katibu Tanzania Bara, naibu katibu Tanzania Zanzibar, mweka hazina, mratibu wa uenezi, wajumbe watano wawakilishi kwenye Baraza Kuu la chama kwa uwiano wa wanne kutoka Tanzania Bara na mmoja Tanzania Zanzibar.

“Wajumbe 20 wawakilishi wa mkutano mkuu wa chama taifa kwa uwiano wa wajumbe 15 kutoka Tanzania Bara na wajumbe watano kutoka Tanzania Zanzibar.

“Katika Baraza la Vijana (Bavicha), ni mwenyekiti taifa, makamu mwenyekiti Tanzania Bara, makamu mwenyekiti Tanzania Zanzibar, katibu taifa, naibu katibu Tanzania Bara, naibu katibu Tanzania Zanzibar, mweka hazina, mratibu wa uenezi, wajumbe watano wawakilishi kwenye Baraza Kuu la chama kwa uwiano wa wanne kutoka Tanzania Bara na mmoja Tanzania Zanzibar.

“Wajumbe 20 wawakilishi wa mkutano mkuu wa chama taifa kwa uwiano wa wajumbe 15 kutoka Tanzania Bara na wajumbe watano kutoka Tanzania Zanzibar. Kwa hiyo tunawakaribisha wanachama wa Chadema wenye sifa ya kugombea nafasi mbalimbali ngazi ya taifa waanze kuchukua fomu za kugombea kuanzia leo (jana),” alisema Dk. Mashinji.

Alisema Desemba 7, Kamati Kuu itakutana ili kuchuja na kupitia majina ya wale wote walioomba nafasi mbalimbali kufanya uteuzi wa awali kwa nafasi ya mwenyekiti na makamu mwenyekiti na kufanya uteuzi moja kwa moja kwa wagombea wa nafasi mbalimbali katika mabaraza ya chama hicho.

Dk. Mashinji alisema Desemba 8, watafanya kikao cha Kamati Tendaji ya Baraza la Wazee na Kamati Tendaji ya Baraza la Vijana na kufuatiwa na mkutano mkuu wa mabaraza hayo Desemba 9 ili kuchagua viongozi wao ngazi ya taifa.

Alisema Desemba 10 kutakuwa na kikao cha Kamati Tendaji ya Baraza la Wazee na Kamati Tendaji wa Bazara la Vijana.

Desemba 11 kutakuwa na Kamati Tendaji ya Baraza la Wanawake (Bawacha) na kutuatiwa na mkutano mkuu wa baraza hilo siku inayofuata ili kuchagua viongozi wake wakuu na Desemba 13 Kamati Tendaji ya baraza hilo itakutana kwa mkutano mkuu.

“Baada ya shughuli hii ya uchaguzi kwenye mabaraza na mikutano itakayokuwa imefanyika kupitia mabaraza, Desemba 16 kutakuwa na kikao cha Kamati Kuu ambayo itafanya uteuzi wa viongozi wa chama ngazi ya taifa.

“Siku inayofuata tutakuwa na mkutano mkubwa wa baraza la chama ambalo ndilo litafanya uteuzi wa mwisho wa wagombea kama mwenyekiti na makamu wake kwa ajili ya kupeleka hayo majina kwenye mkutano mkuu wa chama ambao utafanyika Desemba 18 na kufanya uchaguzi.

“Kwa hiyo wale waliokuwa wanafikiria Chadema haina mpango wa kufanya uchaguzi, Chadema haina ratiba ya uchaguzi, hii ndiyo ratiba yetu rasmi ya uchaguzi,” alisema Dk. Mashinji.

Alisema watatumia mchakato huo wa uchaguzi wa ndani kutoa mfano wa jinsi demokrasia inavyotakiwa kuwa hapa nchini.

“Katika ujenzi wa demokrasia lazima kuwe na ushirikishwaji mkubwa wa wananchi. Sasa sisi tumewashirikisha wanachama wetu kuanzia ngazi ya chini ya chama, kwa katiba yetu ni eneo la kitongoji au mtaa katika miji, ambao hao wameweza kuchagua viongozi wao na viongozi wamechaguliwa kwa uwakilishi mpaka kwenye ngazi ya kanda ambayo itafanya hivi karibuni na baadaye tutakwenda kwenye uchaguzi wa taifa,” alisema Dk. Mashinji.

Alisema kutokana na kufanyika vizuri kwa uchaguzi wa viongozi wa ngazi za chini, kumewawezesha kuweka wagombea zaidi ya asilimia 80 wa nafasi zote katika Uchaguzi wa Serikali za Mitaa jambo ambalo liliwafanya wapinzani wao kuingiwa hofu na woga na kuamua kuwaengua.

Mbowe alichaguliwa na mkutano mkuu kushika nafasi hiyo mwaka 2014 kwa kupata kura 749 sawa na asilimia 97.3 na kumshinda mpinzani wake ambaye hakuwa na nguvu kubwa, Gambaranyera Mongateo aliyepata kura 20 sawa na asilimia 2.5.

Kama Mbowe atapitishwa kugombea tena, hii itakuwa mara yake nne kuwania kiti hicho.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles