Nafasi ya Benki  katika kujenga Uchumi wa Viwanda

0
804

Na Dr. Bill Kiwia

BENKI ni moja kati ya taasisi za fedha zinazotoa mchango mkubwa katika kujenga uchumi wa nchi.

Mfumo wa taasisi ulianza tangu karne ya 3 kabla ya kuzaliwa Kristo lakini uendeshaji wa benki kama taasisi ya kuweka na kuhifadhi fedha na pia kutoa na kukopesha ulianza karne ya 16.

Wakati ule walikuwako wafuaji na wawekaji wa dhahabu wakifahamika kama “goldsmith” waliokuwa wakiweka na kupokea kwa niaba ya wateja wao. Mabadiliko hayo yaliendelea kudumu hadi karne ya 20 ambapo palifanyika mabadiliko makubwa sana ya kimfumo na kiuendeshaji wa taasisi ya benki baada ya makubaliano yaliyofanyika Bretton Woods, USA (Bretton Woods Accord) mwaka 1944.

Sekta ya benki nchini Tanzania ilianza kufanya kazi mwaka 1905 wakati wa utawala wa kikoloni wa kijerumani na mojawapo kati ya benki za awali nchini ilikuwa benki ya Ujerumani iliyojulikana kama Deutsche Ostafrikan Bank. Benki hii ilikuwa ikisimamia na kuratibu fedha zitokanazo na biashara zilizokuwa zikifanywa na wajerumani nchini wakati wa ukoloni.

Hata hivyo haikukaa sana na baada ya vita ya kwanza ya dunia mwaka 1920 na kuendelea, tulianza kuona huduma za kibenki zikiongezeka na kuwa na mabenki mengine nchini kama Barclays, The National and Grindlay, Handlesbank fur Ostafrika, DCO Standard Bank ya Afrika Kusini, Banque de Congo Belge, Niederlandische Handel-Maatschappij, Bank of India na Bank of Baroda, Tanganyika Post Office and Saving Bank (TPOSB), Ottoman Bank ya Uturuki n.k.

Benki zote hizi zilianza kutoa huduma zao nchini mwetu na hadi tunaeleka Uhuru tulikuwa na mabenki zaidi ya 10 yaliyokuwa yanafanya biashara zake nchini.

Hali ya ustawi wa mabenki iliendelea hata baada ya uhuru na kabla kutaifishwa kwa sekta hii kufuatia Azimio la Arusha ambapo idadi ya mabenki iliongezeka zaidi kwa kuletwa kwenye soko mabenki ya wazawa kama National Cooperative Bank, Peoples’ Bank of Zanzibar na Tanzania Bank of Commerce. Hata hivyo, kufuatia kupitishwa kwa Azimio la Arusha mnamo mwaka 1967, kulitokea mabadiliko makubwa kwenye sekta ya biashara ya benki baada ya kuletwa kwa sera za ujamaa na kupelekea kutaifishwa kwa sekta ya benki na kusababisha mabenki kupungua na kubakia benki chache nchini.

Hali hiyo iliendelea hadi baada ya mabadiliko ya sera za kiuchumi ambapo mnamo mwaka 1991 sekta ya benki ilirudi katika hali ya kuwa sekta ya ushindani na kuruhusu benki binafsi kushindana kwenye soko huria.

Hii ni kutokana na mapendekezo ya kamati ya Jaji Nyirabu (Nyirabu, 1988) iliyoainisha changamoto mbali mbali zinazoikabili sekta husika katika kutekeleza majukumu yake kama vile kukosekana kwa ufanisi na tija na muingiliano wa uendeshaji benki.

Baadhi ya benki kama benki ya nyumba (Tanzania Housing Bank) zilifilisika kabisa wakati benki zingine kama Benki ya Taifa ya Biashara zilikumbwa na misukosuko ya kibiashara.

Ili kuleta tija ya uendeshaji na mafanikio kwenye sekta ya benki mapendekezo yakawa ni kuruhusu biashara huria ya sekta ya benki.

Hivyo,   kuanzia mwaka 1991 hadi sasa kumekuwa na ongezeko kubwa la mabenki nchini (Sekta sasa hivi ina mabenki 59 kwa mujibu wa rIpoti ya Benki Kuu ya mwaka 2016). Ongezeko hili linaweza kupelekea mtazamo kwamba sekta inakuwa kwa kasi sana na mafanikio makubwa sana kwa kuangalia thamani ya rasilimali ambazo benki wanazo na mitaji inayoongezeka kila siku. Mfano, mwaka 2000 rasilimali za sekta husika zilikuwa takribani Shilingi Trilioni 1.6 ikilinganishwa na sasa ambapo zimefikia takribani Shilingi Trilioni 27.9.

Vilevile kiwango cha pesa kilichowekwa na wateja kimeongezeka sana toka Bilioni 988 mwaka 1999 hadi kufikia Trilioni 23.6.

Ukuaji huu unahitaji pongezi ya hali ya juu hasa ukifikiria kiwango cha ukuaji huu pia kunamaanisha usambazaji wa mitaji kwa wakopaji na ukuzaji wa sekta zinginezo katika uchumi zinaongezeka.

Pamoja na ukuaji huu wa kasi kuna changamoto zinazoendelea kuwepo kwenye sekta ya kibenki ambazo ninaweza kuzianisha katika maeneo makuu matatu:

  1. Ufahamu mdogo wa bidhaa zitolewazo na benki (Elimu ya fedha).

Elimu ya ufahamu wa huduma za fedha bado iko chini ukilinganisha na uhalisia wa mahitaji ya huduma husika. Inakisiwa mahitaji ya elimu ya matumizi ya fedha ni kubwa kuliko inavyotarajiwa kwani huduma za fedha bado zipo katika kiwango cha chini sana nchini ukilinganisha na mahitaji.

Utafiti wa Finscope mwaka huu unaonyesha utumiaji wa huduma za fedha umeongezeka kwa asilimia 14 kutoka asilimia 51 hadi asilimia 65 ya watanzania. Kwa takwimu hizi inaonekana matumizi ya huduma za fedha yameongezeka kidogo ikizingatiwa kwamba mahitaji ya huduma za fedha (financial needs) nchini yako kwa kiwango kikubwa ambapo kwenye maeneo kama ya vijijini, huduma za fedha zimekuwa zikihitajika kwa kiwango cha hali ya juu kulinganisha na mijini.

Asilimia 59 ya watanzania wanapata kipato kutokana na shughuli zao za kiuchumi kama biashara na kilimo na wengi wao kipato hicho wanakitumia kwenye mahitaji kama chakula, malazi na huduma nyinginezo za kijamii. Asilimia 7 ya kipato hicho kinawekwa kwenye akiba kwa ajili ya matumizi ya baadae ya kijamii.

Benki nchini zinatakiwa ziwekeze kwenye kutoa elimu zikishirikiana na taasisi za elimu kuelimisha manufaa ya huduma ya benki kwenye jamii.

Huduma za kibenki zimebadilika sana tangu wakati wa mkutano wa Bretton. Sasa benki zimekuwa zaidi kama msaidizi katika maisha ya kila siku ya binadamu kuanzia katika kutoa ushauri hadi kusaidia kupanga matumizi ya kila siku ya Mtanzania.

Jamii inahitaji kufahamu hili kwani linaweza kutoa nafasi ya watanzania wengi zaidi kujua faida mbalimbali zipatikanazo kwa kutumia huduma hizo. Hili jambo ni la msingi sana kwa faida ya mabenki na jamii kwa ujumla kwani uwepo wa benki unategemea mahitaji ya huduma za kibenki nchini.

 

  1. Mkusanyiko wa Bidhaa zinazolingana au Kufanana Kwenye Soko.

Sekta ya benki ni sekta yenye ubunifu tangu ilivyoanza miaka 3000 kabla ya Kristo. Kipindi chote sekta hii imebadilika toka kuwa watunza fedha (safe custody) kuwa sekta mdau katika kukuza uchumi wa nchi duniani.

Kwa sasa benki zinafanya mambo mengi kuanzia kutunza fedha, kukopesha, kushauri, bima na kadhalika; jambo linaloonyesha sekta inaenda ikibadilika kutokana na hali ya mazingira ya uchumi wa nchi husika. Benki zimetoka kwenye maofisi na kuhamia kwenye mifuko ya suruali zetu kwa maana kwamba zimehamia kwenye simu zetu kwa kutumia teknolojia.

Huduma za benki sasa zimekuwa zaidi kwenye kupunguza usumbufu kwa wateja na kutoa huduma kwa haraka na umakini zaidi. Ndio maana siku hizi tunaona kuna kadi za plastiki na huduma za benki kwa simu na mtandao. Vyote hivi vinalenga kuondoa usumbufu kwa wateja.

Tanzania nayo haijaachwa nyuma kwani kwa muda wa miaka 10 au zaidi iliyopita teknolojia imekuwa ni chachu ya ubunifu kwa sekta ya benki.

Ila kuna haja ya ubunifu kupanuka zaidi kwani benki bado zina fursa ya kubuni njia mbadala na bora za kukuza biashara zao. Mfano Finscope 2017 inaonyesha kwamba watanzania wengi huwa wanawekeza asilimia 2 hadi 3 ya kipato chao katika ardhi na nyumba.

Benki kwa kushirikiana na serikali wanaweza kubuni mikopo ya kununua nyumba za gharama nafuu kuweza kupunguza uhaba wa nyumba nchini.

Vile vile huduma za fedha kama vile mikopo kwa wanafunzi, wafanyakazi na sekta ya ujenzi ni chachu itakayoweza kuchochea maendeleo katika nchi kwani itaongeza manunuzi na kukuza biashara nchini.

Hata hivyo ni muhimu ubunifu huu uendane na elimu ya huduma ya fedha kwa watumiaji.

 

  1. Ukuaji wa Sekta ya Teknohama na Changamoto zake

Teknolojia ni moja kati ya mambo ambayo yamechangia sana kubadilika kwa sekta ya fedha na benki kwa ujumla. Mfano mmoja wa faida ya teknolojia ni kwamba imekuza kiwango cha utumiaji wa huduma za benki toka asilimia 11 hadi kufikia asilimia 65 kutoka mwaka 2006 hadi 2017.

Ongezeko hili kwa kiasi kikubwa limechangiwa na ukuaji na uwepo wa teknolojia ya mtandao ambayo imechangia kwa kiwango kikubwa upatikanaji wa huduma za fedha katika maeneo mbali mbali nchini.

Hata hivyo teknohama ina changamoto zake kwani ubunifu wa kuunganisha teknohama na mitandao ya benki inabidi uangaliwe kwa umakini zaidi kuepuka mifano kama ya nchini Bangladesh na kwingineko ambako teknohama ilisababisha hasara kwenye sekta ya benki.

Mabadiliko ya kisera na vipaumbele vya nchi vinaweza pia kuwa chachu ya maendeleo katika uchumi nchini. Sekta ya benki ni moja ya sekta muhimu sana katika kuleta maendeleo nchini.

Benki zinaweza kuwa chachu ya kuchangia maendeleo kwa kutoa huduma kama mikopo kwa viwanda vidogo na vikubwa. Lakini huduma ya mikopo na kuhifadhi fedha ni huduma zilizopitwa na wakati kwani benki sasa zimejibadili na kuwa mdau wa maendeleo kwa watu pamoja na maendeleo yao.

Sasa benki ziko kuanzia kwenye mitandao hadi kwenye mifuko ya watu. Benki zimekuwa na huduma zenye wigo mpana kuanzia ushauri, uwekezaji, usimamizi (wealth management), biashara, mikopo na huduma za bima. Haya yanaweza kuchangia maendeleo ya nchi kwa ujumla.

(Dr. Bill Kiwia ni Mhadhiri wa Chuo Cha Usimamizi wa Fedha (IFM)  na Mtaalamu wa TIOB.)

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here