25 C
Dar es Salaam
Wednesday, April 24, 2024

Contact us: [email protected]

‘Nabii’ aliyejitangaza kuwa na dawa ya corona matatani

Mwandishi wetu – Arusha

MKAZI wa Arusha, Mosses Mollel, anayejiita nabii namba saba, aliyetangaza kuwa na tiba ya virusi vya corona, amejikuta matatani baada ya Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dk. Faustine Ndugulile, kusema vyombo husika vinamchunguza juu ya tiba hiyo na kama alikuwa anadanganya umma atachukuliwa hatua za kisheria.

Dkt Ndugulile alitoa kauli hiyo jijini Arusha akiwa katika ziara akisema ana taarifa za mtu huyo ambazo zimesambaa kwenye mitandao ya kijamii na vyombo vya habari akijitangaza kuwa anadawa ya kutibu ugonjwa huo na kumtaka athibitishe kauli yake.

“Kimsingi nimeiona hiyo taarifa ya huyo mtu anayejiita nabii saba kuwa anayo dawa ya kutibu ugonjwa wa corona, ila hapa kwetu Tanzania hatuna maambukizi yoyote ya ugonjwa huyo, tunachotaka huyo mtu  atuthibitishie uwezo wake wa kutibu huo ugonjwa wa corona,” alisema Ndugulile

Alisema iwapo atashindwa kuthibitisha atachukuliwa hatua kali za kisheria.

Alisema hadi sasa Serikali imetuma wataalamu wake kwenda kumsaka na kumhoji kama anavyo vibali vya kutoa huduma ya tiba na kujitangaza kuwa anatoa huduma ya kutibu ugonjwa huo .

Nabii namba saba ambaye ni mkazi wa Ngaramtoni wilayani Arumeru, Mkoa wa Arusha amekuwa akijitangaza kuwa anayo dawa ya kutibu ugonjwa homa hiyo inayosababishwa na virusi vya corona.

Dk. Ndugulile alisema mtu yeyote anayetoa tiba asili na mbadala ni lazima asajiliwe na mamlaka husika ambayo ni Wizara ya Afya, hivyo nabii huyo pia anapaswa kuthibitisha amesajiliwa wapi na lini.

“Tuepuke kutoa kauli ambazo zinakwenda kuchanganya jamii na endapo tutabaini mtu huyu hana sifa ambazo anasema kuwa nazo tutamchukulia hatua za kisheria” alisema Dk. Ndugulile.

Mpaka sasa virusi vya corona vimesababisha vifo vya watu 1,380  nchini China huku wenye maambukizi wakiongezeka kutoka 5,090 hadi 55,748, Tume ya Afya ya China imeeleza.

Tarifa za mwisho kutoka Jimbo la Hubei ambalo ni kitovu cha virusi hivyo zinaonyesha vifo vya mwisho kuripotiwa vilikuwa 116 na maambukizi mapya 4,823 ikilinganishwa na siku moja nyuma ambapo vifo vilikuwa 240 na maambukizi mapya 15,00.

Mkuu wa Programu ya dharura ya afya ya Shirika la Afya Duniani (WHO), Mike Ryan, alisema bado matokeo hayo hayawezi kuchukuliwa kwamba kuna mabadiliko kwenye mlipuko wa virusi hivyo.

Nje ya China kuna vifo viwili vimeripotiwa na watu 447 kuwa na maambukizi ya virusi hivyo kwenuye nchi 24 ambapo juzi Japan ilitangaza kifo kimoja cha corona cha mwanamke mwenye miaka 80 aliyekuwa akiishi kusini magharibi mwa Tokyo.

Kifo cha mwanamke huyo kilibainika kuwa kimetokana na vurusi hivyo baada ya kufanyiwa vipipo baada ya kufariki na inaelezwa hakuwa na uhusiano wowote na Hubei ambapo ni kitovu cha vurusi hivyo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles