31.2 C
Dar es Salaam
Thursday, March 28, 2024

Contact us: [email protected]

Mwongozo wa kutekeleza makubaliano ya Paris wafikiwa

KATOWICE, POLAND

TAKRIABINI mataifa 200 yamefikia makubaliano yatakayopiga jeki mkataba wa Paris uliofikiwa mwaka 2015 kwa lengo la kudhibiti ongezeko la joto duniani ili kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi.

Habri zilizopatikana mjini hapa, wajumbe kutoka mataifa hayo ambao wamekuwa wakijadiliana kwa wiki mbili,  hatimaye jana walifikia mwongozo madhubuti utakaohakikisha malengo ya mkataba wa Paris wa kupunguza joto duniani hadi chini ya nyuzi mbili yanatimizwa.

Rais wa mkutano huo kuhusu mabadiliko ya tabianchi – COP24, Michal Kurtyka alisema kuweka pamoja mpango wa kutekeleza makubaliano ya Paris ni wajibu mkubwa, akiongeza kuwa ilikuwa njia ndefu kufikiwa mwafaka katika mkutano huo.

 Habari hizo zilieleza kuwa miongoni mwa yaliyofikiwa ni pamoja na namna gani nchi zitatoa ripoti kuhusu kiwango cha gesi chafu katika mataifa yao na juhudi za kuipunguza, hakikisho la ufadhili wa kifedha kwa mataifa masikini ili kusaidia kupunguza gesi ya Carbon, kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi yasiyoepukika na kulipa kwa ajili ya uharibifu ambao tayari umetokea.

Hata hivyo inaelezwa kuwa nchi zinazokumbwa na athari kubwa za kimazingira kama mafuriko, ukame na athari nyingine kali zilizotokana na mabadiliko ya hali ya hewa zimesema makubaliano hayo yaliyofikiwa Katowice yanakosa malengo madhubuti kuhusu namna ya kupunguza gesi chafu, hadi kiwango kinachohitajika.

Balozi wa Misri, Wael Aboulmagd aliyewakilisha kundi la nchi zinazoendelea – G77 ikiwemo China, alisema mwongozo huo wa kuyatekeleza malengo ya mkataba wa Paris haujashughulikia mahitaji ya dharura ya nchi zinazoendelea ambazo zimewekwa katika kile alichokitaja tabaka la pili.

Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Kutunza  Mazingira – Greenpeace, Jennifer Morgan alisema wanazidi kushuhudia migawanyiko isiyohitajika kati ya mataifa yaliyo katika hatari – ya visiwani na nchi masikini zikiwa upande mmoja na nchi tajiri ambazo zinaweza kuzuia hatua kuchukuliwa kuhusu tabianchi au kufeli kuwajibika kwa kutochukua hatua za haraka kuyaokoa mazingira.

Katika mkutano huo, nchi zinazoendelea zilitaka ufafanuzi zaidi kutoka kwa nchi tajiri kuhusu mustakabali wa siku za usoni wa kudhibiti athari za mabadiliko ya tabia nchi kwa kueleza bayana ufadhili utatoka wapi na ni hatua gani hasa zitachukuliwa kuchukua hatua za kuepusha maafa zaidi.

Rais wa Ufaransa, Emmanuel Macron alisema nchi yake na Ulaya kwa ujumla zinahitaji kuonesha njia huku akisifu hatua zilizopigwa katika mazungumzo hayo ya Umoja wa Mataifa kuhusu mabadiliko ya tabianchi.

 Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa (UN), Antonio Guterres alisema mapambano hayo ya kudhibiti athari za mabadiliko ya tabia nchi ni mwanzo tu.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles