29.2 C
Dar es Salaam
Thursday, April 18, 2024

Contact us: [email protected]

Mwisho mgumu wa Sumaye Chadema

Andrew Msechu na Asha Bani -Dar es salaam

WAZIRI Mkuu mstaafu Frederick Sumaye ametangaza kujivua uanachama wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kwa kile alichodai ni kutokana na kufedheheshwa na baadhi ya viongozi wa juu wa chama hicho, baada ya uamuzi wake wa kuchukua fomu kuwania uenyekiti wa chama hicho.

Akizungumza katika mkutano na wanahabari Dar es Salaam jana, Sumaye alisema amefedheheshwa na hatua ya baadhi ya viongozi wa chama hicho kufanya jitihada na hata kutumia rushwa, ili kumnyima nafasi ya uenyekiti wa Kanda ya Pwani, ambayo alikuwa mgombea pekee.

“Nimeamua kujitoa. Nimefedheheka sana, sana, hasa nikijua sababu ati nimekosa adabu kwa kuchukua fomu ya kugombea nafasi ya uenyekiti taifa. Ningeweza kukaza shingo kama pale mwanzo na labda yangepita tu. Lakini malengo yetu tutayafikia na kufanikiwa kwa demokrasia ipi ndani ya chama? Kwa umoja upi ndani ya chama?

“Baada ya kutafakari sana kwa kina, na kama hao wakubwa wameweza kuwashawishi wapigakura wa kanda yangu ya Pwani ambapo mimi nilikuwa mwenyekiti wao, wakapiga kura za hapana, ustaarabu unasema Sumaye toka sasa maana hutakiwi. Akuchukiaye hakwambii toka, bali utaona matendo yake kwako.

“Najua wako watakaosikitika sana, lakini pia wako watakaofurahi kwa sababu ninaondoa msongamano na ushindani, hasa katika nafasi ya uenyekiti wa taifa.

“Kwa hiyo nimelazimika kwa kulazimishwa kujiondoa Chadema kutoka leo (jana) hii. Najiondoa kwa kutumia ibara ya 5.4.1 ya katiba ya chama. Kwa tafsiri hii mimi siyo mwanachama wa Chadema kuanzia sasa na sijiungi na chama chochote.

“Kwa bahati nzuri alipokuwa Arusha kwenye mkutano wa kanda, Mwenyekiti Mbowe (Freeman) alishatutahadharisha kuwa sumu haionjwi kwa ulimi, kwa hiyo na mimi siko tayari kuonja sumu kwa ulimi,” alisema Sumaye.

Alisema kwa hatua hiyo ya kujitoa ndani ya Chadema, akiwa tayari alishachukua fomu ya kugombea uenyekiti na kuirejesha, hatima ya fomu hiyo inabaki kwa uongozi wa chama.

Sumaye alisema alichukua fomu hiyo na kuijaza kisha kuilipia Sh milioni moja na kuirudisha kwa wakati, lakini uchunguzi wake kutoka vyanzo mbalimbali unaonyesha si mwafaka wala busara kuendelea na safari hiyo.

“Inabidi leo (jana) nitangaze kuwa hiyo safari ya kugombea uenyekiti ngazi ya taifa naisitisha rasmi kwa usalama wangu, usalama wa wanachama na wa chama chenyewe,” alisema Sumaye.

SABABU ZA KUJITOA

Akielezea sababu zilizomfanya ajitoe, alisema pamoja na kuonyeshwa kuwa hatakiwi kupitia mtiririko wa matukio aliyokutana nayo tangu alipoamua kuchukua fomu ya kuwania uenyekiti wa chama hicho, Sumaye alisema moja ya sababu ni kubaini uwapo wa matumizi ya rushwa iliyowapofua macho wapigakura wa Kanda ya Pwani.

Alisema sababu nyingine ni hatua ya yeye kuchukua fomu ya uenyekiti wa Chadema, ambayo iliibua nongwa, pamoja na kwamba ni haki yake ya kikatiba kulingana na katiba ya chama hicho.

“Lakini pia nilikuwa na lengo la kwanza, kuondoa hisia ambayo imejengeka sana katika jamii kuwa ndani ya Chadema hakuna demokrasia ya kweli, na pili, kuwa nafasi ya mwenyekiti wa taifa ni ya Mheshimiwa Mbowe tu na haisogelewi na mtu yeyote.

“Mimi binafsi nilikuwa siamini kuwa hisia hizi ni za kweli, ndiyo maana niliona haya yasipofutika yanatuchafulia chama chetu.

“Kumbe mimi ndiyo nilikuwa nimekosea sana kufikiri hivyo. Pamoja na nia hiyo njema, badala ya busara kutumika hata kama tungetaka kumlinda Mbowe wetu, njia za ovyo ndizo zilizotumika,” alisema Sumaye.

Alisema kabla ya kuchukua uamuzi wa kujitoa, aliwaambia Chadema inahisiwa kwa kutokuwa na demokrasia ndani mwake na kuwa kiti cha Mwenyekiti Mbowe hakiguswi.

Alieleza kuwa lengo lake katika hayo ni kwamba alitaka kuhakikisha Chadema inayafuta yote inayosingiziwa na iwapo watapiga kura kama walivyopanga, basi watauthibitishia umma kuwa ni kweli ndani ya Chadema hakuna demokrasia ya kweli na kwamba nafasi anayoishikilia Mwenyekiti Mbowe haigusiki.

“Kwa bahati mbaya sana ndivyo ilivyotokea. Na hivyo hivyo waliowahi kujaribu kuwania hiyo nafasi huko nyuma yamewakuta kama haya na labda mengine mabaya zaidi,” alisema Sumaye.

Akizungumzia uchaguzi wa ngazi ya Kanda ya Pwani, Sumaye alisema alipata habari kuwa kuna watu wanakuja kumuona na kumuomba agombee uenyekiti wa kanda na watamchukulia fomu ya kugombea, hivyo alikubali, japo aliwaambia hakuwa na nia sana ya kugombea nafasi hiyo.

“Nikaletewa fomu nikaijaza na kuirudisha kama taratibu zinavyotaka nikawa nashangiliwa kwa furaha kuwa ndiye mwenyekiti, tena nikiwa pekee asiyekuwa na mpinzani.

“Baadhi ya wajumbe wa Kamati Kuu ambao ndio waliofanya mpango wa mimi kuletewa fomu za kanda, ndio wakageuka kuhakikisha mimi ambaye nilikuwa mgombea pekee wa kiti cha kanda nanyimwa kura na kura za hapana zinashinda.

“Wajumbe karibu wote walipigiwa simu na wengi wao walifichwa mahotelini na kupewa fedha kwa kazi hiyo. Sababu kubwa ati kwanini nimechukua fomu ya kugombea kiti cha taifa.

“Basi wangenitahadharisha tu kuwa katika chama chetu nafasi hiyo ina utaratibu wa tofauti nje ya katiba, ningeelewa na labda ningetii na kama nisingetii basi mnanisubiri kwenye vikao vinavyohusu nafasi hiyo.

“Jambo hili limeamsha tena hasira zilizokuwa zimetulia dhidi yangu kutoka marafiki zangu na familia yangu, kutokana na kitendo hiki kilichotokea kwa kutengenezwa na kuongozwa na baadhi ya viongozi wa juu wa chama cha Chadema,” alisema Sumaye.

Alisema alibaini mapema kufanyiwa ‘figisu’ katika uchaguziwa wa kanda na aliwafahamu wahusika wakuu, na alitahadharisha kabla uchaguzi haujaanza kuwa anakijua walichopanga wajumbe kwa kushawishiwa na wachache, suala ambalo si sahihi.

“Huo uchaguzi gani ambao baadhi ya wajumbe wa Kamati Kuu wanawaficha wajumbe na kuwalisha rushwa? Unataka kumwaminisha nani kuwa mimi Sumaye niliyekuwa mwenyekiti wa kanda, waziri mkuu mstaafu niliyekuja kuombwa kugombea na fomu nikachukuliwa na kulipiwa, ati leo watu hao hao wanapiga kura kihalali na kura za hapana zinashinda.

“Walidhani wananikomoa mimi Sumaye, lakini wamekijengea chama mazingira ya ovyo na ya aibu.

“Mbowe najua utakuwa mwenyekiti wetu wa chama. Hilo kundi lako linalojidai ndiyo ’cabinet’ yako ya ndani usipoliangalia litakuvunjia chama,” alisema Sumaye.

Alisema kwa ujumla uchaguzi wa mwaka huu umeacha majeraha mengi ambayo si ya kushindwa kwenye uchaguzi, bali ya mgawanyiko ndani ya chama kwa sababu watu walikuwa wanachaguana kwa kutegemea kundi la nani.

Sumaye alisema kwa wale waliokuwa wanaitwa ‘Team Mbowe’, kulikuwa na nguvu kubwa kutoka nje ya kanda zilizotumika na ambao siyo ‘Team Mbowe’ waliumizwa sana, hivyo Mbowe ana jukumu la kuunganisha makundi maana kwa jinsi anavyowajua baadhi yao, watawasumbua sana wale wengine.

“Ni vema ukweli ukasemwa ili marekebisho yafanyike. Bado tunahitaji kuona upinzani imara. Bado natamani kuona chama cha upinzani kinachopishana uongozi na CCM kama ilivyo kwenye nchi za wenzetu walioendelea. Lakini kwa hali hii safari bado ndefu, lakini tukijitathmini kihalisia na kufanya marekebisho ya kasoro hizi na zingine, safari inaweza kuwa fupi.

“Naamini Chadema ikiweza kusikiliza ushauri mzuri na kubadili utaratibu fulani fulani wa namna ya kuendesha mambo ya chama, bado ni chama tunachoweza kukitegemea kutufikisha katika malengo makuu ya taifa letu,” alisema Sumaye.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles