30.2 C
Dar es Salaam
Friday, March 29, 2024

Contact us: [email protected]

MWINYI ATUA KWA LISSU

Na MWANDISHI WETU-DAR ES SALAAM


RAIS Mstaafu, Ali Hassan Mwinyi amemtembelea na kumjulia hali Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu (Chadema), aliyelazwa katika Hospitali ya Nairobi nchini Kenya kwa matibabu.

Mwinyi anakuwa Rais mstaafu wa kwanza kwenda kumwona Rais huyo wa Chama cha Mawakili Tanganyika (TLS), huku akitanguliwa na Makamu wa Rais Samia Suluhu Hassan aliyemtembelea hospitalini hapo Novemba 28, mwaka huu.

Kiongozi huyo mstaafu alikwenda hospitalini hapo jana saa 11:40 jioni akiwa ameambatana na mkewe, Sitti Mwinyi pamoja na Balozi wa Tanzania nchini Kenya, Dk. Pindi Chana.

Alipofika hospitalini hapo, Mwinyi alimpa pole Lissu huku akimwambia: “Nimekuja kukuona mwanangu je, unaendeleaje na hali yako.”

Baada ya kuulizwa hivyo, Lissu alimjibu mzee Mwinyi kwamba anafurahi sasa anaendelea vizuri.

“Ninafurahi baba yangu ninaendelea vizuri,” alisema Lissu wakati akizungumza na Mwinyi.

Baada ya jibu hilo, Mwinyi alisema: “Nashukuru unaendelea vyema.”

Rais huyo mstaafu alikuwa nchini Kenya katika mahafali ya Chuo Kikuu kimojawapo nchini humo ambapo alikuwa mgeni rasmi.

Lissu ambaye pia ni Mwanasheria Mkuu wa Chadema, alishambuliwa na watu wasiojulikana Septemba 7, mwaka huu, nje ya nyumba yake iliyoko Area D mjini Dodoma.

Alishambuliwa alipokuwa akirejea nyumbani baada ya kutoka kuhudhuria kikao cha Bunge.

Lissu alitibiwa kwanza katika Hospitali ya Mkoa wa Dodoma kabla ya kusafirishwa hadi Nairobi kwa matibabu zaidi.

 

SAMIA

Novemba 28, mwaka huu Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan alimtembelea na kumjulia hali Lissu katika Hospitali ya Nairobi alikolazwa kwa matibabu.

Msafara wa Makamu wa Rais Samia, ulifika katika Hospitali ya Nairobi majira ya saa 11:43 jioni.

Katika msafara huo walikuwemo pia Balozi wa Tanzania nchini Kenya, Dk. Pindi Chana na maofisa wengine wa ubalozi wa Tanzania nchini humo.

Akiwa hospitalini hapo, Makamu wa Rais  alimwombea Lissu apone haraka na kurejea katika hali yake ya kawaida.

“Get well quickly…recover na salamu zako nitazifikisha,” alisema Suluhu.

Awali kabla Makamu Rais hajamtakia afya njema Lissu, yeye mwenyewe (Lissu) alimpa salamu za Rais Dk. John Magufuli.

“Msalimie Rais (Dk. John Magufuli), mwambie nashukuru. Mungu akubariki na mrudi salama nyumbani,” alisema Lissu katika salamu alizomtumia Rais Magufuli.

Lissu amelazwa katika Hospitali ya Nairobi akitibiwa majeraha ya kushambuliwa kwa risasi zaidi ya 30, aliyoyapa Septemba 7, mwaka huu nje ya nyumba yake iliyoko Area D, mjini Dodoma.

Alishambuliwa alipokuwa akirejea nyumbani baada ya kutoka kuhudhuria kikao cha Bunge na kutibiwa kwanza katika Hospitali ya Mkoa wa Dodoma kabla ya kusafirishwa hadi Nairobi kwa matibabu zaidi.

Suluhu alifika hospitalini hapo kumjulia hali Lissu baada ya kuhudhuria sherehe ya kuapishwa kwa Rais wa Kenya, Uhuru Kenyetta.

Kiongozi huyo amekuwa kiongozi wa kwanza wa ngazi ya kitaifa kumtembelea Lissu hospitali kwa ajili ya kumjulia hali na kumtakia afya njema tangu alipolazwa usiku wa Septemba 7, mwaka huu.

Wakati Lissu akikutwa na mkasa huo mbaya, historia yake ya kisiasa inaonyesha kuwa amekwishashtakiwa mara sita, mwaka huu kwa makosa mbalimbali yakiwemo ya uchochezi.

Wachambuzi na wafuatiliaji wa mambo wamekuwa wakieleza kuwa shambulio hilo linaweza kuwa moja ya mikakati ya magenge ya wapinzani wa Serikali waliobanwa na dola ambao sasa wanajaribu kutumia kila aina ya mbinu kuifarakanisha jamii hususan wanasiasa.

Tayari Jeshi la Polisi limekwishaanzisha uchunguzi wa tukio hilo na mkuu wa jeshi hilo, IGP Simon Sirro, ametoa wito kwa mtu yeyote mwenye taarifa zinazoweza kusaidia uchunguzi huo kuzitoa kwa makachero wa polisi.

Sambamba na hilo, Msemaji Mkuu wa Serikali, Dk. Hassan Abbas naye alikutana na waandishi wa habari kuzungumzia tukio hilo na kutoa rai kuwa shambulio hilo lisichukuliwe kisiasa kwa sababu ni uhalifu wenye sura ile ile ya matukio ya kihalifu ambayo yamekuwa yakitokea nchini.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles