24.5 C
Dar es Salaam
Saturday, April 20, 2024

Contact us: [email protected]

Mwinyi aeleza utalii unavyopaisha uchumi Z’bar

Mwandishi wetu -Pemba

RAIS mstaafu Ali Hassan Mwinyi, amesema kuwa sekta ya utalii ni muhimu kwa uchumi wa Zanzibar, kwani inachangia asilimia 27 ya pato la taifa, hivyo juhudi za makusudi zinahitajika kuhakikisha utalii unakua na kuimarika.

Alisema kuwa ni vyema kutumia fursa zilizopo kuutangaza na kuimarisha utalii Zanzibar sambamba na kupewa kipaumbele ili kukuza uchumi wa nchi na kuwanufaisha Wazanzibar wote.

Mwinyi alisema hayo mwishoni mwa wiki kisiwani Pemba, alipokuwa akifunga Tamasha la Utalii.

Alisema kuwa asilimia 80 ya fedha zinatokana na fedha za kigeni za utalii.

“Sehemu 27 ya maisha yetu hapa Zanzibar zinatokana na harakati za kiutalii, hivyo tujue kuwa utalii ni jambo kubwa, ni vyema kujua kuwa kila mmoja unamsaidia kwa nafasi yake,” alisema.

Rais mstaafu alisema idadi ya wageni wanaoingia Zanzibar inaongezeka kila mwaka, ingawa kisiwani Pemba idadi bado ni ndogo.

Alisema kuwa idadi ya watalii walioingia kisiwani Pemba mwaka 2014 ni 26,465 ambapo mwaka jana waliingia watalii 29,403, hivyo juhudi zinahitajika zaidi kuongeza idadi ya watalii kisiwani humo.

“Kumbe kisiwa hiki kina mambo mengi ya kiutalii ambayo hapo awali tulikuwa hatuyajui, tuyatangaze maeneo yetu ya kiutalii ili wageni waingie kwa wingi,” alisema.

Aidha, aliwataka vijana kufanya mazoezi ili kuijenga miili yao sambamba na kufaidika na zawadi zinazotolewa wakati zinapotokea shughuli kama hizo.

Kwa upande wake, Waziri wa Habari, Utalii na Mambo ya Kale, Mahmoud Thabit Kombo, alieleza kuwa mafanikio yanayopatikana katika sekta ya utalii yanatokana na Serikali kuimarisha vianzio mbalimbali vya utalii.

“Sera ya utalii kwa wote imewanufaisha wananchi wote, kwani wanafanya biashara, huuza bidhaa zao kwenye sehemu za kiutalii, wavuvi, wafugaji na wakulima nao hufaidika,” alisema.

Mkurugenzi wa Kamisheni ya Utalii Zanzibar, Abdalla Mohamed Juma, alisema lengo la kufanyika tamasha hilo ni kuifungua Zanzibar kiutalii, hasa Kisiwa cha Pemba ambacho bado kipo nyuma kiutalii.

Kwa upande wao, washiriki wa mbio za nyika waliiomba Kamisheni ya Utalii kuimarisha zaidi maeneo wanayotakiwa kukimbia, ili kuepusha matatizo yanayoweza kuepukika.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles