31.2 C
Dar es Salaam
Friday, March 29, 2024

Contact us: [email protected]

MWIJAGE AWAONYA WAWEKEZAJI NCHINI

 


Na GUSTAPHU HAULE-PWANI
WAZIRI wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Charles Mwijage, amesema tabia ya wawekezaji kuchukua maeneo makubwa bila kuyaendeleza inakwamisha mipango ya Serikali katika uimarishaji wa sekta ya viwanda nchini.

Kutokana na hali hiyo, Mwijage amesema kuanzia sasa, mwekezaji atakayepewa ardhi na kushindwa kuiendeleza ndani ya miezi mitatu, Serikali itamnyang’anya na kumpa mwekezaji mwingine mwenye nia na malengo ya kuiendeleza Tanzania kwa kujenga viwanda kama kauli ya Rais Magufuli inavyosema.

Mwijage alitoa kauli hiyo juzi wakati akizungumza na waandishi wa habari mjini Kibaha, Mkoa wa Pwani, baada ya kutembelea na kukagua mipaka ya eneo la ekari 200 lililopo Tamco, linalolengwa kujengwa viwanda vikubwa zaidi ya vitano.

“Kuna wawekezaji wenye tabia ya kuchukua ardhi na kukaa nayo kwa muda mrefu bila kufanya suala lolote la uendelezaji, jambo ambalo limekuwa likiathiri kwa kiasi fulani mipango ya Serikali ya ujenzi wa viwanda.

“Hata hivyo, kwa sasa atakayefanya hivyo atapokonywa ardhi hiyo na kupewa mtu mwingine mwenye nia ya kuiendeleza.

“Serikali imejipanga kikamilifu juu ya suala la ujenzi wa viwanda nchini, kwa kuwa imedhamiria kukuza uchumi wa nchi na hata uchumi wa Watanzania ambao watafaidika kupitia ajira zinazotokana na viwanda hivyo,” alisema Mwijage.

Kuhusu eneo la Tamco lenye ekari 200, Mwijage alisema eneo hilo lipo chini ya Serikali kupitia Shirika la Maendeleo ya Taifa (NDC).

“Kwa hiyo, eneo hilo litajengwa viwanda vikubwa kikiwamo kiwanda cha nguo, kiwanda cha dawa za wanyama na binadamu na kiwanda cha kuunganishia mitambo na magari.

“Eneo hilo limekaa muda mrefu kwa kuwa halijakaa sawa, kwani lina mito na mabonde ndiyo maana wawekezaji wengi wamekuwa wakilikwepa, lakini tayari Kampuni ya Ulinzi ya Suma JKT imechukua mkataba kwa ajili ya kulisawazisha ili wawekezaji waweze kulitumia.

“Nimekuja hapa kuhakiki eneo hili la Tamco kwa kuwa tunataka hawa wenzetu wa Suma JKT tuwape mkataba wa kulisawazisha eneo hili lenye ukubwa wa ekari 200, ili wawekezaji wa viwanda waweze kulitumia kwa kujenga viwanda vikubwa na vya kati,” alisema.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji Mkuu wa Suma JKT, Brigedia Charo Yateri, alisema anachosubiri ni mkataba na kwamba baada ya kusaini mkataba huo kazi itaanza mara moja.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles