27.9 C
Dar es Salaam
Thursday, March 28, 2024

Contact us: [email protected]

MWIGULU NCHEMBA AJIBIWA KAULI YAKE YA MAANDAMANO

Na PATRICIA KIMELEMETA-DAR ES SALAAM


BAADHI ya wanasiasa na wasomi wamemtaka Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Dk. Mwigulu Nchemba, kuthibitisha kauli yake kuwa maandamano yanayoratibiwa kwenye mitandao yamelenga kuchafua taswira ya nchi na Serikali.

Katibu Mkuu wa Chadema, Dk. Vincent Mashinji amemtaka waziri huyo kujiuzulu kwa kushindwa kumshauri Rais Dk. John Magufuli.

Juzi, akizungumza mbele ya Rais Magufuli wakati wa uzinduzi wa kiwanda cha kutengeneza mafuta ya alizeti mkoani Singida, Mwigulu alisema wanaohamasisha maandamano wanataka watu wakusanyike na baadaye wafyatue risasi ili ionekane Serikali imeua.

Jana, Dk. Mashinji aliliambia MTANZANIA kuwa ameshangazwa kwa kitendo cha waziri huyo kutumia nguvu kubwa kuzuia maandamano wakati Katiba ya nchi inaruhusu.

“Kama ameshindwa kutimiza majukumu yake anapaswa kujiuzulu maana inaonekana ameshindwa kumshauri Rais.

“Anataka kuibadilisha agenda ya maandamano na kuipeleka kwenye agenda ya uhalifu wakati si kweli, ili kulinda heshima anapaswa kukaa pembeni na kupisha vijana wengine ambao ni wasomi wakipewa madaraka wanaweza kuyatumia ipasavyo.

“Suala la maandamano limekuja baada ya wananchi kuchoshwa na vitendo vya utekwaji, kupigwa risasi na baadhi ya watu wasiojulikana huku Jeshi la Polisi likishindwa kutoa majibu yanayoeleweka kuhusu masuala hayo.

“Idadi kubwa ya wanaotekwa au kupigwa risasi ni watu wasio na hatia, lakini wanapojitokeza hadharani na kusema ukweli wanaonekana wabaya.

“Sasa wananchi wamechoshwa na vitendo hivyo ndiyo maana wanataka kufanya maandamano ili kufikisha ujumbe wao kwa Serikali,”alisema Dk. Mashinji.

Kutokana na hilo, alisema kama Mwigulu ana mambo yake binafsi katika suala hilo ni bora angekaa kimya, kuliko kuwadanganya wananchi kuwa wanaotaka kufanya maandamano ni wahalifu.

Kwa upande wake, Naibu Mkurugenzi wa Habari, Unezi na Uhusiano wa Umma wa Chama cha Wananchi (CUF), Mbarara Maharagande alisema kuwa chama hicho kinaunga mkono kufanyika kwa maandamano kwani ni moja ya njia mojawapo ya kufikisha ujumbe kwa Serikali.

Mkurugenzi huyo ambaye yupo upande unaomuunga mkono Katibu Mkuu wa chama hicho, Maalim Seif Sharif Hamad, alisema Serikali inatumia nguvu kubwa ya kuzima maandamano hayo bila kukaa na wananchi ili kusikiliza kero zilizopo, jambo ambalo limewafanya waingize suala la uhalifu wakati halipo.

“CUF inaunga mkono maandamano, lakini tumeshangazwa kuona Serikali inatumia nguvu kubwa ya kuzima maandamano bila ya kusikiliza kilio cha wananchi na sasa wameingiza  maandamano kuwa sehemu ya uhalifu wakati si kweli na Katiba ya nchi inaturuhusu kufanya maandamano,” alisema Maharagande.

Alisema wanachokifanya wananchi ni kufikisha kero zao kwa watawala, hivyo ni vema wakaachwa.

Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam(UDSM), Dk. George Kahangwa alisema kauli ya Dk. Mwigulu ya kufananisha maandamano na uhalifu ni nzito hivyo anapaswa kuthibitisha.

“Maandamano yapo kwa mujibu wa sheria, kama kuna watu watabainika kutumia nafasi hiyo kwa ajili ya kufanya uhalifu wanapaswa kukamatwa na kuchukuliwa hatua, lakini si kuzuia maandamano,” alisema Dk. Kahangwa.

Alisema imefika wakati wabunge wanapaswa kuhoji sababu za Jeshi la Polisi kuzuia maandamano wakati ni haki yao ya kikatiba.

Kwa upande wake, Mchambuzi wa masuala ya kisiasa nchini, Dk. Azavel Lwaitama, alisema: “Wananchi wana haki ya kuandamana pale wanapoona kuna mambo hayajakaa sawa, ili kufikisha ujumbe wao kwa watawala, sasa unapoingiza agenda ya maandamano kwenye suala la uhalifu sijui tukuiteje,”alisema Dk. Lwaitama

Alisema ifike wakati Serikali isikilize kilio cha wananchi na kuyafanyia kazi yale yanayolalamikiwa.

- Advertisement -

Related Articles

1 COMMENT

  1. Mimi nafikiri mkakati wa maandamana hausaidii sana . Ubunifu katika kuisaidia jamii ndiyo njia sahihi. Hakuna anayekatazwa kuchimbia wananchi kisima cha maji au kutoa chakula cha machana kwa wanafunzi au kujenga bweni la wanafunzi. Lowasa aliitikisa CCM kwa mambo aliyokuwa anayafanya na sasa umaarufu unapungua kwa kutokufanya kitu kwa jamii.Jamii ina kero na shida nyingi .Pelekeni nguvu huko vinginevyo mtasahaulika

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles