23.3 C
Dar es Salaam
Saturday, April 20, 2024

Contact us: [email protected]

MWIGULU AZIPA MTIHANI TAASISI, IDARA

Na ELIYA MBONEA -ARUSHA

WAZIRI wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mwigulu Nchemba, ameziagiza idara zilizopo wizarani kwake kufanya kazi za uzalishaji ili kuipunguzia mzigo serikali kuu kwani kuendelea kutumia fedha za walipa kodi kutunza wahalifu magerezani ni hasara kwa taifa .

Kauli hiyo aliitoa jana wakati wa uzinduzi wa nyumba tano za askari wa gereza kuu Arusha lililopo Kisongo mjini hapa zenye thamani ya Sh milioni 253.9 zilizotokana na faida kutoka kwenye mradi wa kilimo unaofanywa na Shirika la Magereza.

Akizungumza kwenye hafla hiyo,  Mwigulu alilishauri Jeshi la Magereza kuangalia  uwezekano wa kuajiri kwa mikataba baadhi ya wafungwa wenye vipaji waliomaliza vifungo vyao na waliorekebishika tabia ili kuongeza nguvu kazi ya uzalishaji.

“Taasisi zilizobakia kuwa na maeneo mazuri ya uzalishaji ni Magereza, bado yana fursa ya maeneo hayo kwenda kwenye mali. Tukizalisha kwenye kilimo tunaweza kukipeleka kwenye matumizi mengine kama walivyofanya Arusha wametoka kwenye kilimo kwenda kwenye nyumba.

“Hii itakuwa chachu kwa Taasisi zilizopo wizarani kwangu, zifanye kazi ya uzalishaji kama huu ni ubunifu mzuri utakaowezesha kupunguza mzigo kwa serikali ikiwamo kuzalisha chakula kwani ni hasara kutumia fedha za walipa kodi kutunza wahalifu magerezani,” alisema.

Alisema ili kufikia malengo ya uzalishaji huo alishauri kwa upande wa magereza kuangalia uwezekano wa watu wenye vipaji wanaomaliza adhabu zao na kuonekana wamejirebisha hivyo watumike kuendeleza vipaji hivyo katika uzalishaji.

Kwa upande wake Kamishna Jenerali wa Magereza nchini, Dk. Juma Malewa, alisema kwamba  tatizo la makazi kwa maofisa na askari wa Magereza kwa nchini nzima bado ni kubwa.

“Nyumba tulizonazo kwa nchi nzima ni 4,221 kuna upungufu wa nyumba 9,800. Niishukuru Serikali kwani mwaka jana ilitoa Shilingi bilioni 10 kwa ajili ya ujenzi wa nyumba za maafisa na askari 320 Gereza la Ukonga Dar es Salaam,” alisema Kamishna Jenerali Dk. Malewa na kuongeza:

“Kwa upande wa ujenzi wa nyumba hizi tano hapa Arusha umefanywa na mafundi wetu kwa maana ya askari na wafungwa kama sehemu ya kuwafundisha kwa kutumia mafundi wa magereza ambapo wameweza kupunguza gharama za ujenzi kwa asilimia 50,” alisema.

Naye Mkuu wa Magereza Mkoa wa Arusha Hamis Nkubas alisema mkoa huo una upungufu mkubwa wa makazi ya askari ambapo nyumba zilizopo ni 142 na hivyo kusababisha askari na maofisa 209 kutokuwa na makazi.

Nkubas alisema nyumba hizo tano zimejengwa Sh. Milioni 50. 7 kila moja na hivyo kufanya jumla ya Sh. Milioni 253.9 ikiwa ni gharama pungufu kulingana na hali halisi kutokana na kutumia nguvu kazi na wataalamu ambao ni askari na wafungwa.

Naye Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema (Chadema),  aliishauri serikali kuweka mkakati wa kupata taarifa nyingi ndani ya magereza ikiwamo kuwalinda watoa taarifa hizo.

“Ndani ya magereza kuna taarifa nyingi kuliko nje kama kukitengenezwa mkakati mzuri mnaweza kupata taarifa nyingi zaidi za kulisaidia Taifa kuliko nje.Kwa uzoefu wangu ndani kuna taarifa nyingi,” alisema Lema.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles