23 C
Dar es Salaam
Saturday, April 20, 2024

Contact us: [email protected]

Mwenyekiti Baraza la Biashara mbaroni kwa tuhuma za upotevu wa Sh bilioni 54

OSCAR ASSENGA-TANGA

Mwenyekiti wa Baraza la Biashara la Jumuiya ya Uchumi ya Nchi za Kusini mwa Afrika (SADC), Salum Shamte na vigogo wengine wa Kampuni ya Katan Ltd, wametiwa mbaroni na Jeshi la Polisi mkoani hapa kwa tuhuma za upotevu wa Sh bilioni 54.

Tukio la kukamatwa vigogo hao lilitokana na agizo la Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Martine Shigella, aliyemwagiza Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tanga, Edward Bukombe na Kamanda wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), Christopher Mariba, kuwakamata.

Shigella alitoa agizo hilo jana baada ya kupokea ripoti ya Mkaguzi wa Ndani wa Serikali katika mkutano wa wadau wa mkonge, ambayo ilionyesha Kampuni ya Katani  ina upotevu wa zaidi ya Sh bilioni 54.

Awali akiwasilisha ripoti hiyo, Mkaguzi wa Ndani Mwandamizi Wizara ya Fedha na Mipango, Idrisa Ally, alisema ukaguzi huo ulianza Januari 22 hadi Februari 22, mwaka huu ambao ulihusu miaka ya fedha kuanzia 2008 hadi 2018.

Ally alieleza kuwa kazi ya ukaguzi huo, walilenga kuangalia miamala ya Mfuko wa Hifadhi ya Jamii wa NSSF, wakulima na fedha za Saccos ya wakulima hao sambamba na mikataba iliyoingiwa baina ya pande zote tatu.

Alisema  katika ukaguzi huo, zaidi ya Sh bilioni 54 hazikufahamika zilipo ama matumizi yake yakiwemo madeni ya wakulima, makato ya wanachama wa NSSF, mkopo na kutolipwa kwa kodi ya Serikali kwa mujibu wa taratibu.

Mkaguzi huyo alieleza yaliyojitokeza katika ukaguzi huo ni pamoja na madeni ya wakulima Sh bilioni 29.8 ambayo hata hivyo alieleza kuwa hayakuonyeshwa kwenye taarifa za kampuni hiyo, Sh  milioni 1.7 za makato waliyokatwa wakulima huku Saccos ya wakulima ikiidai kampuni hiyo Sh milioni 5.55.

Ilionyesha pia  fedha zinazodaiwa na kampuni hiyo kwa wakulima ni  zaidi ya Sh bilioni 2.8.

Baada ya ripoti hiyo kuwasilishwa kwenye mkutano huo, Shigella alitoa nafasi kwa pande zote kujieleza na ndipo Shamte ambaye ni mmiliki wa Kampuni ya Katan, kudai ripoti hiyo haina usahihi na hawakushirikishwa katika kuiandaa.

Alisema wao kama walezi wa wakulima, tangu  mwaka 1999 walikuwa wakiendesha kilimo cha mkataba wa kibiashara baina yao, bodi ya mkonge  na wakulima.

“Hakuna mkulima anayeibiwa, sisi sote lengo letu ni kuinua zao la mkonge kwa kuwanufaisha wakulima, ripoti hii haikuhusisha walengwa, yaani Katan Ltd, hivyo naomba ripoti hii ipitiwe upya kwa kushirikishwa,” alisema Shamte.

Waliokamatwa kwenye mkutano huo sambamba  na Shamte ni Mkurugenzi Mtendaji wa Katan Ltd, Juma Shamte, Fadhil Mhina ambaye ni mhasibu wa Katan Ltd, Fatma Diwani Mkurugenzi na Theodora Mtegeti ambaye ni Ofisa Uhusiano.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles