30.2 C
Dar es Salaam
Saturday, April 20, 2024

Contact us: [email protected]

MWANDISHI SHADRACK SAGATI AFARIKI DUNIA KWA AJALI

NA HARRIETH MANDARI, GEITA


WATU wawili wamefariki dunia kwa ajali wilayani Geita, akiwamo Ofisa Habari wa Wizara ya Viwanda na Biashara, Shadrack Sagati na mwananchi mmoja,   Semeni Kibiriti (36).

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Geita, Mponjoli Mwabulambo, alisema ajali hiyo ilitokea juzi wakati dereva wa gari l namba   STK 9565 aina ya Toyota Land Cruiser V8, alipomkwepa mpita njia, Happiness James (7), aliyekatiza barabarani ghafla  wilayani Chato, Mkoa wa Geita.

Alisema kutokana na ajali hiyo, watumishi wa wizara hiyo akiwemo Naibu Katibu Mkuu, Ludovick Nuhiye, Mchumi Nickson Matembo, Mkaguzi Mkuu wa Ndani, Yusuph Mbwalwa na dereva, Lucas  wamelazwa katika Hospitali ya Mkoa wa Geita wakipatiwa matibabu.

Kamanda Mwabulambo  alisema ajali hiyo ilitokea katika eneo la Minkoto, Kijiji cha Kalembela wilayani Chato mkoani Geita.

“Gari hilo lilikuwa likitokea Mkoa wa Kagera kwenda Mwanza na  binti huyo  e alinusurika kugongwa baada ya dereva kufanya jitihada za kumkwepa.

“Dereva alilazimika kupeleka gari upande wa kulia ambako pia alikutana na mpitanjia,   Semeni Kibiriti  ambaye alifariki dunia hapo  hapo.

“Tulipofika kwenye eneo la ajali tuliwatoa abiria hao  pamoja na yule mwenda kwa miguu aliyefariki dunia.

“Tuliwapeleka katika Hospitali ya Mkoa wa  Geita ambako kwa bahati mbaya  Sagati alifariki dunia wakati juhudi za kumpatia matibabu zikiendelea,” alisema Kamanda Mwabulambo.

Alisema chanzo cha ajali hiyo hakijajulikana  na  jeshi la polisi linaendelea na uchunguzi.

“Kwa kweli hata sisi bado tunachunguza chanzo cha hiyo ajali kwa sababu dereva alifanya kila juhudi kunusuru waenda kwa miguu na abiria wake.

“Lakini bahati mbaya tu imetokea hivyo inawezekana tatizo lilitokea kwenye gari hilo lakini  bado tunaendelea kuchunguza chanzo chake,” alisema.

Alisema hali za majeruhi zinaendela vizuri na kwa sasa wanaendelea vema na matibabu katika Hospitali ya Mkoa wa Geita.

Wakati huohuo, habari zilizopatikana kutoka Wizara ya Viwanda jana zilisema mwili wa Sagati unatarajiwa kupokewa nyumbani kwake Dar es Salaam keshokutwa Alhamisi.

Kwa mujibu wa taarifa hizo, marehemu anatarajiwa kusafirishwa kwenda nyumbani kwao katika Jimbo la Mwibara mkoani Mara kwa mazishi, Ijumaa wiki hii.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles