24.7 C
Dar es Salaam
Tuesday, March 19, 2024

Contact us: [email protected]

Mwanamke ampenda mume wa dada yake, aishi naye

CARO Nduti ni mama ya watoto wawili na kwa muda wa miaka minne ndoa yake ilifana, lakini anasema alifurahia matunda ya ndoa hiyo kwa muda mfupi tu.

Caro ambaye alizaliwa mwaka 1981 anasema alilelewa kijijini na kwamba alikwenda mjini Nairobi, Kenya kwa mara ya kwanza alipoanza maisha ya ndoa na kutafuta ajira.

Alikutana na baba wa watoto wake wakiwa washirika kanisani, kama vijana wadogo wote walikuwa shuleni na walikuwa wameshikilia maadili ya dini.

Lakini wakati huo wawili hao walikuwa washirika wa kanisa na wala hawakufikiria kama mapenzi yao yangeota mizizi.

Baada ya shule alikutana tena na rafiki yake wa kanisani mwaka wa 2002 alipoijiunga na taasisi ya mafunzo.

Anakumbuka akimtembelea katika taasisi ya mafunzo aliyokuwa anaisomea na hapo ndipo wakaanza uhusiano wa kimapenzi, licha ya kwamba alikuwa bado anasoma walianza kuishi pamoja kama mume na mke, japo taasisi yenyewe ilikuwa ya bweni.

“Mpenzi wangu alinisihi nipate ujauzito kabla ya kumaliza chuo kikuu, alikuwa na wasiwasi kwamba baada ya kufuzu mafunzo ningemtoroka,” anasema Caro.

”Nilimpenda na sikuwa na ufahamu wa maisha kwani nilikuwa bado msichana mdogo tu, nikakubali kupata ujauzito,” anaendelea kusimulia.

Baada ya kumaliza mwaka wa mwisho wa chuo alikuwa na ujauzito wa miezi kadhaa na kwamba hata jamaa wa mpenzi wake walikuwa wanamfahamu kama mke wake.

“Mume wangu alishiriki sherehe yangu ya kumaliza masomo huku akiandamana na watu wa familia yake wakiwa wamejaza gari kuja kunichukua, kitendo hicho kilinifanya kujihisi kupendwa na familia yake.”

Desemba mwaka 2003, alijifungua mtoto wao wa kwanza ambaye ni mvulana huku familia yao ikiwa ni ya furaha na utangamano.

Mwaka 2006 akajifungua mtoto wa pili ambaye alikua ni mvulana pia, lakini katika muda huo alianza kugundua kuwa tabia za mumewe zilikuwa zinampa wasiwasi na hofu; alikuwa anaona dalili za mwanamume aliyekuwa na wanawake wengine nje ya ndoa.

Anasema kwa kuwa alikuwa na umri mdogo wa miaka 22, aliogopa kumuuliza maswali ya udanganyifu katika ndoa kwahiyo aliishi kana kwamba hakukuwa na jambo linalomkera.

“Nilikuwa najiuliza hakuna chochote ninachokosa kwenye ndoa, kwahiyo acha afanye mambo yake nje mradi mimi nimeridhika, mwanamke ni kuvumilia,” alijifariji.

Cha kushangaza ni kwamba alikuwa anawajua baadhi ya wanawake wanaotembea na mumewe, mara nyingi mume hakuficha michepuko yake – haikuwa siri.

“Wakati mwingine nilikuwa nawafahamu, tulikuwa tunakula na kunywa na wao katika majumba ya starehe, ni kana kwamba mume wangu alihisi kuwa nilikuwa muoga wa kuuliza maswali, “anasema.

Wakati fulani binamu yake ambaye anamtambulisha kama dada yake, kwa sababu walilelewa katika mazingira sawa – Caro alilelewa na mama wa binamu yake, kwani mama yake alifariki dunia akiwa na umri wa miaka saba.

Kwahiyo, mlezi wake alikuwa ni shangazi yake alimfananisha kama mama na kwamba watoto wa shangazi yake walikuwa ni dada zake.

Binamu yake alipomaliza shule ilibidi pia aanze kutafuta maisha mjini; kile anachofahamu ni kwamba yale matembezi ya binamu yake kwake ndio chimbuko la uhusiano wa kimapenzi kati yake na mume wake.

Anakumbuka kuwa mume wake alikuwa harudi nyumbani tena, ilifika mahali ambapo mume alikuwa hafichi tena uhusiano wake na shemeji yake.

“Nakumbuka mume wangu alikuwa ananipigia simu na kuniambia kuwa hatarudi nyumbani atakuwa na binamu yangu, sikuwa na la kufanya zaidi ya kuvumilia,” anasema.

Anasema baadae dada yake (binamu) alianza kumtukana mara kwa mara kupitia ujumbe wa simu.

Licha ya kwamba alikuwa akimuonyesha mume wake ujumbe huo wa matusi, hakuwahi kumtilia maanani.

Uhusiano kati ya mume wa Caro na dada yake uliendelea hadi pale ulipogunduliwa na jamaa zao, licha ya kuwa mama wa binamu yake kupinga uhusiano huo, dada yake hakujali.

Mwaka wa 2008 Caro aliamua kumwachia binamu yake mume.

Caro aliposhindwa na maisha hayo aliondoka na kuanza kuishi pekee yake. Lakini baada ya muda mumewe alimtafuta na wakarejea tena nyumbani.

Licha ya kuwa binamu yake alikuwa anaishi na mumewe kama wanandoa, aliamua kurudi nyumbani kwa maslahi ya watoto wake ambao alihisi walihitaji malezi ya baba.

Sasa ikawa ni mtindo, Caro na mumewe kuachana, baada ya muda wanarudiana, kwani licha ya uhusiano wake na dada yake kuwapo, binamu yake alijifungua watoto wawili wa kike.

Caro alikuwa amekubali kulea watoto wa binamu yake akitamani uhusiano kati ya binamu yake na mumewe uishe kabisa.

Cha ajabu alipokuwa anapigania uhusiano wa hao wawili uishe upande mwingine aligundua kuwa mumewe alikuwa anafanya uhusiano na kila msichana wa kazi aliyekuwa anamwajiri.

Maisha yakawa magumu, na hapo ndipo Caro akashindwa kuvumilia maisha ya mumewe ya michepuko ya kila siku sio kwa binamu yake, ila hata kwa wasichana wa kazi aliokuwa anawaajiri.

Caro aliondoka siku moja kwenye ndoa yake na hakurudi tena kwa mumewe.

Anasema aliyekuwa mumewe bado wanaishi na dada yake kama mume na mke na kwamba alishawasamehe kabisa.

Anasema tabia ya mumewe ilimfanya kuwa na uchungu mwingi na hata kufikia hatua ya kujichukia.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
584,000SubscribersSubscribe

Latest Articles