23.3 C
Dar es Salaam
Wednesday, April 24, 2024

Contact us: [email protected]

Mwanamke ajioa Uganda

KAMPALA, UGANDA

MWANAMKE mmoja nchini hapa ameshangaza wengi baada ya kujioa mwenyewe.

Lulu Jemimah mwenye umri wa miaka 32 alijioa Agosti mwaka huu jijini hapa na kudai kuwa kwa miaka kadhaa watu wamekuwa wakimuuliza lini angefunga ndoa.

“Nikiwa na miaka 16 baba yangu aliandika hotuba yake kwa ajili ya kuisoma siku ya harusi yangu. Kila nilipokuwa nasherehekea siku yangu ya kuzaliwa mama yangu alikuwa akiniombea, na kwa miaka ya karibuni maombi yake yalikuwa pamoja na kupata mume bora, ambaye atanifaa,” alisema Jemimah.

Kwa mujibu wa Shirika la Utangazji la Uingereza – BBC, mwaka jana Jemimah alichaguliwa kujiunga na masomo ya juu ya uandishi wa ubunifu katika chuo kikuu maarufu cha Oxford nchini Uingereza.

Hata hivyo licha ya mafanikio hayo ya kielimu, alisema bado watu waliendelea kumuuliza anapanga kuolewa lini ili aanzishe familia na kupata watoto.

“Hawaamini kuwa kinachonifanya kuwa macho usiku si hofu ya uwezekano wa kutopata bahati ya kutembea altareni kwenda kufunga ndoa,” alisema mwanamke huyo.

Alisema kutokana na hali hiyo, aliamua kuchukua uamuzi wa kuwatuliza.

“Nilipotimiza miaka 32 nikaamua kujioa. Naamini mimi nitajitunza na kujipa amani,” alisema.

Taarifa zinaeleza harusi yake ilimgharimu Dola za Marekani 2.62, ikiwa ni gharama ya usafiri hadi mahala harusi hiyo ilipofanyikia.

“Rafiki yangu mmoja aliniazima gauni la harusi, mwingine akijitolea kuniremba, dada yangu aliniazima vito na kaka akaoka keki,” alisema mwanamke huyo.

Alisema waalikwa wote walielekezwa wapi pa kwenda na huko walitakiwa wajilipie gharama za vinywaji na chakula.

“Ndoa ni kielelezo cha upendo na msimamo thabiti wa maisha. Lakini kwa watu wengi nyumbani ni njia pekee ya mwanamke kujihakikishia usalama wa kifedha. Hata mimi nahitaji hivyo vitu, lakini tofauti pekee hapa ni kuwa nitajipatia mimi mwenyewe,” alisema.

Jemimah aliandika maelezo hayo ya maisha yake katika ukurasa wa mtandao wa kukusanya pesa kwa watu wenye uhitaji unaofahamika kama Go Fund Me.

Tayari ameshakamilisha mwaka wa kwanza wa masomo kwa msaada wa watu 279 wakiwamo marafiki na watu asiowafahamu.

Alieleza ili kumaliza masomo yake hayo ya uzamili, anahitaji pauni 10,000 kwa ajili ya ada na mahitaji mengine ya ziada na mwezi huu tayari alishapata usaidizi wa pauni 4,000 zilizochangwa na watu 69.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles