Imechapishwa: Wed, Oct 11th, 2017

MWALIMU NYERERE NI MFANO WA UTU ULIOISHI

KATIKA juma hili lililoanzia Oktoba 9, ziko situ tatu ambazo huadhimishwa kimataifa na kitaifa na kwa kuangalia maudhui yake tunaweza kuona jinsi gani siku hizi zimefungamana.

Fungamano hilo ni la kimtazamo na hata kimaudhui. Siku ya Oktoba 10 ni siku ya kimataifa ya kupinga adhabu ya kifo.

Siku hii huadhimishwa kama ishara ya kuonyesha thamani ya utu wa mwanadamu na haki ya mwanadamu ya kuishi. Siku ya Oktoba 11 yaani leo Jumatano nayo ni siku ya mtoto wa kike.

Siku hii huadhimishwa kwa kutambua umuhimu wa mtoto wa kike na thamani aliyonayo katika jamii. Watoto wa kike ulimwenguni wanakaribia au wapo bilioni moja na milioni mia moja na wana changamoto nyingi pamoja na fursa.

Siku hii huwa ni kuziweka bayana changamoto hizo na fursa zilizopo na hasa katika juhudi za kuziba ufa wa ubaguzi dhidi ya watoto wa kike na wenzao wa kiume.

Siku ya tatu ni kumbukumbu ya kifo cha muasisi wa Taifa la Tanzania Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, baba wa Taifa. Hii ni Oktoba 14 siku ya Jumamosi.

Watanzania huitumia siku hii kumkumbuka Mwalimu na hasa masuala muhimu aliyoyasimamia na yale aliyotolea miongozo kwa kauli au kwa vitendo.

Katika maadhimisho haya kila mmoja  huadhimishwa kwa njia mbalimbali na kwa hizi za kimataifa kila nchi huadhimisha kwa njia inayoona kwao inafaa.

Katika kuziangalia siku hizi naona zote zimeangukia mwezi wa kumi na ziko katika wiki moja. Mwalimu Nyerere pamoja na kuwa amefariki miaka 18 iliyopita hakuna dalili ya kusahaulika hapa nchini au hata sehemu mbalimbali nje ya nchi.

Kama nilivyoelezea kwenye makala ya wakati kama huu mwaka jana, ni vigumu sana kwa Watanzania kumuweka Mwalimu kuwa historia, Mwalimu anaonekana kuwa hai kutokana na jinsi alivyoweza kuongoza Taifa hili kwa kumaanisha kile alichokuwa anakisimamia.

Kila siku hutaikosa sauti ya Mwalimu ama kwenye runinga au redio na maandishi kwenye magazeti. Mwalimu alienzi utu na thamani ya utu kwa njia kadhaa. Alithamini elimu ambayo ndiyo humuinua mnyonge kutoka katika unyonge wake na kumbadilisha kuwa kiumbe chenye kujiamini na kuweza kubadili maisha kabisa bila kujali elimu hiyo ameipatia wapi.

Wasichana wengi wa Tanzania wakati nchi inapata uhuru walikuwa hawana fursa za kupata elimu, zaidi ya kuandaliwa kuwa wake na hivyo kuozwa wakiwa wadogo.

Falsafa ya elimu ya ujamaa na kujitegemea haikuwa na ubaguzi hivyo kwa wazazi walioifuatilia na waliohamasika katika kipindi hicho cha Mwalimu walichukua fursa iliyokuwepo na kuwawezesha watoto wao wa kike kupata elimu.

Idadi ya watoto wa kike mashuleni iliongezeka. Fursa nazo ziliongezeka shukrani kwa falsafa hiyo iliyokuwa inapambana na ubaguzi wa kijinsia uliokuwa ukiwaweka watoto wa kike jikoni na si kuwapa fursa ambapo tulikuja kuziona, pale tulipoanza kusikia mwanamke wa kwanza rubani nchini Tanzania.

Haya yalikuwa zao la elimu na fursa zilizojengwa kipindi cha mwalimu. Wasichana wengi zaidi walipitia katika elimu tukawapata madaktari, wahandisi na hata wanasayansi.

Tunapoiadhimisha siku hii kwa mwaka huu tunajua kuwa changamoto bado zipo na pia fursa zipo, hivyo ni bora kuendelea kuzikumbuka falsafa za Mwalimu katika kuongeza fursa za watoto wa kike na kuwakinga dhidi ya madhara yatokanayo na mila potofu.

Hali halisi katika jamii zinazowafanya watoto wa kike wasiweze kufikia fursa zilizopo na kuweza kuyaishi maisha yenye hadhi na kuthaminika.

Tukiangalia hii haki ya kuishi tunaona kuwa adhabu ya kifo iko bado katika vitabu vya sheria nchini mwetu. Adhabu hii ni ya kutweza utu.

Tunaoipinga adhabu hii tunakumbuka pia  kuwa utu wa mtu ni wa thamani na kama uhai ulivyo na thamani ukamilifu wake ni jinsi mtu anavyoishi. Tunamkumbuka sana Mwalimu kutokana na jinsi alivyoishi. Wapo watu wengi ambao wamekufa lakini walisahaulika mara walipozikwa tu.

Lakini kumbukumbu ya Mwalimu inaendana na thamani aliyoiweka katika uhai na ndio maana pamoja na kuwa amekufa maneno yake na yale aliyoyasimamia yako hai bado.

Watetezi wa haki ya kuishi wanasimama na falsafa ya utu alioijenga Mwalimu pale alipoweka kama msingi kuwa binadamu wote ni sawa na wana utu sawa. Ikiwa hivyo ndivyo hakuna sababu ya kuufisha utu kwa kuwabagua watoto wa kike au kwa kuondoa uhai wa mtu kwa sababu yoyote ile.

Wapo watakaosema mbona Mwalimu aliweza kutia saini watu wakanyongwa? Ukifuatilia utaona kuwa haikuwa kwa njia ya ufahari bali kwa kuwa sheria ilikuwepo na ikabidi ifuatwe lakini haikuendelea na hata haiko katika kumbukumbu kuwa ni jambo lililomfurahisha sana tofauti na tulivyomsikia akielezea adhabu ya waliokuwa wanakula rushwa.

Sauti yake katika hili kuwa rushwa ni adui wa haki na aliichukia kwa dhati kiasi kwamba aliielezea adhabu iliyokuwa ikitolewa kwa hisia za kiasi alivyoichukia.

Hii haikuwa sawa na hii adhabu ambayo kwa mara ya kwanza tangu adhabu hiyo iache kutekelezwa nchini, Rais aliyeko madarakani ameielezea hadharani ugumu wake na kuwa hayuko tayari kuitekeleza.

Katika wiki hii tunapojiangaliza siku hizi tatu muhimu inabidi kuvuta fikra na kuangalia yale yote yanayofungamana katika siku hizi, kuiangalia siku ya mtoto wa kike kimataifa, siku ya kupinga adhabu ya kifo wakati tukimkumbuka muasisi wa taifa hili.

Fungamano niliyonalo hapa ni utu na thamani iliyopo hata kwa mhalifu wa kosa kubwa kuliko makosa yoyote yale. Pia  kuthamini utu wa mtoto wa kike ili kumuwezesha kukua kufikia upeo wake na kumuwezesha kuzikabili changamoto zinazofunika thamani ya utu wake na kuzifikia fursa zinazohuisha thamani ya utu.

Fikra na falsafa za Mwalimu Nyerere ni mfano unaoishi wa mtu aliyeuishi utu pamoja na ubinadanu wake, kipaumbele ni thamani ya utu na ndio maana aliamini katika ujamaa alioujengea kauli mbiu kuwa  ni utu, utu, utu.

Mwandishi ni Mkurugenzi  Mtendaji wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC)

Weka maoni yako

XHTML: You can use these html tags: <a href="" title=""> <abbr title=""> <acronym title=""> <b> <blockquote cite=""> <cite> <code> <del datetime=""> <em> <i> <q cite=""> <s> <strike> <strong>

YOUTUBE

MWALIMU NYERERE NI MFANO WA UTU ULIOISHI