27.5 C
Dar es Salaam
Friday, March 29, 2024

Contact us: [email protected]

Mwalimu Nyerere: Miaka 19 baada ya kifo chake

NA MARK MWANDOSYA –MORONI, COMORO



HOTUBA ya Profesa Mark Mwandosya kwa Chuo Kikuu cha Comoro wakati wa Maadhimisho ya Miaka 19 ya kifo cha Mwalimu Nyerere, Moroni, Comoro, Oktoba 26, 2018.

Utangulizi

Wakati tukikulia katika vitongoji vya Kiafrika vya Makao Makuu ya Jimbo la Nyanda za Juu Kusini la Mbeya, katika Tanganyika chini ya Udhamini wa Umoja wa Mataifa, tulikuwa tukitambua kuna kitu mahali hakiko sawa.

Mbeya kipindi hicho ilikuwa mfano wa miji iliyokuwa na maeneo yaliyogawanywa kufuata rangi kutokana na ubaguzi wa rangi kusini mwa Afrika, na hasa Afrika Kusini ya Kibaguzi.

Kwa maeneo ya kifahari, yaliyofahamika kama Uzunguni, yalikuwa maalumu kwa makazi ya Wazungu tu hasa watawala wa Kikoloni wa Uingereza.

Mji wenye wenye shughuli za kibiashara, ulikuwa maalumu kwa watu wenye asili ya Kiasia na ulifahamika kama Uhindini.

Baada ya saa 12 jioni, Wafrika walikuwa hawaruhusiwi kuonekana maeneo ya Uzunguni au Uhindini, isipokuwa tu kwa watumishi wa ndani au walinzi. Katika rika letu la umri wa miaka mitano, hali hiyo haikutusumbua sana.

Kitongoji chetu kilikuwa na nafasi ya kutosha ya kucheza pamoja na shule ya msingi. Mbali ya hayo, tulikuwa katika ukingo wa mji, ambao ulizamia msituni ukichanganyika na vichaka na nyasi. Mazingira yalitupatia vyote tulivyohitaji kupitisha muda: viwanja vya mpira visivyo rasmi; mikondo ya maji baridi lakini yaliyo safi, ambako tulijifunza kupiga mbizi na kuogelea bila kikomo; na ambako wengine wangetumia muda wao kuwinda ndege na panya.

Mfumo wa ubaguzi wa rangi wa Kiingereza, haukuishia katika kutenga maeneo ya vitongoji kulingana na rangi pekee bali pia uliendelea hadi katika suala la aina ya makazi, ambayo yalipaswa kujengwa katika eneo husika.

Hata aina ya vyoo, vilijengwa kulingana na rangi kama vile: maliwato kwa ajili ya Wazungu; maliwato kwa Waasia; na maliwato kwa Waafrika, ambayo yalikuwa choo cha shimo.

Sekta ya usafirishaji haikusalimika na ubaguzi huu. Mabehewa ya treni yalitengwa kufuatana na rangi, ambapo Daraja la Kwanza lilikuwa kwa ajili ya Wazungu, Daraja la Pili kwa ajili ya Asia na Daraja la tatu kwa Waafrika.

Katika elimu, shule nzuri na zilizopewa ruzuku nono zilikuwa kwa ajili ya watoto wa Kizungu, hasa Waingereza, mfano ni Shule ya Mbeya, ambayo sasa inafahamika kama Sekondari ya Iyunga. Zikafuatia shule za Waasia. Shule za Waafrika zilikuwa chini ya kile kilichojulikana Machifu, hazikupewa fungu la kutosha na zilikuwa na mazingira mabaya.

Hata silabu (muhtasari wa masomo) uliakisi msingira ya shule. Kwa ujumla watoto wa Kiafrika walifundishwa ili hapo baadaye waje kufanya kazi za ukarani, ualimu, usaidizi katika sekta ya afya na ufundi sanifu.

Na hilo linaweza kuthibitishwa na uchache wa wataalamu wakati Tanganyika ilipopata uhuru, ambapo kulikuwa na chini ya wahitimu 20 wa Kiafrika wa chuo kikuu.

Tulikuwa tumesikia kuhusu harakati za kupigania uhuru za nchi chache za Afrika. Tangazo la Kwame Nkrumah la uhuru wa Gold Coast (Ghana) lilikuwa kiashirio cha zama mpya za kumkomboa Mwafrika na Afrika.

Karibu na Mbeya, kulikuwa na mvumo wa kilio cha kutaka uhuru wa Tanganyika, kilichoongozwa na Chama cha Tanganyika African National Union (TANU). Kama chama cha umma, kiliundwa Julai 7, 1954, kwa ajili ya harakati za kupigania uhuru wa Tanganyika.

Nyerere na harakati za kupigania uhuru wa Tanganyika

TANU iliundwa kutokana na Chama cha Tanganyika African Association (TAA), taasisi ya kiraia iliyoundwa mwaka 1950 na kile tunachoweza kuita “wanazuoni wa nyumbani”, asasi ya kiraia na ambayo kwa siri ilijikita katika kupigania huduma za watumishi wa umma wa Kiafrika.

Kleist Sykes na Cecil Matola, Myao kutoka Nyasaland (Malawi) walikuwa watu muhimu waliopelekea kuundwa kwa African Association (AA), kisha ikafuata TAA mwaka 1929.

Sykes Mboweni, baba wa Kleist Sykes alikuwa  Mzulu aliyeletwa Tanganyika kutoka Afrika Kusini na utawala wa Kiingeeza kupambana na ukoloni wa Kijerumani.

Abdulwahid, mtoto wa Kleist Sykes na kaka yake, Ally Sykes walishiriki katika Vita ya Pili ya Dunia.

Walirudi baada ya vita kama sehemu ya Jeshi lijulikanalo kama King’s African Rifles (KAR) kutoka Burma wakaja na wazo kuhusu Mahatma Gandhi na harakati za kupigania uhuru wa India.

Nyuma ya kuundwa kwa  TAA kulikuwa na mwungwana na mtaalamu wa kuzungumza Hamza Kibwana Bakari Mwapachu, rafiki wa Mwalimu Nyerere kutokana na nyakati zao wakisoma Chuo cha Makerere  nchini Uganda mwaka 1943 hadi 1945 na  Bwana Soko wa Kariakoo, Abdulwahid Sykes, mtoto wa Kleist Sykes rafiki mwingine wa karibu wa Nyerere.

Abdulwahid Sykes akawa Katibu Mkuu mwasisi wa TAA pamoja na Kaimu Rais. Wajumbe wengine wa TAA ni pamoja na “Vijana wa Makerere”, miongoni mwao : Dk. Warte Barte Kenneth Mwanjisi, Dk. Joseph Mutahangarwa, Dk. Vedasto Kyaruzi na Dk. Lugazia, Andrew Tibandebage, Gosbeth Rutabanzibwa na wengineo.

Marehemu Dk.  Mwanjisi alitokea Rungwe, Mbeya, na alikuwa kaka wa Roland Mwanjisi, Frank Mwanjisi, Elifasi Mwanjisi na Victoria Mwanjisi, wote walisomea Makerere. Dk. Mwanjisi alikuwa baba wa Jane Mwanjisi, Kapteni Tony Lazaro na Mhandishi Cosmas Mwanjisi.

Mcomoro mwenye makazi yake Dar es Salaam, Ali Mwinyi Tambwe aliwahi kumtembelea Hamza Mwapachu, Ofisa Ustawi huko Ukerewe, kupata maoni yake kuhusu nani ambaye angepaswa kuwa Rais wa TAA, mtu ambaye atachochea ari, utamaduni na au farsafa ya kisiasa ndani ya TAA na kuongoza mageuzi ya TAA, kutoka taasisi ya kiraia na ustawi kuwa chama cha siasa.

Alikuwa Hamza Mwapachu, ambaye alimpendekeza Nyerere kuwa angekuwa chaguo bora la kuiongoza TAA.

Itaendelea wiki ijayo

 

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles