26.9 C
Dar es Salaam
Thursday, April 25, 2024

Contact us: [email protected]

MWAKYEMBE, MWIJAGE NAO WAMJIBU CAG

Na Fredy Azzah- Dodoma


WAZIRI wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk. Harrison Mwakyembe na Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Charles Mwijage, wamejibu hoja zilizomo katika ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Profesa Mussa Assad.

Mawaziri hao wanatoa ufafanuzi wa hoja hizo baada ya juzi Waziri wa Fedha na Mipango, Dk. Philip Mpango na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Selemani Jafo, kujibu hoja za CAG zilizoibuliwa katika wizara zao wanazoziongoza.

Akizungumza na waandishi wa habari mjini hapa jana wakati akijibu hoja hizo, Mwakyembe, alisema Serikali imefungua ukurasa mpya na Kampuni ya Star Times Group iliyokubali kutoa Sh bilioni tatu kama ruzuku kwa mwaka 2018 wakati mambo mengine yakiendelea kushughulikiwa.

Alisema pamoja na mambo mengine, lugha ya Kichina iliyotumiwa katika mifumo ya kampuni hiyo ilikuwa chanzo cha baadhi ya matatizo yaliyobainika.

Alisema ripoti ya CAG na ile ya kamati maalumu aliyoiunda ikiongozwa na Msemaji Mkuu wa Serikali, Dk. Hassan Abbasi, zilibaini mkataba ulioingiwa kati ya Shirika la Taifa la Utangazaji (TBC) na Kampuni ya Star Communication ulikuwa mbovu kwa sababu uliipa kampuni hiyo mamlaka makubwa ya usimamizi wa fedha na uendeshaji bila kuishirikisha TBC yenye hisa asilimia 35.

“Udhaifu katika uamuzi wa wawakilishi wetu kwenye Kampuni ya Star Media, ulijitokeza dhairi mwaka 2014 ambapo Mkurugenzi Mkuu wa TBC aliyepita alikuwa pia Mwenyekiti wa Bodi ya Star Media aligoma kusaini hesabu za kampuni hiyo mwaka 2014 kwa hoja kuwa baadhi ya hoja zilikosa uthibitisho na toka hapo akajiuzulu uenyekiti na kuacha Wachina waendeshe kampuni,” alisema.

Katika ripoti yake ya ukaguzi maalumu, CAG alibainisha maeneo matatu ambayo vifaa vya Sh bilioni 34.4 vyenye msamaha wa kodi kutotumika katika mradi husika, Star Media kutoza uchakavu wa Dola milioni 30.11 za Marekani isivyo halali na kampuni hiyo kutochangia gharama ya mtaji wa Dola 650,000 za Marekani.

Dk. Mwakyembe alisema baada ya majadiliano ya muda mrefu na Star Times, hatimaye waliikubali hoja ya CAG na mapendekezo yote na wameipa mamlaka bodi ya wakurugenzi madaraka yake stahili.

“Hivyo kuruhusu uwazi wa kutosha katika uendeshaji kampuni, kuiruhusu TBC na wataalamu wake kuingia kwenye mifumo ya tehama ya uendeshaji wa kampuni hiyo ya ubia na kuleta uwiano.

“Iliamliwa bodi ya Star Media ambayo Mwenyekiti wake ni Mkurugenzi Mkuu wa TBC, ianze mara moja kupitia utekelezaji wa bajeti mpya ya mwaka 2018 na kuchukua hatua stahili kwenye maeneo yaliyoainishwa na CAG,” alisema.

Pia alisema wakati hoja nyingine zikifanyiwa kazi, Star Media itatoa Sh bilioni tatu kwa TBC kama ruzuku kwa mwaka huu wa fedha.

Dk. Mwakyembe alitoa agizo kwa Bodi ya TBC na Mwenyekiti wa Star Media Tanzania kusimamia kwa ukaribu na kikamilifu utekelezwaji wa hoja zote zilizopo katika mkataba huo.

“Wizara yangu itafuatilia kwa karibu utekelezaji na haitasita kuchukua hatua kali za kisheria na kinidhamu kwa mtendaji wa upande wowote atakayekuwa kikwazo katika uendeshaji kampuni,” alisema.

Alisema pamoja na udhaifu wa uendeshaji uliobainika, ubia huo uliwezesha kuhamisha matangazo ya runinga nchini kutoka katika mfumo wa analojia kwenda kidijitali.

SEKTA YA VIWANDA

Akijibu hoja za CAG zilizoibuliwa, Mwijage, alisema taarifa ya CAG ilieleza sekta hiyo inachangia asilimia 35 katika Pato la Taifa kiwango ambacho si cha kuridhisha kulinganisha na matarajio ya asilimia 40.

Mwijage alisema kwa mwenendo uliopo, uchangiaji wa asilimia 40 kama ilivyotarajiwa utafikiwa ifikapo mwaka 2025 hasa ikizingatiwa mwaka 2012 mchango wa sekta hiyo katika Pato la Taifa ulifikia asilimia 28 na mwaka 2017 ulifikia asilimia 35.

“Kwa kulinganisha mchango wa sekta hii kwa Tanzania katika Pato la Taifa na nchi nyingine bado nchi yetu inafanya vizuri. Kenya sekta hiyo inachangia asilimia 25, Uganda asilimia 20, Afrika Kusini asilimia 36, India asilimia 40 ikiwa imeajiri watu milioni 120 na Tanzania milioni sita. Malaysia asilimia 40, China asilimia 60 na katika nchi za Umoja wa Ulaya (EU) sekta hiyo inachangia asilimia 50 kigezo cha ajira ni watu 249 na Tanzania watu 99,” alisema.

Kuhusu kiwango cha asilimia nane cha kufungwa kwa shughuli za ujasiriamali zilizoanzishwa kama ambavyo CAG alivyobainisha, alisema kiwango cha Tanzania kufunga biashara ni kidogo.

Alisema wastani wa dunia ni zaidi ya asilimia 50 ya biashara zilizoanzishwa hufungwa katika kipindi cha miaka mitano.

“Hata katika nchi zinazoendelea Marekani na Canada, kiwango cha kufunga biashara zilizoanzishwa katika miaka mitano kinafikia asilimia 50,” alisema.

Pia alisema wizara itaendelea kuweka mazingira mazuri kutoa elimu za kuendesha biashara kwa wajasiriamali ili pengo la ufungwaji biashara zilizoanzishwa liendelee kupungua.

Kuhusu mchango hafifu wa asilimia moja katika mauzo ya nje kwa bidhaa za viwandani, Mwijage, alisema wizara inaandaa mkakati wa kukuza wajasiriamali watakaowezesha kukua kuwezesha kushiriki kuuza bidhaa za nje.

Alizitaja sababu nyingine ni bidhaa nyingi za wajasiriamali kuuzwa nje ya nchi bila kuwepo utaratibu rasmi, hivyo kukosa kumbukumbu sahihi za mauzo.

Hoja nyingi ya CAG ambayo Mwijage aliijibu ni uchakavu wa teknolojia za karakana za Sidon na alisema Serikali ilitambua mapema uchakavu wa karakana hizo katika mikoa saba kwa sababu zina zaidi ya miaka 30.

“Kwa kutambua hilo, wizara katika bajeti ya mwaka wa fedha wa 2018/2019, imetenga shilingi bilioni tano kuanza kuzifanyia maboresho karakana hizo,” alisema.

Mwijage pia alisema bajeti ndogo ya maendeleo inayoelekezwa Sido, kwa mwaka wa fedha 2017/2018 ilitengewa Sh bilioni 14.1 ikilinganishwa na mwaka uliopita iliyotengewa Sh bilioni 26.8.

 SABABU ZA CAG KUJIBIWA

Kuhusu sababu ya Serikali kujibu hoja za CAG kupitia waandishi wa habari tofauti na ilivyozoeleka, Waziri wa Fedha na Mipango, Dk. Philip Mpango, alisema sheria zinawataka wawasilishe bungeni majibu ya hoja zote za mkaguzi siku ambayo ripoti yake anaiwasilisha bungeni.

Alisema Sheria ya Ukaguzi wa Umma, sura 418 kifungu cha 38 (3) ndicho kinachoitaka Serikali kuwasilisha bungeni majibu ya hoja za CAG.

Alisema miaka ya nyuma walikuwa wakikaa kimya bila kusema kwa umma, lakini sasa wameona watoe pia kwa umma majibu ya hoja zilizotolewa na CAG kwa kuwa ripoti hiyo ikishafika bungeni inakuwa ya umma.

“Jana (juzi) nilieleza kuwa baada ya CAG kuwasilisha bungeni taarifa yake, Sheria ya Ukaguzi wa Umma sura ya 418, kifungu cha 38 (3), kinaitaka Serikali kuwasilisha bungeni majibu ya hoja za CAG na mpango kazi wa utekelezaji mapendekezo ya CAG,” alisema.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles