MWAKINYO SASA AMTAMANI AMIR KHAN

0
1146

LONDON, ENGLANDBONDIA Hassan Mwakinyo wa Tanzania, ametangaza nia ya kuzichapa na bondia maarufu kutoka Uingereza, Amir Khan.

Mwakinyo kwa sasa amepanda hadi nafasi ya 16 kati ya orodha ya mabondia 1,830, inayoongozwa na Khan.

Mwakinyo (23), Jumamosi iliyopita alimtandika Mwingereza, Sam Eggington (25), katika raundi ya pili na sasa yupo tayari kupambana na Khan.

Pambano la Mwakinyo na Eggington la uzito wa kati, lilikuwa la utangulizi kabla ya pambano kubwa la Amir Khan dhidi ya Samuel Vargas. Khan alishinda kwa tofauti ya alama dhidi ya Vargas.

Mwakinyo aliingia katika ulingo wa Arena Birmingham, jijini Birmingham Uingereza kama mbadala wa bondia mwingine aliyetakiwa kupambana na Eggington kushindwa kufikia vigezo.

Wachambuzi wengi wa masuala ya masumbwi waliliona pambano hilo kuwa rahisi kwa Eggignton ambaye alikuwa na rekodi bora zaidi.

Wakati Mwakinyo akiwa na rekodi ya kushinda mapambano 11 na kupigwa mawili, mpinzani wake alikuwa ameshinda mapambano 24 na kupigwa manne. Eggignton pia ni bingwa wa zamani wa Uingereza, Ulaya na nchi za Jumuiya ya Madola.

Haikuchukua muda mrefu toka pambano lianze kwa Mwakinyo kufurumusha mvua ya makonde kwa Eggington.

Mwakinyo alianza raundi ya pili kwa kasi aliyomaliza nayo raundi ya kwanza na baada ya kumsukumia makonde kadhaa bila majibu, mwamuzi wa mchezo huo, Kevin Parker, alilazimika kumnusuru Eggington kwa kumaliza pambano hilo.

Mara baada ya ushindi huo, Mwakinyo alisikika akiimba kuwa anataka kupambana na bondia mwingine kutoka Uingereza, Kell Brook.

“Eggington aliingia ulingoni akiwa mwenye kujiamini sana. Nilitaka kuonesha uwezo wangu, siye wengine ni mabingwa pia lakini hatuonekani kutokana na mazingira tunayoishi,” alisema Mwakinyo baada ya pambano hilo na kuongeza: “Nimefurahi sana kwa ushindi huu na nimeionesha dunia uwezo wangu halisi.”

“Sasa nataka kupambana na Kell Brook, nikishamchapa namtaka Amir Khan.” Alipoulizwa kama wataweza kustahimili nguvu za Brook akajibu kwa kujiamini: “Kwani wanionaje?”

Wakati huo huo, Serikali imempongeza Mwakinyo kwa ushindi alioupata baada ya kumtwanga bondia Eggington na kusema kuwa matokeo hayo yanatokana na mabadiliko ya kikatiba na kanuni yaliyofanyika katika kusimamia ngumi za kulipwa nchini.

Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk. Harrison Mwakyembe, alisema hayo bungeni jijini Dodoma, alipokuwa akijibu mwongozo wa Mbunge wa Tarime Mjini (Chadema), Ester Matiko, aliyehoji kwanini Serikali haiwaandai mabondia lakini imekuwa ikiwapongeza pindi wanapofanya mazoezi.

Dk. Mwakyembe alisema Serikali imefanya juhudi kuhakikisha mabondia wananufaika na kwamba nchi ilikuwa haina uratibu kwa miaka yote kwa sababu sera ilikuwa haitambui ngumi za kulipwa na hata kwenye sheria.

“Tumevunja kwanza vyombo vyote vilivyokuwa vikisimamia ngumi za kulipwa ambapo kila kimoja kilikuwa kikipeleka wanamasumbwi nje ya nchi na ndio maana walikuwa wakipigwa,” alisema.

 

 

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here