24.4 C
Dar es Salaam
Tuesday, April 23, 2024

Contact us: [email protected]

Mwaka 2020 funga kazi upinzani

ANDREW MSECHU-DAR ES SALAAM

KIONGOZI wa Chama cha ACT Wazalendo, Zitto Kabwe, amesema anatamani kuwania urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na yuko tayari kuwania nafasi hiyo, iwapo atapitishwa kupitia muungano wa vyama vya siasa.

Akizungumza na wanahabari jana, Zitto alisema nafasi hiyo itampa fursa ya kuijenga Tanzania inayopaa kiuchumi, ambayo kutokana na maoni mengi ya Watanzania aliowatembelea wanaihitaji.

Alisema chama chake kimejipanga na kiko tayari kuhakikisha kinajenga uwezo na kuhakikisha wananchi wanafaidika na rasilimali za taifa na kutumia jiografia kufaidika kiuchumi.

Zitto alisema katika kuelekea Uchaguzi Mkuu wa 2020, chama chake kinaendelea kukutana na vyama vingine ili kujenga ushirikiano wa vyama vya upinzani utakaoviwezesha kuiondoa CCM madarakani.

“Tayari tumekuwa katika mazungumzo na vyama vinane vya siasa nchini na tunaendelea kuvikaribisha vyama vingine kuunganisha nguvu kwa kujenga ushirikiano wa vyama vya siasa kuiondoa CCM madarakani,” alisema Zitto.

Matarajio ya 2020

Zitto alisema kwa mwaka 2020 ambao ni wa uchaguzi, ACT Wazalendo imedhamiria kuijenga Tanzania inayopaa kiuchumi kwa kubuni na kutekeleza sera zitakazohakikisha uchumi shirikishi unaozalisha ajira.

Alisema ni muhimu kwa wananchi kufahamu kuwa Chama cha ACT Wazalendo kinajiandaa kuongoza Serikali itakayovutia uwekezaji kutoka nje (FDI) ili kuongeza mitaji nchini na kupanua wigo wa ajira, shughuli za uzalishaji na kutekeleza sera sahihi zitakazogusa uwezo wa kufaidika na rasilimali za madini, misitu, mafuta na gesi.

“Ninataka pia tuongeze idadi ya watalii nchini kufikia watalii milioni sita kwa mwaka ili kutengeneza ajira nyingi na bora, pia kuongeza mapato ya fedha za kigeni,” alisema Zitto.

Alisema katika mikakati ya chama chake, anataka kuongoza Serikali itakayotumia nafasi ya Tanzania kijiografia ya kuzungukwa na nchi nyingi zisizo na bahari kufaidika kiuchumi na kuhudumia nchi nyingine kwa kuifanya kuwa kituo kikuu cha kibiashara katika maeneo ya maziwa makuu.

“Lakini pia ninataka kuwekeza zaidi kwenye shughuli za wananchi wengi, hasa kilimo, kwa kuongeza eneo linalotumika kwa kilimo cha umwagiliaji, uvuvi na ufugaji.

“Lengo la yote haya ni kuongeza shughuli za kiuchumi kwa watu. Uchumi wa watu ndio unaojenga taifa imara na si uchumi wa Serikali,” alisema Zitto.

Alisema ACT Wazalendo inaiwaza Tanzania yenye huduma bora za kijamii, kutoa elimu bora inayokwenda na wakati, inayozalisha wahitimu wenye weledi, ubunifu na uwezo katika nyakati hizi za sayansi na teknolojia, wakufunzi wa kutosha, madarasa na vitendea kazi, huku ikiweka mkazo kwenye elimu ya ufundi.

Zitto alisema lengo lao ni kufikia huduma bora na nafuu za afya, inayojikita kwenye kuwakinga na kuwatibu wananchi kwa kuwa na zahanati, vituo vya afya na hospitali za kutosha, zenye watendaji wenye sifa, vitendea kazi na vifaa tiba vya kutosha, pia kuwa na huduma bora na ya uhakika ya maji safi na salama, kipaumbele ikiwa ni kupunguza maradhi yatokanayo na matumizi ya maji yasiyo salama.

“Lengo la ACT Wazalendo wakati ikielekea katika Uchaguzi Mkuu ni kujenga mifumo imara ya utoaji haki nchini kwa kujenga uwezo wa kupambana na rushwa, kuondoa vikwazo vinavyotuhakikishia watu wote walioonewa katika kipindi cha miaka hii minne kwa kubambikiwa kesi kwanza wanaachiwa huru, na wale waliohukumiwa adhabu mbalimbali wakifutiwa rekodi zao za adhabu,” alisema Zitto.

Alisema ni wazi kwamba mazingira ya kisiasa nchini kwa sasa yamebadilika na kwamba hilo linadhihirishwa na yaliyotokea kwenye Uchaguzi wa Serikali za Mitaa Novemba mwaka jana.

Alidai katika uchaguzi huo chama tawala kiliamua kuingilia kati na kuvuruga uchaguzi huo.

 “Tunashuhudia, hivi karibuni tumetoka kwenye Uchaguzi wa Serikali za Mitaa ambao mchakato wake mzima umeporwa. Lazima tuseme kuwa tunapoelekea kwenye Uchaguzi Mkuu wa 2020 lazima tubadilishe namna ya kufanya siasa na kulinda matokeo yetu,” alisema Zitto.

KAULI YA MAALIM SEIF

Akizungumza katika mkutano huo, Mshauri Mkuu wa ACT Wazalendo, Maalim Seif Sharif Hamad, alisema iwapo atakutana na Rais wa Zanzibar, Dk. Ali Mohamed Shein kwa sasa yuko tayari kusalimiana naye na kumshika mkono, tofauti na awali, ambapo aliwahi kumnyima mkono hadharani.

Maalim Seif alisema alimnyima Rais Shein mkono kwa kuwa alitaka ujumbe ufike, na kwa kuwa tayari ujumbe ulishafika, hana chuki wala hana uhasama na mtu yeyote.

Akitoa salamu zake kuelekea mwaka 2020, Maalim Seif alisema ACT Wazalendo inautangaza mwaka 2020 kuwa ni mwaka wa kuing’oa CCM na yeye binafsi ataongoza juhudi za kuunda umoja wa dhati utakaovishirikisha vyama vyote makini vya siasa, asasi za kiraia, vyama vya kitaaluma na makundi yote ya kijamii, ambao utawaongoza Watanzania.

Alitoa wito kwa viongozi wa vyama vyote vya siasa, pamoja na changamoto kadhaa zilizopo miongoni mwa vyama, bado masilahi yanayowaunganisha kwa madhumuni ya kuing’oa CCM ni makubwa zaidi kuliko tofauti zao, hivyo ni wakati wa kuziweka tofauti zao pembeni ili kuwaunganisha Watanzania pamoja kuing’oa CCM 2020.

“Huu utakuwa ni mwaka ambao Watanzania tunakwenda kuandika historia, historia ya kwenda kuyazika madhila haya na kujiletea mabadiliko mema yatakayobadilisha maisha yetu.

“Mwaka 2020 ni mwaka wa vitendo, wa kuleta mabadiliko ya kweli na kumaliza ulaghai wa watawala wa CCM.

“Mwaka 2020 ni mwaka wa kuhitimisha uongo wa watawala wa CCM, watawala ambao kila ikifika miaka mitano wamekuwa mahodari wa kutoa ahadi mpya bila ya kutueleza Watanzania kwanini ahadi zilizopita ambazo wamekuwa wakizitoa miaka nenda miaka rudi wameshindwa kuzitekeleza,” alisema Maalim Seif.

Alisema yeye na kiongozi wa chama, Zitto wanaongoza ziara waliyoipa jina la ‘Listening Tour’ ambayo lengo lake ni kuwashirikisha wananchi katika maandalizi ya ilani zao kwa kusikiliza maoni yao kuhusu maeneo yapi wangependa kuyaona yanazingatiwa katika ilani hizo, kwa maana ya Ilani ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Ilani ya Zanzibar.

Alisema Serikali ya CCM imepandikiza mbegu za ubaguzi miongoni mwa Wazanzibari kwa kitendo cha Serikali iliyopo kuwapa haki watu wa kundi moja na kuwanyima wengine.

“Haya yanadhihirika katika suala zima la ajira, hivi leo ambapo kijana wa Kizanzibari haajiriwi kwa uwezo wake bali anaajiriwa kwa kuangaliwa amezaliwa wapi na amezaliwa na nani kwa itikadi za kisiasa. Pia hata vyeo navyo vinagawiwa kwa misingi hii hii.

“GSO tuliyoitarajia kufanya kazi ya kuhakikisha usalama wa nchi, leo imegeuka kuwa kikundi cha kupita mitaani kutafuta itikadi za kisiasa za wanaoomba ajira wao na za wazazi wao,” alisema Maalim Seif.

Alisema ubaguzi pia umehamia hata katika kupata nyaraka na huduma muhimu kama vile vyeti vya kuzaliwa na vitambulisho vya Mzanzibari ambavyo hutumika kwa matumizi mbalimbali, ikiwa ni pamoja na haki ya kujiandikisha katika daftari la wapigakura, kusafiria, benki, huduma za miamala ya simu, pia kwa wanafunzi wanaojiunga na elimu ya juu.

“Kwa masikitiko makubwa, vitambulisho hivi navyo hutolewa kwa ubaguzi kutegemeana na itikadi ya mtu ya kisiasa anayodhaniwa kuwa nayo.

“Wananchi wananyimwa haki zao za msingi na wengine kuharibiwa hatima za maisha yao kwa kunyimwa kitambulisho hiki,” alisema Maalim Seif.

Alidai kuna taarifa za fedha za wawekezaji, ambazo wakubwa serikalini wamezifanya ngawira kwa kugawana miongoni mwao, hivyo miradi kadhaa imeshindwa kuendelezwa kwa sababu za kifisadi.

Maalim Seif alidai hali ya maisha kwa wananchi wa Zanzibar imezidi kuwa mbaya, kipato cha mwananchi mmoja mmoja kimepungua maradufu, uchumi unashuka kila uchao hata kama watawala wanajitahidi kutoa takwimu za kukua kwa uchumi.

Alidai katika robo ya kwanza ya mwaka huu wa fedha, SMZ imetumia fedha nyingi zadi kwenye matumizi mengineyo kuliko hata mishahara ya wafanyakazi na sehemu kubwa ya fedha hizo ni kutoka Mfuko wa ZSSF.

Maalim Seif alidai kuwa shirika hilo lilitoa mkopo mpya kwa SMZ kiasi cha deni la ndani kufikia Sh bilioni 141 kutoka Sh bilioni 108 mwaka unaoishia Septemba 2018.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles