26.2 C
Dar es Salaam
Friday, March 29, 2024

Contact us: [email protected]

Mvua yaua watoto wawili, shule zafungwa Dar

LEONARD MANG’OHA-DAR ES SALAAM

JESHI la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, limesema   mvua inayoendelea kunyesha jijini humo imesababisha vifo vya watoto wawili.

Akizungumza na waandishi wa habari   Dar es Salaam jana  Kamanda wa Polisi wa Kanda Maalumu, Lazaro Mambosasa,  alisema Mei 5 mwaka huu   alasiri maeneo ya Matosa Goba Wilaya ya Kinondoni   ulipatikana na mwili wa mtoto   Francis Byabato baada ya kutoweka kwa siku mbili.

Kamanda Mambosasa alisema mtoto huyo alipatikana akiwa amefariki dunia ndani ya kisima cha futi 30 kilichokuwa wazi, nyumbani kwao.

“Tukio jingine ni la Mei 12  maeneo la Mongo la Ndege,  ambako uliokotwa mwili wa mtoto wa kiume anayekadiriwa kuwa na umri wa miaka minne hadi mitano ambaye hajafahamika jina.

“Mwili huo ulikuwa ukielea katika Mto Msimbazi ukiwa hauna jeraha lolote, mwili huo umehifadhiwa katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili,” alisema Mambosasa.

Alisema mvua hiyo  inayoendelea kunyesha   pia  imesababisha uharibifu wa majengo ya Shule ya Msinge Mwale na Majani ya Chai zote za Kiwalani Wilaya ya Ilala   na Shule ya Sekondari Kibasila katika Wilaya ya Temeke ambayo imejaa maji na kusababisha kusimamishwa     kwa muda.

“Pia mvua hii  imesababisha kufungwa   baadhi ya barabara ikiwamo Barabara ya Morogoro eneo la Jangwani ambayo ilifungwa tangu saa 10 alfajiri na barabara ya Kawawa eneo la Mkwajuni ambayo magari madogo hayaruhusiwi kupita mpaka maji yatakapopungua  na kujiridhishakuwa eneo hilo ni salama.

“Jeshi la Polisi linatoa wito kwa wakazi wa   Dar es Salaam kuchukua tahadhari dhidi ya mvua inayoendelea kunyesha, sambamba na kuwa makini na watoto wenye umri mdogo. Pia tunaendela kufuatilia taarifa ya mvua  inayoendelea kunyesha,” alisema Mambosasa.      

Mapema jana asubuhi, Mkuu wa Idara ya Mawasiliano ya Kampuni ya UDA-RT, Deus Buganywa, alitoa taarifa ya kusimamishwa   huduma ya usafiri wa mabasi yaendayo haraka  kati ya Kimara – Kivukoni,   Kimara – Gerezani, Morroco – Kivukoni na Morroco – Gerezani.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, huduma hizo zilisimamishwa kuanzia saa 10: 30 alfajiri ya jana kutokana na eneo hilo la Jangwani kujaa maji.

“Huduma zinazotolewa sasa ni kati ya Kimara – Mbezi, Kimara – Magomeni Mapipa, Kimara – Morroco, Gerezani – Muhimbili, Kivukoni – Muhimbili na Gerezani – Kivukoni.

“Tunaendelea kufuatilia  hali ya maji katika eneo husika, maji yakipungua huduma zitarejea katika hali ya kawaida. Tunaomba radhi kwa usumbufu unatokana na kusimamishwa  safari hizo,” alisema.

Wakati huo huo, Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) imetoa angalizo la kuwapo mvua kubwa kwa mikoa ya Dar es Salaam, Pwani, Tanga na Visiwa vya Unguja na Pemba kuanzia leo hadi Mei 18 mwaka huu.

Taarifa ya TMA pia metoa angalizo la kuwapo upepo mkali na mawimbi makubwa katika baadhi ya maeneo ya ukanda wa Pwani kwa kipindi chote cha kuanzia leo.

Jana,  MTANZANIA lilishuhudia msongamano mkubwa wa magari katika barabara nyingi za kuingia na kutoka katikati ya jiji hilo, ikiwamo barabara ya Bagamoyo, kutokana na magari mengi kulazimika kutumia njia hiyo baada ya kufungwa  barabara ya Morogoro.

Katika eneo la Jangwani licha ya kufungwa,  wananchi wengi walionekana wakivuka kwa miguu na baadhi yao wakitumia mikokoteni maarufu, kwa jina la guta, ambayo   iligeuka   biashara kubwa.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles