24.2 C
Dar es Salaam
Friday, April 19, 2024

Contact us: [email protected]

Mvua yaua sita Mwanza, Kagera

Baadhi ya wakazi wa Mwanza wakiangalia nyumba iliyoporomokewa na mwamba katika Mtaa wa Nyerere A Sinai-Mabatini jana.
Baadhi ya wakazi wa Mwanza wakiangalia nyumba iliyoporomokewa na mwamba katika Mtaa wa Nyerere A Sinai-Mabatini jana.

SITTA TUMMA NA RENATHA KIPAKA

WATU sita wamefariki dunia na wengine saba kujeruhiwa katika matukio mawili tofauti yaliyoambatana na mvua katika mikoa ya Mwanza na Kagera.

Katika tukio la jijini Mwanza, vilio na simanzi jana vilitawala kwa wakazi wa maeneo ya Sinai-Mabatini, baada ya vifo vya watu wanne wa familia mbili tofauti, vilivyotokana na mvua iliyosababisha miamba mikubwa ya mawe kuporomoka na kuponda nyumba zao usiku wa manane.

Tukio hilo la kusikitisha limeripotiwa kutokea saa nane usiku kuamkia jana, wakati mvua iliyoambatana na upepo wa wastani ilipokuwa ikiendelea kunyesha, na kusababisha miamba hiyo mikubwa inayokadiriwa kufikia tani mbili kuporomoka na kuziponda nyumba hizo na kusababisha vifo hivyo na majeruhi wanne.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Valentino Mlowola, alithibitisha kutokea kwa tukio hilo na kuwataka wananchi kuchukua tahadhari wakati wa mvua.

MTANZANIA Jumapili lilifanikiwa kufika eneo la tukio na kushuhudia miamba hiyo ikiwa imeharibu nyumba, huku nyumba moja iliyojengwa kwa matofali ya tope ikiwa imeanguka na kubaki kifusi.

Nyumba zilizokumbwa na maafa hayo zinamilikiwa na watu waliotajwa kwa majina ya Joseph William na Lameck Ajiji, na kila moja watu wawili wamefariki kwa kukandamizwa na miamba hiyo.

Katika nyumba ya William iliyokuwa na watu watano, waliofariki wametajwa kuwa ni Kefa Joseph (15) na Emmanuel Joseph (12), wote mwanafunzi wa Shule ya Msingi Mbugani na majeruhi mmoja ambaye hakufahamika jina lake ambaye alikimbizwa hospitali.

Nyumba inayomilikiwa na Ajiji yenye watu watatu, waliofariki wametambuliwa kuwa ni mama wa nyumba hiyo, Kwinta Geko (24) na mumewe Samson Odinya.

Waliojeruhiwa ni mtoto Bety Samson (4) na Godfrey Joseph (14) mwanafunzi wa Shule ya Msingi Mbugani.

Tukio hilo ni la pili kutokea katika eneo hilo la Sinai. Mara ya kwanza ilikuwa ni mwaka 2009 baada ya miamba kuporomoka na kusababisha vifo vya watu wawili wa familia moja.

Tukio la jana lilivuta hisia tofauti kwa wakazi wa Jiji la Mwanza, huku wengine wakiangua vilio.

Mamia ya wananchi waliofika eneo hilo, walijitolea kwa kumpa fedha mtoto Bety aliyenusurika kufa kutokana na tukio hilo.

Mbunge wa Nyamagana jijini Mwanza, Ezekiel Wenje (Chadema), alifika eneo la tukio na kutoa pole kwa wananchi, ndugu jamaa na marafiki wa familia zilizoathirika na janga hilo, ambapo alionyesha kushtuka baada ya kuelezwa na wananchi kwamba hakuna kiongozi yeyote wa Serikali aliyefika eneo hilo.

Akizungumza kwa kutumia kipaza sauti mbele ya umati wa watu waliokuwa wamefurika katika eneo hilo la tukio, alisema: “Inashangaza sana kuona hata mkuu wa wilaya hajafika hapa. Nitawasiliana na viongozi wa Serikali na mchana nitarudi hapa tena.”

Baadhi ya wananchi waliozungumza na MTANZANIA Jumapili katika eneo la tukio, waliiomba Serikali kuzuia wananchi kujenga karibu na miamba mikubwa, kwani kufanya hivyo itasaidia sana kuepusha maafa kama hayo.

“Kwa kweli tukio hili linasikitisha sana, na tunaomba viongozi wa serikali wasaidie wananchi kuwaondosha kwenye maeneo ya kwenye miamba,” alisema mmoja wa wananchi hao ambaye pia ni balozi wa Shina Namba Tano, Mtaa wa Nyerere A, Jackson Kitundu.

Katika tukio jingine, watu wawili wa familia mojawakazi wa Kitongoji cha Kaburi, Kata ya Kanoni wilayani Karagwe, wamefariki dunia papo hapo na wengine watatu kujeruhiwa baada ya kupigwa na radi.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kagera, Henry Mwaibambe, amethibisha tukio hilo na kusema lilitokea juzi mchana baada ya mvua kubwa kunyesha ikiambatana na upepo mkali pamoja na radi.

Waliofariki dunia wametajwa kuwa ni Coletha Porotas (30) na Onesimo Nestori (14), huku waliojeruhiwa ni Emmanuel Jeremia (44), Tumsifu Emmanuel (10) na Jovinus Nestori (10), wote wakazi wa Kitongoji cha Kaburi, Kijiji cha Kanoni, Wilaya ya Karagwe mkoani Kagera.

Akizungumzia tukio hilo, Mwenyekiti wa Kitongoji cha Kaburi, Willison Kristian, alisema mvua hiyo iliyonyesha kwa takribani saa moja, iliambatana na mawe, upepo mkali na radi.

Kristian alisema radi hiyo iliwakuta watu hao ndani nyumba tofauti katika kijiji hicho na kuwarusha nje.

- Advertisement -

Related Articles

2 COMMENTS

  1. nawapa pole sana wote walopata maswaib ya nvua. naomba serikali au mbunge wa nyamagana aangalie jinsi ya kunsaidia huyo mtoto alieachwa na wazazi wake kusudi aweze pata mahitaji muhimu na hasa elimu

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles