26.2 C
Dar es Salaam
Friday, March 29, 2024

Contact us: [email protected]

Mvua yabomoa nyumba, yasomba madaraja Bahi

Ramadhan Hassan-Bahi

ZAIDI ya nyumba 120 zimebomoka na madaraja kuharibika Wilaya ya Bahi mkoani Dodoma, kutokana na mvua zinazoendelea kunyesha.

Maeneo yaliyoathiriwa na mvua hizo ni Bahi Sokoni, Bahi Misheni, Mji mpya, Nkogwa, Mbuyuni, Uhelela, Laloi, Mugu na Nagulo.

Juzi Mkuu wa Wilaya, Mwanahamisi Mukunda akiongozana na wataalamu wa Halmashauri ya Bahi na watendaji wa vijiji, walitembelea baadhi ya wakazi walioathirika na mafuriko hayo na madaraja ambayo yameharibika.

Akizungumza na waandishi wa habari, Mwenyekiti wa Kijiji cha Sokoni, Sifael Mbeti alisema mvua imesababisha mito mingi kufurika na hivyo kusababisha maji kuleta madhara kwa kubomoa nyumba na madaraja.

“Wazazi waangalie watoto wao wanaoogelea ovyo na hiyo ni hatari kwa maisha yao,” alisema.

Ofisa Mtendaji wa Kijiji cha Bahi Sokoni, Fredrick Kachiwile alisema zaidi ya nyumba 86 katika kijiji hicho zimebomoka.

Alisema katika Kijiji cha Uhelela taarifa za awali zinaonyesha nyumba 35 zilibomoka na katika Kijiji cha Nagulo barabara imekatika na mawasiliano ni ya shida.

Mwenyekiti wa Kijiji cha Nagulo, Ashery Silla alisema jumla ya nyumba 18 zimeanguka.

Naye mkazi wa Kitongoji cha Miembeni Bahi Mwanachugu, Issa Rashidi alisema mvua zilizonyesha juzi zimeleta madhara makubwa ikiwa ni pamoja na maji kuzidi kujaa kwenye Mto Nkongwa na kuanza kusambaa kwenye makazi ya watu.

“Mto ulihama kutokana na kujaa mchanga, maji yalivyoanza kuzagaa kwenye makazi ya watu wananchi walianza kupiga kelele ndipo walipofika mtoni na kujitolea kujaza mchanga kwenye viroba na kuweka kwenye sehemu ya kingo ya mto iliyopasuka,” alisema Rashidi.

Alisema maji hayo yalitoka kwenye vijiji vya Msisi na Mundemu.

Akizungumzia hali hiyo, Mkuu wa Wilaya ya Bahi, Mukunda, aliwataka wananchi kuendelea kuchukua tahadhari kufuatia mvua zinazoendelea kunyesha.

Alisema mito mingi imekuwa ikiishia katika Wilaya ya Bahi hali ambayo inasababisha maji kuingia kwenye makazi ya watu kutokana na uharibifu wa mazingira na kuharibiwa kwa kingo za mito.

“Tuendelee kuchukua tahadhali, tuliomba kiasi cha Sh milioni 400 kwa ajili ya ukarabati wa miundombinu ikiwemo madaraja, na fedha hizo tumeshazipata na zitafanya kazi iliyokusudiwa,” alisema Mukunda.

Alisema Serikali iko makini kuhakikisha shughuli za kiuchumi hazisimami kwa sababu ya mvua.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles