MUSWADA WA TAKWIMU WATUA TENA BUNGENI

0
757

Na ESTHER MBUSSI,DODOMAMuswada wa Marekebisho ya Sheria ya Takwimu umetinga bungeni, ambapo pamoja na mambo mengine, utamwongezea mamlaka Mtakwimu Mkuu kuanzisha, kurekebisha au kufuta takwimu rasmi zilizokusanywa kwa njia ya tafiti au sensa, bila kuwa na kibali cha Mtakwimu Mkuu ambapo atakayekiuka hayo atakuwa ametenda kosa la jinai.

Aidha, muswada huo ambao umo katika Muswada wa Marekebisho ya Mbalimbali Namba tatu, unaopendekeza marekebisho ya sheria sita, ikiwamo Sheria ya Mamlaka ya Rufaa, Sheria ya Uendeshaji wa Mashauri ya Jinai, Sheria ya Mahakama za Utatuzi wa Migogoro ya Ardhi, Sheria ya Mahakama za Mahakimu na sheria ya Baraza la Taifa la Michezo Tanzania, uliwasilishwa jana na Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Dk. Adelardus Kilangi.

Akiwasilisha muswada huo, Dk. Kilangi alisema lengo ni kuboresha na kuimarisha utekelezaji wa sheria hizo kwa kuondoa upungufu ulioonekana wakati wa kuzitumia na kuweka masharti mengine ili kuleta uwiano kati ya sheria zinazorekebishwa na zilizopo, kwa kufuta, kurekebisha na kuandika upya maneno kwenye vifungu hivyo na kuandika maneno mapya.

SHERIA YA TAKWIMU

Dk. Kilangi alisema katika sheria hiyo sehemu ya saba, sura ya 351, Serikali inapendekeza kufutwa kwa kifungu cha 37 (4), na kukiandika upya kwa kuweka masharti, kuwa mtu yeyote atakayechapisha au kusambaza takwimu rasimu au taarifa za kitakwimu kinyume na sheria hiyo, atakuwa ametenda kosa la jinai.

Alisema kwamba, marekebisho hayo yanalenga kuhakikisha masharti kuhusu uchapishaji au usambazaji wa takwimu rasimu au taarifa za kitakwimu, yanatekelezwa ipasavyo.

“Marekebisho mengine katika sehemu hii yanayopendekezwa ni kuongeza kifungu kipya cha 24A, ambacho kinaweka masharti kuwa mtu aliyepata kibali kutumia takwimu rasmi za Ofisi ya Taifa ya Takwimu, hatachapisha au kutoa taarifa husika kwa umma bila kupata kibali kutoka ofisi hiyo.

“Sehemu hii pia inapendekeza pia kurekebisha kifungu cha tatu cha Sheria ya Takwimu kwa kuandika upya tafsiri ya maneno ‘official statstics’ ambayo inamaanisha takwimu zilizopatikana, kuhakikiwa, kuunganishwa au kusambazwa na au kwa mamlaka ya ofisi ya takwimu, lengo la marekebisho haya ni kutofautisha takwimu rasmi na takwimu nyingine zinazotolewa na taasisi au watu wengine.

“Aidha, kifungu cha 17(3)(a) na (b) cha sheria hiyo, kinaelezea kuwa, ofisi ya takwimu ya Taifa katika kutekeleza jukumu la utaratibu wa takwimu chini ya sheria hiyo, inatoa kanuni za utendaji ambazo zitazingatiwa na wakala zinazotoa takwimu rasmi na kwamba ofisi hiyo itaandaa benki ya takwimu iliyoanzishwa na wakala husika,” alisema.

Pamoja na mambo mengine, Dk. Kilangi alisema kifungu hicho kirekebishwe kwa kuweka masharti yatakayowezesha kanuni za utendaji kazi kuzingatiwa pia na taasisi nyingine za Serikali na ofisi ya Taifa ya Takwimu kutumia benki ya takwimu ya taasisi za Serikali.

SHERIA MASHAURI YA MADAI

Katika sheria hiyo, Dk. Kilangi alisema sheria hiyo inaweka masharti kuhusu utaratibu wa masuala muhimu katika uendeshaji wa mashauri ya madai katika Mahakama Kuu, Mahakama ya Hakimu Mkazi na Mahakama ya Wilaya.

“Kwa ujumla marekebisho katika sehemu ya pili na ya tatu ya muswada, yanalenga kutekeleza ipasavyo ibara ya 107(2) ya Katiba ambayo inaainisha kanuni za kuzingatiwa na mahakama nchini katika kutoa uamuzi wa mashauri.

“Katika kutekeleza masharti hayo, muswada unaweka mwongozo ambao utazingatiwa na majaji na mahakimu katika kushughulikia madai yaliyoko Mahakama ya Rufani, Mahakama Kuu na Mahakama ya Hakimu Mkazi na Mahakama ya Wilaya,” alisema.

SHERIA MAMLAKA YA RUFAA

Dk. Kilangi akizungumzia marekebisho ya sheria ya Mamlaka ya Rufaa, alisema muswada unapendekeza kifungu kipya cha 3B, ambacho kinaitaka Mahakama ya Rufani kushughulikia jambo linaloletwa mbele yake kwa lengo la kuhakikisha haki inapatikana.

SHERIA YA UTATUZI WA MIGOGORO YA ARDHI

Kuhusu sheria hiyo, Dk. Kilangi alisema marekebisho yanayopendekezwa ni kuongeza kifungu kipya cha 41A kuhusu mamlaka ya nyongeza ambacho kinapendekeza kuweka masharti, kwamba jaji mkuu baada ya kushauriana na waziri mwenye dhamana ya masuala ya sheria pamoja na Mwanasheria Mkuu wa Serikali, atoe amri itakayochapishwa kwenye Gazeti la Serikali ambayo inampatia hakimu mkazi mamlaka ya kusikiliza rufaa au marejeo kutoka Baraza la Ardhi na Nyumba la Wilaya au kutoka baraza la kata.

MAONI YA KAMATI

Akiwasilisha maoni ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba na Sheria, Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Mohamed Mchengerwa, alisema kamati imezingatia ongezeko la usambazaji wa takwimu mbalimbali na matumizi yake chini ya usimamizi usioridhisha.

Alisema hali hiyo mara nyingi imekuwa ikisababisha mkanganyiko mkubwa miongoni mwa jamii jambo ambalo linaweza kuathiri ustawi wa jamii.

KAMBI YA UPINZANI

Akiwasilisha maoni ya Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, Msemaji wa Kambi hiyo, Ally Saleh, alisema mabadiliko yaliyopendekezwa kwenye kifungu cha 24A (i), yana nia ovu ya utafiti unaofanywa nchini.

“Kambi rasmi ya upinzani katika hili la mashauriano, inaona kuna uwezekano ikawa ni kumwambia mtafiti kurekebisha matokeo ya utafiti uendane na matakwa ya Ofisi ya Taifa ya Takwimu au kufutwa kwa utafiti husika.

“Kwa ujumla, kifungu hiki kina nia ovu na utafiti utakaokuwa unafanywa nchini.

“Kambi Rasmi ya Upinzani kwa ujumla inaona kuwa, dhana ambayo ilikusudiwa katika marekebisho yaliyoletwa katika sheria mbalimbali, haionekani katika vifungu vya sheria ambavyo vinapendekezwa kutungwa ili kuwa sheria,” alisema

Akichangia mjadala huo, Mbunge wa Babati Mjini, Pauline Gekul (Chadema), alisema marekebisho ya sheria ya takwimu hayajazingatia matakwa wala uhalisia kwa wananchi.

“Sheria hii imekuja kuwakomoa Twaweza baada ya kutoa takwimu za utafiti ulioonyesha umaarufu wa Rais John Magufuli umeshuka,” alisema.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here