33.2 C
Dar es Salaam
Friday, March 29, 2024

Contact us: [email protected]

Muswada kuruhusu watoto kupima VVU wapitishwa

RAMADHAN HASSAN-DODOMA

 BUNGE limepitisha marekebisho ya Sheria ya Usimamizi na Udhibiti wa VVU na Ukimwi inayoruhusu umri wa kupima virusi vya ugonjwa huo bila ridhaa ya mzazi au mlezi kuwa miaka 15.

Akizungumza jana bungeni, Waziri wa Afya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu, alisema lengo la kuweka umri wa miaka 15 ni kutokomeza maambukizi ya Ukimwi ifikapo mwaka 2030.

Alisema lengo la Serikali ifikapo mwaka 2020 ni kufikia 90, 90, 90, lakini changamoto kubwa ni kuifikia 90 ya kwanza ambayo ni kuhakikisha kila Mtanzania awe amejua hali yake ya maambukizi.

“Mtoto mwenye umri chini ya miaka 15 hakatazwi kupima, lakini apime kwa uangalizi wa wazazi, kwa mujibu wa TDHS ya mwaka 206/17 mihemuko ya kufanya mapenzi inaanzia miaka 15.

“Mwalimu alisema sheria hiyo siyo sheria wala msahafu, endapo ikionekana haifai itabadilishwa,” alisema Ummy.

SERIKALI

Akiwasilisha muswada wa marekebisho ya sheria mbalimbali namba 7 wa mwaka 2019, Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Profesa Aderalus Kilangi, alisema katika Sheria ya Usimamizi na Udhibiti wa VVU na Ukimwi, sura ya 431, inapendekezwa kufanya marekebisho kwa lengo la kujumuisha katika sheria hiyo masharti ya kujipima VVU.

Alisema marekebisho haya yanalenga kuainisha wajibu kwa mtu anayejipima VVU na mtu anayetoa au kusambaza vifaa vya kujipima VVU na kumwezesha waziri kutoa miongozo ili kuhakikisha kuna usimamizi wa viwango vya vifaa vya kujipimia VVU vinavyosambazwa au kuuzwa kwa watumiaji.

“Inapendekezwa pia kuweka wajibu wa kutunza siri kwa mtu anayemsaidia mtu mwingine kujipima na kufanya kitendo cha kutoa siri kuwa kosa chini ya sheria hii.

 “Marekebisho haya yamelenga kuweka bayana umri wa mtoto katika masuala ya upimaji wa virusi vya Ukimwi (VVU) na kueleza maana ya dhana ya kujipima VVU.

“Kifungu cha 16 kinapendekezwa kurekebishwa kwa lengo la kuruhusu majibu ya vipimo ya mtu mwenye umri wa chini ya miaka 18 kutolewa pia kwa mzazi, mlezi au mtu mwingine ambaye mwenye vipimo anamwamini.

KAMATI

Kuhusu suala la umri wa kujipima VVU kwa hiari, kwa watoto chini ya umri wa miaka 15, Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba na Sheria, Mohamed Mchengerwa alisema jambo hilo liliibua mjadala mahsusi, lakini wenye tija kwa ustawi wa taifa wakati wadau wakitoa maoni.

 “Mheshimiwa Spika, pamoja na wadau kupendekeza umri wa mtoto ushuke hadi miaka 12, bado uchambuzi wa kamati kupitia sheria za nchi mbalimbali kama vile Ethiopia, Rwanda, Uganda, Afrika Kusini, Lesotho na nchi nyingine ikiwemo nchi ya Kenya.

 “Pamoja na kupitia miongozo ya Shirika la Afya Duniani (WHO), kamati ilijiridhisha pasipo shaka kuwa suala la umri wa mtoto kujipima kwa hiari linaamuliwa na nchi yenyewe kwa kuzingatia mila na tamaduni na misingi ya maadili ya nchi husika,” alisema.

UPINZANI

Akiwasilisha maoni ya upinzani, Msemaji Mkuu wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni katika Wizara ya Sheria na Katiba, Salome Makamba alisema wanapendekeza kwamba kifungu cha 15 cha muswada huu ambacho kinarekebisha kifungu cha 3 cha sheria mama, kirekebishwe kwa kupunguza miaka kutoka 15 hadi miaka 12.

 “Mheshimiwa Spika, ziko sababu mbalimbali za kufanya mapendekezo haya. Mosi, tayari Tanzania inazo sheria nyingine ambazo zinatambua kuwa mtoto wa miaka 12 anaweza kuwajibika kisheria, sheria ni pamoja na Sheria ya Kanuni ya Adhabu Sura ya 16 ambayo kifungu cha 15(1), (2) na (3) kinatambua kwamba mtu yeyote anaweza kufanya kosa la jinai akiwa na zaidi ya miaka 10, isipokuwa kwenye masuala ya kujamiiana ni kuanzia miaka 12, kwa hiyo marekebisho tunayopendekeza yataendana na kifungu hiki cha sheria hii.

“Mheshimiwa Spika, mwaka 2009 Bunge lilitunga Sheria ya Mtoto Namba 21, pamoja na kwamba kwa sheria hii mtoto ni mtu mwenye umri chini ya miaka 18, lakini kifungu cha 15 cha sheria hii kinampatia mtoto wajibu wa kulinda maadili pamoja na kutumia uwezo wake na akili yake kwa manufaa mapana ya jamii na taifa kwa ujumla,” alisema.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles