MUSWADA BODI YA WALIMU WALIGAWA BUNGE

0
910
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Joyce NdalichakoNa ESTHER MBUSSI,DODOMA

Serikali imewasilisha bungeni Muswada wa Sheria ya Bodi ya Kitaalamu ya Walimu Tanzania ya Mwaka 2018, ambao umeainisha majukumu saba ya chombo hicho huku wabunge wakigawanyika kuhusu mamlaka anayotewa waziri na mswada huo pamoja na adhabu zilizoainishwa.

Akiwasilisha muswada huo bungeni jana, Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Joyce Ndalichako, alisema walengwa katika bodi hiyo ni mwalimu au mtu yeyote aliyefuzu mafunzo ya ualimu katika Chuo cha Ualimu au Chuo Kikuu kinachotambuliwa na mamlaka husika katika ngazi ya Astashahada, Stashahada, na Shahada.

Alisema mwalimu atakayeguswa na sheria hiyo baada ya kupita ni yule anayefundisha katika shule za awali, msingi, sekondari, chuo cha ualimu na chuo au kituo cha elimu ya watu wazima.

Profesa Ndalichako alisema madhumuni ya muswada huo ni kuweka muundo wa kisheria wa usimamizi na uendeshaji wa Bodi ya Kitaalamu ya Walimu ambayo pamoja na mambo mengine itakuwa na jukumu la kuinua kiwango cha utaalamu wa walimu na kuhakikisha  wanakuwa na viwango stahiki kitaaluma na maadili.

Alisema bodi hiyo itakuwa na majukumu ya kuweka viwango vya utaalamu wa ualimu, kusajili walimu wote nchini, kutoa leseni za kufundishia kwa walimu na kuwezesha na kusimamia utoaji wa mafunzo kwa walimu.

Majukumu mengine ni kusimamia maadili ya utaalamu wa ualimu, kufanya tafiti kuhusiana na utaalamu wa ualimu ili kuboresha tasnia na kusikiliza na mashauri dhidi ya mwalimu yanayohusiana na uvunjifu wa Kanuni na Maadili ya Utaalamu wa Ualimu na kuyatolea maamuzi.

Profesa Ndalichako alisema kutokana na idadi kubwa ya walimu kumekuwapo na changamoto zinazohitaji mfumo thabiti wa usimamizi wa ubora wa walimu na taaluma ya ualimu nchini.

“Ualimu ni kada ambayo wahitimu wake ni wengi na hufanya kazi katika maeneo mbalimbali ikiwamo shule, vyuo, taasisi za Serikali na zisiszo za serikali, idadi ya walimu wanaofundisha elimu ya awali hadi vyuo vya ualimu katika sekta ya umma na binafsi iliongezeka kutoka walimu 257,469 mwaka 2012 hadi kufikia walimu 332,740 mwaka 2016.

“Kati ya walimu hao, 293,909 wanafundisha katika shule na vyuo vya serikali na 38,831 wanafundisha katika vyuo vya ualimu visivyo vya serikali. Aidha, wako walimu 1,192 kutoka nje ya nchi wanaofundisha katika shule zisizo za serikali kwa kuzingatia taratibu zilizopo,”

Alisema kutokana na idadi kubwa ya walimu, kumekuwapo na changamoto zinazohitaji kuwa na mfumo dhabiti wa usimamizi wa ubora wa walimu na taaluma ya ualimu.

Alisema Kamishna wa Elimu atakuwa na jukumu la kusimamia taaluma na utaalamu wa ualimu kwa kusajili walimu wote, kutoa leseni ya kufundisha kwa waombaji wasiokuwa walimu na kufuta leseni ya mwalimu yeyote atakayekiuka maadili ya ualimu.

“Hata hivyo, uzoefu unaonyesha kuwa masuala ya taaluma na utaalamu wa ualimu yanaweza kusimamiwa kikamilifu na kwa ufanisi zaidi pale ambapo majukumu hayo yanafanywa na chombo mahususi chenye mamlaka huru ya kisheria.

TAARIFA YA KAMATI

Akiwasilisha maoni ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Kudumu ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii, Peter Serukamba alisema kamati inashauri kuwekwa ukomo wa madaraka ambayo kwenye muswada huo haionyeshi.

“Kamati pia inashauri kufutwa kwa kufutwa kwa kifungu cha 18 (1) (b), kinachotaka kuonyesha kuwa mtu yuko sawa na sahihi kufanya kazi ya ualimu, sifa hii kufahamaika kwake ni kwa mujibu wa vipimo vya daktari ndiye anaweza kuonyesha kama mtu huyo yuko timamu kufanya kazi ya ualimu.

“Ni ushauri wa kamati kifungu hicho kifutwe kwa kuwa kimeweka sifa ambazo haziwezi kubainika kwa macho wakati wa usajili ili mwalimu aweze kupata usajili wa bodi,” alisema.

MAONI YA KAMBI RASMI YA UPINZANI

Akiwasilisha maoni ya Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, Susan Lyimo, alisema kuanzishwa kwa bodi hiyo ni kuongeza idadi ya chombo kipya katika muundo wa Serikali ambapo ni wazi itahitajika bajeti ambayo haikuwapo yaani kutakuwa na ongezeko la matumizi ya serikali katika kukiendesha chombo hicho.

Alisema pendekezo la muswadawa sheria hiyo kuwakata tena ada ya cheti cha usajili kwenye bodi kila mwaka ni kuwafanya walimu waendelee kuwa duni kiuchumi lakini pia ni kuwavunja moyo na kuwaondolea morali ya kufundisha.

“Muswada huu umelenga kuwadhibiti walimu badala ya kuwaendeleza kwa kutilia mkazo kwenye kuwadhibiti na kuwaadhibu walimu pindi wanapokosea katika kutekeleza majukumu yao.

“Pia haujazungumzia namna ya kuwapa walimu ushauri nasaha pindi wanapokuwa na msongo wa mawazo au matatizo yanayoweza kuwasababishia kushuka kwa weledi wao lakini pia muswada huu umejaa orodha ndefu ya makatazo, makosa na adhabu kwa mwalimu atakayetenda kosa,” alisema.

Pamoja na mambo mengine, Mwenyekiti huo alisema wanaishauri serikali kupunguza utitiri wa vyombo na taasisi zinazoshughulikia masuala ya walimu na kubaki na chombo kimoja kwa ajili hiyo.

MAONI YA WABUNGE

Mbunge wa Viti Maalumu, Anatropia Theonest (Chadema), alisema maeneo mengi Waziri anateua watu wengi akiwamo Mwenyekiti wa Bodi na Wajumbe wanane wa bodi hiyo, wasimamizi au wasaidizi katika wilaya na mikoa.

“Hayo yote ni mawazo ya waziri kwa hiyo tunakwenda kuwa na bodi ambayo ni maoni ya waziri, ingependekeza kama ikioneakana inafaa watu wenye vigezo wajitokeze wagombee hizo nafasi ambapo katika washindani hao ndiyo waziri ateue mmojawapo, pia tuwaache walimu wenye uwezo wajitokeze kushika nafasi katika bodi hiyo kwa maana wao ndiyo wana maono ya namna ya kuendesha chombo chao,” alisema.

Aidha, akizungumzia kuhusun ada ya usajili wa leseni hizo alisema inatambulika walimu hawalipwi vizuri hivyo ada ipunguzwe au isiwepo kabisa ili mradi awe na vigezo vinavyokubalika ila kama inaendana kunazishwa kwa bodi hiyo kunaendana sambamba na ongezeko la mishahara.

Naye Serukamba akitoa maoni yake alisema “yako mambo hayako sawa, tunamtaka Waziri wa Elimu kuleta marekebisho ya muswada huu kwa kuweka kifungu ambacho kinampa mamlaka Rais kuteua Mwenyekiti wa Bodi kama inavyofanyika katika bodi nyingine za kitaaluma nchini, asiteue yeye.”

Mbunge wa Nzega Mjini, Hussein Bashe (CCM), alisema sekta ya elimu inahitaji mabadiliko kama uanzishwaji wa bodi hiyo lakini bodi hiyo pia inampa mamlaka waziri ambapo kwa muundo wa kiutawala anyesimamia uendeshaji wa waalimu ni Waziri wa Tamisemi lakini anayesimamia sera ni Waziri wa Elimu.

Aidha, alipendekeza Serikali kuipangia ruzuku bodi hiyo ili isitegemee ada na tozo zinazotokana na walimu katika uendeshaji wake.

“Mwenyekiti mimi nimeipitia sheria hii, napendekeza viwango vya ada vitakavyopangwa katika utekelezaji wa sheria hiyo viwango vya mishahara ya walimu nchini ambao wanafanya kazi katika mazingira magumu.

 

 

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here