31.7 C
Dar es Salaam
Thursday, March 28, 2024

Contact us: [email protected]

Museveni, JK wajadili mafuta ya Uganda

Museveni - 1NA MWANDISHI WETU

RAIS Jakaya Kikwete na mwenzake Yoweri Museveni wa nchini Uganda, wamekutana jijini New York, Marekani na kujadili mambo mbalimbali ikiwemo maendeleo ya uchimbaji wa mafuta yanayopatikana nchini Uganda.

Marais hao walikutana juzi katika Hoteli ya Trump International and Tower iliyopo jijini humo ambako viongozi hao wapo huko ili kuhudhuria shughuli za mwaka huu za Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa.

Taarifa iliyotolewa jana na Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais, Ikulu, ilisema mbali na hilo pia viongozi hao walizungumzia uhusiano kati ya nchi hizo mbili pamoja na masuala ya Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) ambako nchi hizo ni wanachama.

“Miongoni mwa mambo ambayo viongozi hao walizungumzia ni maendeleo ya uchimbaji mafuta nchini Uganda na faida za mafuta hayo kwa Tanzania na kwa nchi zote wanachama wa EAC, wakati mafuta hayo yatakapoanza kutumika,” ilisema taarifa hiyo.

“Rais Kikwete na Rais Museveni pia walipata nafasi ya kujadiliana kuhusu hali ya kisiasa Afrika na jinsi gani inavyoweza kuimarishwa katika baadhi ya nchi,” ilisema taarifa hiyo.

Katika mazungumzo hayo, Kikwete na Museveni walijadili pia hali ya kisiasa nchini Burundi ambako rais huyo wa Uganda ndiye aliyepewa jukumu na viongozi wenzake wa EAC kusimamia mazungumzo ya kuleta maelewano na maridhiano.

Burundi pia ni mwanachama wa EAC ambayo Mwenyekiti wake ni Rais Kikwete.
“Mbali na hilo, viongozi hao walijadili hali ya kisiasa na kiusalama ilivyo katika nchi jirani ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) na juhudi zinavyoweza kufanyika kusaidia kuboresha hali hiyo hasa kwa kutilia
maanani kuwa Tanzania inayo majeshi ya kulinda amani nchini humo,” ilisema taarifa hiyo.

Mazungumzo hayo yalihudhuriwa pia na Sam Kutesa ambaye ni Waziri wa Mambo ya Nje wa Uganda anayemaliza muda wake na Rais wa Baraza Kuu la Usalama la Umoja wa Mataifa pamoja na Tuvako Manongi ambaye ni Mwakilishi wa Kudumu wa Tanzania, Umoja wa Mataifa.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles