23.9 C
Dar es Salaam
Wednesday, April 24, 2024

Contact us: [email protected]

MUME, MKEWE WAFUNGWA MIAKA 55

Na Kulwa Mzee -Dar es Salaam

MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam imewahukumu kwenda jela miaka 55 mke na mume kwa kosa la kukutwa na meno ya tembo yenye thamani zaidi ya Sh bilioni 2.

Hukumu hiyo ilitolewa jana na Hakimu Mkazi Mkuu, Huruma Shahidi, baada ya kuwatia hatiani Peter Kabi na mkewe Leonidia Kabi mwishoni mwa wiki.

Washtakiwa walikutwa na meno ya tembo nyumbani kwao yakiwa ndani ya jeneza, huku wakijiandaa kulifunika kwa kutumia bendera ya Taifa kwa ajili ya kuyasafirisha kama mwili wa askari ili wasikaguliwe wakati wakielekea Tarakea mkoani Kilimanjaro.

Akisoma hukumu hiyo, Hakimu Shahidi alisema washtakiwa ni wakosaji wa mara ya kwanza, imethibitika jinsi gani walivyofanya uhalifu wa kuua tembo 93.

“Washtakiwa wameathiri uchumi kwa kiasi kikubwa, hakuna mtalii anayeweza kufika kuangalia mizoga, jambo hili halikubaliki.

“Hii nchi ni yetu, ninyi kama mke na mume mmeamua kula haya matunda ya edeni kinyume cha utaratibu na mimi nawaadhibu.

“Kwa kosa la kwanza, mtakwenda jela miaka isiyozidi 15, kosa la pili mtakwenda jela miaka isiyozidi 20 na kosa la tatu mtakwenda jela miaka isiyozidi 20, adhabu hizo zitakwenda kwa pamoja,”alisema.

Hakimu Shahidi, alisema hoja ya Wakili wa Serikali, Paul Kadushi kwamba mahakama itaifishe mali za washtakiwa ikiwemo nyumba, hakuna ushahidi wa umiliki wa nyumba hiyo.

Alisema kama wanahitaji kutaifisha nyumba hiyo, wawasilishe maombi yasikilizwe na kutolewa uamuzi.

Washtakiwa hao, walikuwa wanakabiliwa na mashtaka   matatu ya kuendesha biashara ya nyara za Serikali na kukutwa na nyara hizo kinyume na sheria.

Wanadaiwa  Oktoba 27, 2012 katika eneo la Kimara Stop Over, Dar es Salaam kwa pamoja, washtakiwa hao  walitenda vitendo vya uharifu kwa   kupanga, kukusanya na kuuza  vipande 210 vya meno ya tembo na vipande vitano vya mifupa ya tembo.

Alidai  vipande hivyo, vilikuwa na uzito wa kilogramu 450.6 zenye thamani ya Dola za Marekani 1,380,000 .

Kwa upande wa vipande vitano vya mifupa ya tembo,  vilikuwa na  thamani ya Dola za Marekani 30,000 na kwamba vyote jumla walikuwa tembo 93 wenye  thamani ya Dola za Marekani 1,410,000 ambayo ni sawa na Sh  2,206,611,000.

Akizungumza nje ya Mahakama Mkurugenzi wa Idara ya Wanyamapori, Alexander Songorwa alihamasisha kila Mtanzania kushiriki vita hiyo ili kulinda rasilimali zilipo.

Naye Mkurugenzi wa Mashtaka nchini(DPP), Biswalo Mganga alisema tembo waliouawa walikuwa na thamani ya Sh 2,206,611,000, kutokana na uamuzi wa mahakama wanatarajia kuwasilisha maombi kwa ajili ya kufilisi nyumba ambayo washtakiwa walikuwa wamehifadhia meno ya tembo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles