23.3 C
Dar es Salaam
Saturday, April 20, 2024

Contact us: [email protected]

MUGABE KING’ANG’ANIZI AISEE!

  • Aibuka hadharani bila mke, Jeshi lampa ulinzi kama Rais

HARARE, ZIMBABWE

RAIS wa Zimbabwe, Robert Mugabe, kwa mara ya kwanza jana alionekana hadharani tangu Jenerali Constantine Chiwenga alipoliongoza Jeshi la nchi hiyo kuchukua madaraka Jumatano wiki hii.

Mugabe ambaye nyumba yake imezungukwa na jeshi la nchi hiyo kwa siku nne sasa, jana alitoka akiwa na ulinzi ule ule anaotakiwa kuwa nao Rais na kisha kuhudhuria mahafali ya Chuo Kikuu Huria cha nchini humo (ZOU) yaliyofanyika mjini Harare.

Jambo ambalo ni la tofauti na pengine limeibua minong’ono, ni kitendo cha Mugabe kuonekana pasipokuwa na mkewe, Grace ambaye anaelezwa kuwa msingi wa mzozo wa kimamlaka unaoshuhudiwa sasa nchini Zimbabwe.

Haijajulikana mara moja mahali alipo Grace kwa sasa, lakini kitendo cha kutoonekana pembeni ya Mugabe kimeibua hisia kwamba huenda ikawa kweli amekimbilia nchini Namibia ama Jeshi la nchi hiyo linamshikilia au limemzuia.

Pamoja na kwamba Mugabe kuhudhuria mahafali hayo ni utamaduni wake wa kila mwaka kwa nafasi yake ya urais kama Mkuu wa Chuo hicho, lakini wengi hawakutarajia kumwona kutokana na mzozo huo.

Si hilo tu kitendo cha Jeshi ambalo linaonekana kutaka kukatisha madaraka ya Mugabe jana kuendelea kumpa heshima ile ile kama Rais na hata kumwita ‘Mheshimiwa Rais ama Amiri Jeshi Mkuu, kimezidi kuibua utata kuhusu hatima ya ama kuondoka au kuendelea kusalia madarakani.

Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC), jana lilinukuu Jeshi la nchi hiyo likisema kuwa mazungumzo na Rais Mugabe yanaendelea hivyo kuwaomba wananchi kuwa watulivu kwa kuwa watafahamishwa kinachoendelea haraka iwezekanavyo.

Wakati Jeshi likitoa taarifa hiyo, kitendo cha Mugabe kutokea kwenye mahafali hayo huku akitembea kwa mwendo wa pole pole katika zuria jekundu kiliibua shangwe na nderemo.

Gazeti la NewsDay, liliandika kuwa Mugabe alishangiliwa na mamia ya watu waliohudhuria mahafali hayo mara baada ya kumaliza kuzungumza, ambapo alijumuika nao kuimba wimbo wa taifa.

Gazeti maarufu la mtandaoni la Daily Mail, la nchini Uingereza, liliripoti kuwa akiwa katika mahafali hayo kuna wakati Mugabe alionekana kusinzia kiasi cha kuyumba yumba kichwa.

Gazeti hilo liliweka katika mtandao wake kipande kidogo cha video kinachomwonyesha Mugabe mwenye umri wa miaka 93 akiwa amevalia joho na kofia ya mahafali, huku macho yake akiwa ameyafumba na kichwa chake kikiwa kinayumba yumba mithili ya mtu anayesinzia.

Mbali na Grace, katika hali nyingine ya kushangaza kwenye mahafali hayo Mugabe hakuambatana na Waziri wa Elimu ya Juu, Jonathan Moyo, kama ilivyo desturi.

Itakumbukwa Moyo alikamatwa na wanajeshi wa nchi hiyo siku ya kwanza walipozingira makazi ya Rais Mugabe, Ikulu na kudhibiti Serikali.

Pamoja na kwamba Moyo hakuwepo, nafasi yake katika sherehe hizo ilikaliwa na Naibu wake, Godwin Gandawa na vyombo vya habari vya kitaifa na vile vya kimataifa vinavyofuatilia mzozo huo vimeripoti kuwa hapakuwa na maelezo yoyote ya ziada.

Miongoni mwa waliotunukiwa shahada katika mahafali hayo ni Marry Chiwenga, mke wa Mkuu wa Majeshi wa nchi hiyo, Jenerali Chiwenga, aliyewaongoza majeshi kudhibiti nchi hiyo.

Jeshi la Zimbabwe lililazimika kuingilia kati mara baada ya Mugabe kumfukuza kazi Makamu wake, Emmerson Mnangagwa wiki iliyopita.

Taarifa zinasema kuwa Mnangagwa amekuwa akitazamwa kama mrithi wa kiti cha urais, hivyo kufukuzwa kwake kulitengeneza njia rahisi kwa Grace Mugabe kukabidhiwa madaraka hayo makubwa Zimbabwe.

 UTATA ZAIDI

Mhariri wa habari za Afrika wa BBC, Mary Harper, amesema kujitokeza kwa Mugabe katika mahafali hayo kumeweka taswira ya kana kwamba mambo yamekuwa ya kawaida, lakini hali halisi ni tofauti.

Ameeleza kuwa hatua hiyo imeongeza utata kuhusiana na hali ya baadaye ya rais huyo aliyetawala Zimbabwe kwa miaka 37.

Jeshi limedhibiti nchi kwa muda wa siku nne na kwa msaada wa wapatanishi kutoka Afrika Kusini wanashiriki mazungumzo na Mugabe.

Kiongozi huyo mwenye uzoefu wa mapambano amepinga shinikizo la kuondoka madarakani haraka, lakini anakabiliwa na sintofahamu ya kuachia ngazi baada ya miongo minne ya kukaa madarakani.

AMLILIA MKEWE WA ZAMANI

Taarifa ya mtandao wa PaZimbabwe, zinaeleza kuwa tangu Jeshi kudhibiti nchi hiyo, vyanzo vya ndani vilivyoko karibu na Mugabe vimesema kiongozi huyo amekiri kifo cha mkewe wa zamani, Sally Sarah Hayfron, kilichotokea mwaka 1992 kimemwachia pengo kubwa na alimkumbuka mara baada ya tukio hilo.

“Alituambia kwamba, Sally Sarah Hayfron, alikuwa mpenzi wa maisha yake yote,” chanzo cha habari kimeeleza.

Mugabe alioana na mkewe wa kwanza mwaka 1961 na kupata mtoto mmoja, Michael Nhamodzenyika “Nhamo”, lakini alifariki baadaye mwaka 1966 kwa ugonjwa wa malaria katika kipindi ambacho Mugabe mwenyewe alikuwa jela.

KAULI YA JESHI

Kwa mujibu wa gazeti la Serikali la The Herald, kwenye mtandao wake likikariri taarifa ya Jeshi la nchi hiyo (ZDF) kuwapo mazungumzo mazuri baina ya pande zote mbili.

ZDF limesisitiza kukamilika kwa asilimia kubwa operesheni yake ya kukabiliana na wahalifu waliomzunguka Rais Mugabe kwa lengo la kuleta utulivu na haki kwa ujumla.

Hata hivyo, jeshi hilo halijataja majina ya wahalifu waliokamatwa licha ya kuwashikilia baadhi ya mawaziri wa Serikali ya Mugabe.

“Tunaheshimu hisia za kila mtu na makundi yaliyopo katika jamii zetu nchini, tunapenda kuthibitisha kwamba hakuna mtu aliyeruhusiwa kuzungumza kwa niaba yetu (ZDF).

“Tutakuwa tunatoa taarifa kwa umma ili kueleza hatua zilizofikiwa ndani ya nchi yetu. Jeshi linawaomba wananchi kuwa watulivu kama walivyofanya na wawe na subira hadi tukapokamilisha operesheni hii.”

AMEKATAA KUJIUZULU?

Uvumi umeenea nchini Zimbabwe huku baadhi ya watu wakisema kitendo cha Rais Mugabe kuonekana hadharani kwenye mahafali ya Chuo Kikuu Huria (ZOU) cha Zimbabwe, ni ishara ya kukataa kuachia ngazi kwa matakwa ya Jeshi la nchi hiyo pamoja na mazungumzo yake na majenerali wa nchi hiyo.

Wanasema taarifa ya Jeshi hilo iliyotolewa juzi na Jenerali Chiwenga kwa vyombo vya habari, inamtaja Mugabe kama Rais na Amiri Jeshi Mkuu, inadhihirisha kuwa kiongozi huyo bado yuko madarakani.

Awali, Rais wa Afrika Kusini, Jacob Zuma, aliliambia Bunge la nchi yake mjini Cape Town, kwamba ni mapema mno kuchukua uamuzi thabiti kutokana na hali ya kisiasa iliyopo, ambayo muda si mrefu itajulikana wazi.

VIONGOZI WATOA KAULI

Rais wa Botswana, Ian Khama, aliliambia Shirika la Habari la Reuters  viongozi wa kikanda wa Kusini mwa Afrika kuwa hawamuungi mkono Mugabe kubaki madarakani.

“Sisi marais, hatutokani na utawala wa kifalme,” alisema Khama.

Rais wa Nigeria, Muhammadu Buhari, amewaomba wananchi wa Zimbabwe kuwa watulivu na kusisitiza kuwa Katiba lazima iheshimiwe.

Kwa upande wao Umoja wa Afrika umesema utairuhusu Jumuiya ya Maendeleo ya Mataifa Kusini mwa Afrika (SADC), kuwa mpatanishi katika mzozo huo.

Kamishna wa amani na usalama wa Umoja wa Afrika, Smail Chergui, amesema umoja huo una matumaini kwamba hatua ya Jeshi la Zimbabwe kuchukua madaraka si ya mapinduzi.

Inaonyesha kuwa kuna juhudi za kufuata sheria, badala ya kuwapo mapinduzi.

Amesema wajumbe wa SADC wamefanikiwa kukutana na Rais Mugabe na kwamba Afrika ina imani na juhudi zao.

Naye Rais wa Umoja wa Afrika, Alpha Conde, amesema umoja huo hautaruhusu mapinduzi ya kijeshi nchini Zimbabwe.

Ameviambia vyombo vya habari nchini mwake kuwa ni muhimu kurejeshwa utawala unaotambuliwa na Katiba Zimbabwe.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Guterres, ametoa wito wa kupatikana suluhu kwa njia ya amani.

Msemaji wa Guterres, Stephane Dujarric, amesema umoja huo una wasiwasi na kwamba hautaki kuona nchi hiyo inakosa utulivu.

WAHUSIKA WA MAZUNGUMZO

Katika mazungumzo ya kutafuta mwafaka wa hali ya kisiasa nchini humo, kwa mujibu wa gazeti la Serikali la The Herald ni Mugabe, Majenerali wa Jeshi la Zimbabwe wakiongozwa na Jenerali Chiwenga pamoja na Waziri wa Ulinzi wa Zimbabwe, Sydney Sekeramayi,  Waziri wa Usalama na Ujasusi, Kembo Mohadi, Askofu wa Kanisa Katoliki na rafiki mkubwa wa Mugabe,  Fidelis Mukonori.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles