26.2 C
Dar es Salaam
Friday, March 29, 2024

Contact us: [email protected]

MUGABE ALITUNISHIA JESHI MSULI

WAANDISHI WETU NA MASHIRIKA 

WAKATI Jeshi nchini Zimbabwe likiingia siku ya tatu ya kushika madaraka ya nchi, Rais Robert Mugabe na mkewe Grace, wanadaiwa kuendelea kuwekwa kizuizini nyumbani kwao baada ya kiongozi huyo mkongwe zaidi Afrika kukataa kung’atuka.

Vyombo mbalimbali vya habari vya kimataifa jana viliripoti kuwa, Rais Mugabe, amesisitiza kutaka kumaliza muhula wake wa urais ndipo atoke madarakani.

Kwa mujibu wa mtandao wa Times Live wa Afrika Kusini, Mugabe anasisitizia kuwa yeye bado ni rais wa Zimbabwe na apewe nafasi ya kumaliza muhula wake.

Kwa kiasi kikubwa mazungumzo ya sasa yanaendeshwa na ujumbe wa Jumuiya ya Nchi za Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (SADC) huku hasimu mkubwa wa kiasiasa wa Rais Mugabe, Morgan Tsvangirai, jana akisema lazima mkongwe huyo wa siasa ajiuzulu ili taifa hilo libaki salama.

Mbali na SADC, Kanisa la Katoliki nchini Afrika Kusini, linatajwa kuwa mtu muhimu na wa karibu zaidi na Rais Mugabe, ambaye amekuwa akitumiwa na jeshi kama mtu wa kati ya Rais Mugabe na jeshi la nchi hiyo.

Wakati hayo yakiendelea, baadhi ya wachambuzi wameilaumu China kuwa ipo nyuma ya mapinduzi hayo yanaelezwa kuwa ya kisasa zaidi kuwahi kutokea, ikilinganishwa na mengine yanayoambatana na umwagaji damu.

Hata hivyo, China imeridhia kufanyika mapinduzi hayo ikipendelea uwapo wa serikali ya mpito itakayoshirikisha wapinzani.

Mugabe (93) amebakia kujichimbia katika makazi yake hayo yenye thamani ya pauni milioni 7.5 sawa na Sh bilioni 32 yanayojulikana kama ‘Blue Roof’ katika mji mkuu wa Harare.

Awali kulikuwa na sintofahamu kuhusu mahali alipo mkewe, ‘Gucci’ Grace Mugabe (52), baada ya mamlaka za Namibia kusisitiza hakuna ukweli wa madai kuwa amekimbilia nchini humo.

Lakini jana asubuhi, vyanzo vya habari vilisema kwamba wenzi hao pamoja na vigogo wawili muhimu wa mtandao wa kisiasa wa Grace Mugabe, Generation 40 wapo pamoja kizuizini katika makazi hayo.

Vigogo hao wa G40 ni pamoja na Jonathan Moyo na Saviour Kasukuwere, ambao walikimbilia hapo baada ya nyumba zao kushambuliwa usiku wa Jumanne.

 KASISI ASIMAMIA MAZUNGUMZO

 Miongoni mwa wanaohusika na majadiliano baina ya Mugabe na majenerali wa jeshi walioidhibiti nchi kwa kile walichosema kuwalenga wahalifu waliomzunguka Rais Mugabe, ameelezwa kuwa ni Padri wa Kanisa Katoliki ambaye ana urafiki wa karibu na familia ya Mugabe.

Kasisi Fidelis Mukonori amekuwa rafiki wa rais huyo tangu miaka ya 1970, kwa mujibu gazeti la Serikali la Herald na anachukuliwa kama ‘kiongozi wa kiroho’ wa Mugabe.

Bado haijafamika kuhusu mazungumzo hayo yanayonekana kulenga kufanya makabidhiano ya madaraka bila umwagaji wa damu baada ya kuondoka kwa Rais Mugabe ambaye ameiongoza Zimbabwe tangu ilipopata uhuru mwaka 1980.

Rais Mugabe, bado anaonwa na Waafrika wengi kama shujaa wa ukombozi lakini anachukuliwa na mataifa ya Magharibi kama dikteta aliyeubomoa uchumi wa taifa lake na ambaye yuko tayari kutumia mabavu kujibakisha madarakani.

 MNANGAGWA URAIS SASA AU KUSUBIRI

Majadiliano yanayoendelea yanalenga kuwezesha Rais Mugabe kujiuzulu mara moja au miezi michache ijayo na kutoa fursa kwa aliyekuwa mshirika na makamu wake wa rais Emmerson ‘Mamba’ Mnangagwa.

Hiyo inamaana iwapo Rais Mugabe atakubali kujiuzulu sasa, itaundwa serikali ya mpito itakayoongozwa na Mnangwagwa na iwapo hilo litashindikana na Rais Mugabe kupewa ruhusa ya kumalizia muhula wake kama anavyosisitiza, Mnangagwa atawania urais kupitia ZANU-PF katika uchaguzi mkuu ujao.

Iwapo suala la serikali ya mpito litapita inatarajia kuwahusisha wapinzani akiwamo kiongozi wa upinzani, Morgan Tsvangirai anayetibiwa  katika nchi za Uingereza na Afrika.

Waziri Mkuu huyo wa zamani wa Zimbabwe ameripotiwa kurejea Harare juzi, siku ambayo Mnangwagwa pia alitokea Afrika Kusini, Taarifa za kidemokrasia kutoka nchini Zimbabwe zinaeleza kuwa jeshi lina uwezo mkubwa wa kufanya kadiri linavyotaka, lakini bado linamheshimu Mugabe. Kwamba halitaki kumdhalilisha kwa kumngo’a kwa fedheha bali linasaka njia ang’atuke kwa heshima.’

Pamoja na Mugabe kuhesabika bado shujaa katika nyonyo za wengi, hali hiyo haiko kwa mkewe Grace, katibu wake muhtasi wa zamani, ambaye alianza uhusiano na Mugabe mapema miaka ya 1990 wakati mkewe Sally akipigania uhai kutokana na maradhi ya figo.

Akifahamika kama “Gucci Grace” kutokana na sifa yake ya kufanya manunuzi ya kutisha huku Wazimbabwe wengi wakiwa hoi kiuchumi, Grace alipanda haraka katika kilele cha madaraka ndani ya chama cha ZANU-PF miaka miwili iliyopita na kusababisha kufukuzwa kwa Mnangagwa, hatua inayotajwa kumsafishia njia ya kumrithi mumewe. 

MSHIRIKA WA MUGABE AOMBA RADHI

 Wakati hilo likitokea, Kiongozi wa Kitengo cha Vijana cha chama tawala cha Zanu-PF, Kudzai Chipanga, ambaye amekuwa akimuunga mkono Rais Mugabe na mkewe Grace ameomba radhi kutokana na hatua yake ya kulishutumu na kulionya jeshi dhidi ya kuchukua madaraka nchini humo.

Jumanne, alikuwa amemwambia Mkuu wa Majeshi, Jenerali Constantino Chiwenga kuwa anapaswa kusalia kwenye kambi za jeshi.

Alikaririwa akieleza wanachama wake hawatakubali wanajeshi wakiuke Katiba na kwamba yeye na wafuasi wake walikuwa tayari kufa wakimtetea Rais Mugabe.

Lakini usiku wa kuamkia jana, alisoma taarifa kwenye runinga ya taifa (ZBC), akisema kwamba alikuwa amekosea.

“Tangu wakati huo nimetafakari na kutambua binafsi kwamba nilikosea, pamoja na wakuu wenzangu kwa kudunisha ofisi yako yenye heshima.

“Sisi bado ni wadogo na hufanya makosa na tumejifunza mengi kutokana na makosa haya,” alisema.

AFRIKA KUSINI YAINGILIA KATI

Mwenyekiti wa Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika (SADC), Rais wa Afrika Kusini Jacob Zuma, amemtuma Waziri wa Ulinzi, Nosiviwe Mapisa-Nqakula na Waziri wa Usalama Bongani Bongo kusaidia majadiliano yanayoendelea baina ya Mugabe na majenerali, taarifa zinasema.

Mawaziri hao wameshawasili kwenye mji mkuu wa Zimbabwe, Harare juzi usiku tayari kwa mazungumzo hayo ya dharura.

Aidha, viongozi wa nchi wanachama wa SADC wamekutana mjini Gaborone, Botswana kujadili hali inayoendelea nchini Zimbabwe.

CHINA YADAIWA INA MKONO

Wakati hayo yakijiri, kuna minongono imeenea jana kuwa wakuu wa jeshi waliiomba China kubariki mapinduzi hayo kabla ya hatua hiyo.

Awali Wizara ya Mambo ya Nje ya China ilisema kwamba ziara ya Beijing wiki iliyopita iliyofanywa na Mkuu wa Majeshi Jenerali Constantino Chiwenga, ambaye anaonekana kuchukua udhibiti wa Zimbabwe, ilikuwa ya kawaida kijeshi.

Lakini wafuatiliaji wa mambo wanaamini huenda China imetoa baraka zake kwa Chiwenga kufanya mapinduzi hayo, gazeti la Daily Telegraph limeripoti jana.

Alipoulizwa iwapo Chiwenga aliwaarifu maofisa wa China kuhusu mpango wowote wa kuitwaa Zimbabwe kijeshi, msemaji wa serikali ya China Geng Shuang aliwaambia wanahabari kuwa Wizara ya Ulinzi iliandaa safari na haikufahamu lolote kuhusu mpango huo.

“Ninachoweza kukuambia ni kwamba ziara yake ilikuwa ya kawaida ya kijeshi kama zilivyokubaliana nchi mbili,” alisema Geng.

Novemba 10, mwaka huu katika blogu yake, Wizara ya Ulinzi ilimuonyesha Chiwenga akitabasamu na kushikana mikono na Waziri wa Ulinzi wa China, Chang Wanquan wizarani mjini Beijing.

Picha nyingine iliwaonyesha wawili hao wakiwa wamekaa na ujumbe wao katika meza za mkutano.

China imekuwa muungaji mkono wa Rais Mugabe licha ya shutuma dhidi yake kutoka jumuiya ya kimataifa kuhusu utawala wake wa kiimla na ukiukaji wa haki za binadamu.

Uhusiano wa kijeshi baina ya pande hizo mbili unarudi nyuma wakati China iliposaidia harakati za kijeshi za Zimbabwe dhidi ya utawala kandamizi wa wazungu wachache katika miaka ya 1970.

Mugabe na familia yake wana uhusiano wa karibu na China hasa utawala wa Hong Kong, ambako walihusika na kesi ya madai kuhusu miliki ya kifahari huku binti yao Bona Mugabe akiwa amesoma chuo kikuu hapo.

WAZIRI AKAMATWA AKITOROKEA AFRIKA KUSINI 

Mbunge ambaye pia ni Waziri wa Serikali, Paul Chimedza amekamatwa katika kizuizi cha barabarani akijaribu kukimbia kwenda Afrika Kusini.

Taarifa zilizoripotiwa na baadhi ya vyombo vya habari vya Zimbabwe jana zilieleza kuwa Chimedza, ambaye ni Waziri wa Serikali ya Mkoa wa Masvingo alimatwa eneo la Bubi kusini mwa Zimbabwe.

HARARE TULIVU

Tofauti na harakati zinazoendelea nyuma ya pazia kumshawishi Rais Mugabe kuondoka kwa amani na kuhakikisha kunapatikana uongozi mpya wa mpito, katika Jiji la Harare hali ni tulivu na raia wanaendelea na shughuli zao za kawaida.

Maeneo ambayo watu wamezuiwa kuingia ni mitaa inayozunguka majengo muhimu ya serikali huku vizuizi katika barabara kuu kwa sasa vikisimamiwa na askari polisi wenye silaha badala ya wanajeshi.

Jeshi limekuwa likikwepa kueleza utwaaji huu madaraka badala yake wameeleza ni usahihishaji wa demokrasia.

Juzi Umoja wa Afrika (AU) ilitoa taarifa ikisema kuwa kinachoendelea Zimbabwe kinaonekana kama mapinduzi na ilitoa mwito kwa jeshi kujiondoa na kuheshimu Katiba.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles