25.2 C
Dar es Salaam
Tuesday, April 23, 2024

Contact us: [email protected]

Mufti: Nchi inaelekea pabaya

Mufti Issa Shaaban Simba
Mufti Issa Shaaban Simba

NA WAANDISHI WETU, DAR ES SALAAM

SHEIKH Mkuu wa Tanzania, Mufti Issa Bin Shaaban Simba, amesema taifa linaelekea pabaya kutokana na kushamiri kwa vitendo vya ulipuaji wa mabomu vinavyofanywa na watu kwa nia ya kulipiza visasi.

Alisema kutokana na hali hiyo, vitendo hivyo vinaonyesha wazi vina lengo la kuchochea uhasama kwa viongozi wa dini na waumini wao ili kuvuruga amani ya nchi.

Mufti Simba aliyasema hayo jijini Dar es Salaam jana wakati akizungumza na MTANZANIA katika mahojiano maalumu.

Alisema matukio hayo yameendelea kutokea kwa sababu ya vyombo vya dola kutokuwa na ufuatiliaji wa kutosha.

“Taifa linaelekea pabaya, kinachosikitisha zaidi ni kwamba, vyombo vya dola ambavyo vimepewa dhamana ya kusimamia vimeshindwa kufuatilia pindi matukio haya yanapotokea.

“Kitendo hiki kimesababisha wanaofanya vitendo hivi kujaa kiburi kwa sababu kinawapa jeuri ya kuendelea kutimiza azma zao.

“Siwezi kutabiri moja kwa moja kuwa vitendo vya ulipuaji wa mabomu vinavyoendelea kutokea nchini vinahusiana na masuala ya kisiasa au la, isipokuwa hali ninayoiona ni mpango wa watu wachache wa kuvuruga amani ya viongozi wa dini na nchi kwa ujumla,” alisema Mufti Simba.

Alisema kama watu hawa wangekuwa wanakamatwa na kuchukuliwa hatua zinazostahili, matukio ya aina hii yangepungua.

Alisema ni jambo la kusikitisha kuona mambo ya dunia yanageuzwa kama sehemu ya kulipiza kisasi dhidi ya watu wasiokuwa na hatia.

Alisema ipo siku watu wanaofanya unyama huo Mungu atawaumbua tu.

“Sisi viongozi wa dini hatupendi vitendo hivi viendelee kutokea kwenye jamii yetu, kwani tunaumia mno kuona taifa linachafuliwa na watu wachache wenye chuki za malipizi kwa watu wasiokuwa na hatia.

“Lakini hata kama ni kulipa visasi, basi isiwe kurushiana mabomu na kujeruhi, kwani viongozi wa dini hawana uhasama wowote na hawahusiki na mambo ya siasa, kwa hiyo wanachotakiwa ni kutubu na kumrudia muumba wao katika kipindi hiki cha Mwezi Mtukufu wa Ramadhani.

“Naomba vyombo vya dola vifanye kazi zake kwa umahiri na kuhakikisha vinawakamata wahusika wote na kuwatia nguvuni ili kukomesha matukio ya aina hii,” alisema Mufti Simba.

DK. SLAA

Naye Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Dk. Wilbrod Slaa, amelitaka Jeshi la Polisi kuwafikisha mahakamani viongozi wa chama hicho waliodai wana ushahidi wa mtu aliyelipua bomu kwenye mkutano wao mkoani Arusha.

Itakumbukwa tukio hilo lilitokea   kwenye Uwanja wa Soweto Arusha Juni 16, mwaka jana na kujeruhi watu kadhaa.

Kauli ya Slaa imekuja siku moja baada ya Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI), Yesaya Ngullu, kudai kuwa viongozi hao hawana ushahidi wa mtu aliyerusha bomu kwenye mkutano huo.

Alisema baada ya kutokea kwa tukio hilo, aliwaita viongozi hao na kuzungumza nao kuhusu suala hilo, lakini mpaka sasa hakuna hata kiongozi mmoja aliyetoa ushahidi.

Akizungumza na MTANZANIA mjini Dar es Salaam jana, Dk. Slaa alisema  polisi wanajua sheria na taratibu kwa mtu anayetoa ushahidi wa uongo hadharani, baada ya kuwaona wamesema hivyo walipaswa kuwafikisha mahakamani ili wachukuliwe hatua za kisheria.

“Kama wanajua tumesema uongo kwanini wasitupeleke mahakamani ili tuchukuliwe hatua za kisheria, mbona walishindwa kuchukua taarifa zetu zozote badala yake wakaamua kumwita  mwenyekiti wetu, Freeman Mbowe akajieleza,” alisema Dk. Slaa.

MBATIA

Kwa upande wake, Mbunge wa kuteuliwa, James Mbatia ameitaka Serikali kuacha kulala usingizi wa pono katika kushughulikia matukio ya mabomu yanayoendelea kugharimu maisha ya Watanzania.

Ameitaka Serikali na vyombo vyake vya dola kuingia kazini kwa kuhakikisha usalama unarejea kwani damu za majeruhi katika milipuko ya mabomu hayo zina athari kubwa kwa taifa katika siku zijazo.

Akizungumza jijini hapa jana, Mbatia aliyejitambulisha kuwa ni mtaalamu wa majanga, alisema mtu mwenye jukumu la kwanza kuhakikisha anawalinda raia wa nchi ni yule aliyeapa kulinda Watanzania na mipaka yake.

“Nimetembelea eneo la tukio hali inasikitisha kabisa, yaani mwenye mgahawa hajui lolote yupo yupo analalamika,” alisema Mbatia na kuongeza:

“Hatuhitaji Serikali ambayo itakuwa inaweka maisha yetu rehani, Serikali makini lazima ijue kesho kutatokea kitu gani sio bomu linalipuka wewe umelala au unaenda kwenye kikao cha barabara.”

Alisema Serikali yoyote duniani kipaumbele chake cha kwanza huwa ni ulinzi na usalama wa wananchi wake na sio barabara.

MAJERUHI

Hadi kufikia jana majeruhi sita wa mlipuko huo wa bomu waliokuwa wamelazwa katika Hospitali ya Selian jijini Arusha walisafirishwa kuelekea jijini Nairobi kwa ajili ya matibabu zaidi.

Taarifa kutoka kwa jamaa za majeruhi zilibainisha kwamba, majeruhi hao waliondolewa hospitalini hapo jana jioni kwa gari la kubebea wagonjwa huku majeruhi wawili wakiendelea kupatiwa matibabu.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Tiba na Kaimu Mganga Mkuu wa Hospitali ya Selian, Dk. Paul Kisanga, alithibitisha kupewa ruhusu kwa wagonjwa hao sita huku akibainisha kuwa majeruhi aliyekatwa mguu bado anaendelea na matibabu hospitalini hapo.

“Majeruhi sita wamepewa ruhusa ila mpaka sasa tunao majeruhi wawili Deepack Gupta (25) na Prateek Jaley ndio wanaoendelea na matibabu.”

Taarifa hii imeandaliwa na Oliver Oswald, Patricia Kimelemeta, Grace Shitundu na Eliya Mbonea (Arusha).

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles