29.2 C
Dar es Salaam
Wednesday, April 24, 2024

Contact us: [email protected]

‘Mtu wa mkono’ yaamsha mjadala uimara wa upinzani

KINARA mwingine wa upinzani ambaye ameamua kuweka ‘silaha’ chini na kufanya kazi na Rais Uhuru Kenyatta ni kiongozi wa Chama cha Wiper ambacho ni moja ya vyama vinavyounda Muungano wa NASA, Kalonzo Musyoka.

Hii ni kumaanisha Rais Uhuru sasa anafanya kazi pamoja na aliyekuwa mpinzani wake katika uchaguzi uliopita, Raila Odinga na mgombea mwenza wake Kalonzo kwa lengo la kuinua uchumi wa Kenya na kudumisha amani.

Kauli ya Kalonzo kwamba atakuwa ‘mtu wa mkono’ wa Rais Uhuru aliyoitoa wakati wa mazishi ya baba yake, Mzee Musyoka Mairu hivi karibuni, imepokewa kwa hisia tofauti. Wapo wale wanaona Kalonzo anahitaji kufuata nyayo za Raila na kukubali kufanya kazi na Rais Uhuru.

Kuna kundi lingine linalopinga kwa madai panahitajika moja wa vinara wa upinzani kuwa upande wa pili kuhakikisha wanaipiga darubini na kuikosoa Serikali ya Rais Uhuru pale inapoteleza. Swali sasa linabaki, Je, upinzani bado upo Kenya? Na kama upo, nani mwenye ushawishi wa kuikosoa serikali?

Kalonzo ambaye ameshawahi kuwa Makamu wa Rais na mara mbili mgombea mwenza wa urais, alikuwa anatajwa kama mtu sahihi wa kuvaa viatu vya Raila kuelekea Uchaguzi Mkuu 2022. Aidha wengi walitarajia kiongozi huyo wa Wiper angechukua majukumu ya kinara wa upinzani na kuisuka upya kambi  hiyo baada ya ushirikiano wa Raila na Uhuru kusababisha kinara wa ODM kuteuliwa Balozi wa Umoja wa Afrika anayeshughulikia miundombinu msingi.

Hata hivyo, Kalonzo aliamua naye kuunga mkono juhudi za Rais Uhuru kuleta maendeleo pale alipoongoza wabunge wa chama chake kwenda Ikulu jijini Nairobi. Hivi karibuni aliweka wazi atakuwa ‘mtu wa mkono’ wa Rais Uhuru na tayari ameteuliwa Balozi Maalumu wa Rais atakayesimamia amani ya Sudan Kusini. Kalonzo anachukua nafasi ya aliyekuwa Rais wa Botswana, Festus Mogae.

Uamuzi wa kufanya kazi na Rais Uhuru pia umeshuhudia Kalonzo akirudishiwa walinzi wake ambao Serikali iliwaondoa kufuatia kitendo cha Raila Januari mwaka huu kujiapisha Rais wa wananchi.

Moja wa wanasiasa aliyekerwa na kauli ya Kalonzo ni Seneta wa zamani wa Machakos, Johnson Muthama, aliyesema jamii wa Wakamba wataacha kumuunga mkono Kalonzo na badala yake kuwasapoti wapinzani wake endapo Makamu Rais huyo wa zamani hataonesha nia ya dhati ya kuutaka urais 2022.

“Kalonzo anahitaji kuwaambia viongozi wa Wiper na wafuasi wake nini alichomaanisha na kauli yake ya kazi ya ‘mtu wa mkono’ wakati wa mazishi ya baba yake. Sisi tunamsukuma (Kalonzo) aende mbele na yeye anarudi nyuma. Tunaweza tukamuacha na kuunga mkono wapinzani wake,” alihoji Muthama.

Kama ilivyo kwa Muthama, naye Mwenyekiti wa Wiper ambaye pia ni Gavana wa Makueni, Kivutha Kibwana, alishangazwa na kauli ya Kalonzo na kusisitiza hakufikiria kabla ya kuitamka.

“Wakati kiongozi wa watu anakuwa mtu wa mkono, Je, wafuasi wake wamuelewe vipi? Na kweli anayo nia ya dhati kugombea tena urais 2022? alisema Kibwana.

Alisisitiza wafuasi wa Wiper hawana tatizo na kiongozi wao kuungana na kufanya kazi na serikali kwani ni jambo ambalo wamekuwa wakimshawishi lakini hawaungi mkono kauli yake ya kuwa ‘mtu wa mkono’ wa Rais Uhuru.

Kibwana alisema wafuasi wa Kalonzo wanahisi kama wamesalitiwa na ishara kwamba amesalimu amri kutimiza nia yake ya kugombea urais. Alidokeza kwamba yeye na viongozi wengine wa Wiper siku zote wamekuwa wakiunga mkono uamuzi unaotolewa na Kalonzo ikiwamo ule wa mwaka 2017 alipoamua waungane na NASA licha ya chama kumshauri kufanya kazi na Jubilee.

“Kusema ukweli tulitaka awe ndani ya serikali, afanye kazi na Uhuru na Naibu wake William Ruto. Lakini sasa hatuwezi kufuata uamuzi kwamba atakuwa ‘mtu wa mkono’ wa Uhuru,” alisema gavana huyo wa Makueni.

Wakati Mwenyekiti wa Wiper akimshangaa Kalonzo, Katibu Mkuu wa chama hicho, Judith Sijeny, alikiri kuwapo na mazungumzo kabla kinara wa chama chao kuruhusiwa kukubali majukumu mapya.

Sijeny anasisitiza Makamu Rais huyo wa zamani alipata baraka zote za chama na kusema viongozi wanaompinga wamekurupuka na anashindwa kujua kwanini ghafla wameingiwa na hofu.

Kalonzo hahitaji kusubiri hadi 2022 kugombea urais na kwa mujibu wa Mbunge wa Kathiani, Robert Mbui, ni bora ahusishwe kufanya kitu kwa ajili ya taifa kwa sababu alishawahi kuwa Makamu wa Rais na yeye ni miongoni mwa wanasiasa wanaopenda kuhubiri amani.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles