30.2 C
Dar es Salaam
Saturday, April 20, 2024

Contact us: [email protected]

Mtendee hivi mpenzi ambaye haonyeshi kukujali, kukuthamini

AMANI katika uhusiano ni hitaji la kila mmoja. Kila mtu akiwa na mtu ampendaye, kumjali na kumpa kipaumbele ni kitu cha kawaida katika maisha yake. Ila vipi ukiwa na mtu unayempenda sana ila yeye haonyeshi kukujali na kukuthamini? Mtu wa aina hii, unahitajika pia kuendelea kumwonyesha kumjali na kumpa hadhi kamili katika mahusiano yako?

Kama uko na mtu ambaye haonyeshi thamani na hadhi katika maisha yako japo huwa anasema anakupenda sana, unatakiwa kufanya yafuatayo.

Onyesha kumpenda na kumjali. Onyesha ni kwa namna gani ana thamani na umuhimu katika maisha yako. Japo itakuwa inauma kuonyesha upendo na thamani kwa mtu asiyefanya vile unavyotaka ila kumbuka upendo ni tiba.

 Kuonyesha kumpenda na kumjali mtu ni mbegu inayoweza kuota ua la upendo katika nafsi yake. Binadamu kaumbiwa upendo. Hufarijika, hujisikia amani sana pale anapoonyeshwa kupendwa na kuhitajika.

 Hivyo kumwonyesha upendo mtu asiyeonyesha kujali ni njia ya kuathiri akili na hisia zake ili uweze kufanikiwa kukuza thamani na hadhi yako katika maisha yake. Tathmini zinaonyesha kila mtu hupenda kuona akipendwa na kuthaminika hata kama haonyeshi kufurahi au kuheshimu suala hilo.

 Baada ya kuonyesha kumjali kwa muda mrefu kiasi huku yeye akijifanya hana habari, mpotezee kiaina. Punguza kuonyesha ni kwa  kiwango gani unampenda. Punguza kuongea naye juu ya thamani na hadhi aliyo nayo katika nafsi yako. Acha kabisa kulalamika juu ya tabia zake ambazo zimekuwa zikikukera.

 Dhamira ya kufanya hivyo ni kumfanya akumbuke hadhi yako katika maisha. Kama nilivyosema mwanzo, kila mtu anapenda kuambiwa maneno matamu na mtu anayempenda, kila mtu hupenda kuona akipendwa na kubabaikiwa, hivyo kuacha mambo hayo kutamfanya aanze kufikiri juu ya tabia yako mpya.

 Atajiuliuza ni kwanini sasa umebadilika? Nani anakufanya usimwone wa hadhi na thamani kama ilivyokuwa mwanzo? Maswali hayo, yatampeleka kujiuliza juu ya tabia zake pia.

 Ataanza kujitathimini kama alivyokuwa anakutendea ilikuwa haki. Mawazo hayo huweza kumpeleka haraka katika wivu wa kuamini tabia zake za kijinga alizokuwa akikufanyia zimekufanya uwe na mtu mwingine anayekupa unachotaka ndiyo maana sasa hivi huna tena habari naye.

 Kwa woga wa kukupoteza anaweza kuanza kukujali na kukufanyia mengi ambayo anahisi alikuwa hakufanyii ili akudhibiti usiende kwa mwingine.

 Kosa la wengi katika mahusiano pale wanapoona wenzao hawawajali na kuwapa thamani inayotakiwa ni kuanza kulalamika sana ama kuwalilia na kudhani kwa kufanya hivyo itakuwa njia ya kupendwa na kupewa wanachotaka, kitu ambacho sio kweli hata kidogo.

Mapenzi ni mbinu na mikakati. Unatakiwa kujua kucheza na akili pamoja na hisia za mwenzako ili uweze kutawala maisha yake.

 Ukiwa unamlilia sana mwenzako usidhani atabadilika tabia zake za ovyo. Mwenzako ili akupe thamani na hadhi stahili anatakiwa kuhisi wewe ni wa thamani na bora na unatakiwa kutendewa mengi makubwa na siyo hayo anayokutendea. Na njia bora ya kumfanya ahisi wewe ni wa thamani na bora zaidi ni kucheza na hisia pamoja na akili yake.

Ili upendwe sana auhitaji kumfanya mwenzako akuonee huruma. Jenga mazingira ya kumfanya muhusika ajue kabahatika kuwa na wewe ndipo atakupa hadhi na heshima stahili. Siyo kwa kulia wala kutoa lawama kila siku ila kwa kuonyesha wewe ni bora na unaweza kuwa na amani na utulivu hata bila yeye.

Instagram: g.masenga

Mwandishi wa makala haya ni mtaalamu mbobezi wa masuala ya ushauri wa uhusiano, maisha na utulivu wa hisia ( Psychoanalyst)

  [email protected]

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles