24.2 C
Dar es Salaam
Friday, April 19, 2024

Contact us: [email protected]

MTANDAO WIZI FEDHAWAKITHIRI NCHINI

Na Justin Damian


MATUKIO ya uhalifu na hususani wa fedha kwa njia ya mtandao unaelezewa kukuwa kwa kasi duniani. Kwa mujibu wa ripori ya mwaka jana iliyotolewa na PricewaterhouseCoopers (PWC) uhalifu wa masuala ya kifedha kwa njia ya mtandao, unagharimu kati ya asilimia 2-5 ya pato la ndani duniani

Kama ilivyo kwa nchi nyingine duniani, Tanzania imekuwa ikikumbwa na matukio haya japokuwa mamlaka zinazohusika zimekuwa hazijitokezi hadharani na kueleza ukubwa wa tatizo pamoja na kutoa elimu ya kutosha kwa umma juu ya namna ya kuepukana na kadhia hii

Moja kati ya habari kubwa iliyobeba toleo la gazeti letu la mwisho wa wiki au MTANZANIA Jumapili, ilikuwa ni habari ya Padri wa Kanisa katoliki ambaye anwani yake ya barua pepe iliingiliwa na wezi  (hackers) wa njia ya mtandao na kisha kuitumia kuomba fedha kwa ndugu jamaa na marafiki wa Padri huyo wakiwadanganya kuwa anatakiwa kubadilisha figo.

Kwa mujibu wa Padri Padri Paschal Luhengo ambaye ni Paroko wa Parokia ya Lupiro, Jimbo Katoliki Mahenge wahalifu hao walianza kutekeleza nia yao ovu mwaka jana mwezi wa Oktoba baada ya kufanikiwa kuiteka anuani yake ya barua pepe.

Padre alieleza kuwa, alitumiwa fedha na rafiki yake anayeishi Ulaya kwa njia ya Western Union lakini alipokwenda kuzichukua  alishangazwa kuambiwa kuwa fedha hizo tayari zimeshachukuliwa.

Baada ya hapo wahalifu hao waliendelea kuwasiliana na watu mbali mbali hususani waishio barani Ulaya marafiki wa Padre Luhengo wakijifanya ni yeye huku wakiwashawishi wachangie matibabu yake na walifanikiwa kupata malioni ya shilingi.

Kwa mujibu wa ripoti mbali mbali za kiuchunguzi ambazo gazeti hili imeziona, muhusika mkuu katika mchezo huo wa kihalifu yupo New Jersey nchini Marekani. Muhusika huyu hufanikisha upatikanaji wa fedha na kisha kuzituma kwa wahusika waliopo Tanzania kwa njia ya Western Union ambao huzitoa fedha hizo na kisha kuchukua sehemu na sehemu nyingine humrudishia mhusika.

Ni mtandao mpana ambao unaonekana kufanya kazi kwa ustadi mkubwa (organised crime) na kumekuwepo na tuhuma kwamba wahalifu hawa wanaushirikiano wa karibu na jeshi la Polisi ambao kwa namna fulani huwalinda.

Kuthibitisha hili la ushirikiano na Polisi, Padri Luhengo anasema,  yupo Padre mwenzake ambaye aliibiwa kama ilivyotokea kwake na wahusika walikamatwa kisha wakakiri kosa kwa Polisi na wakakubaliana wamlipe kidogo kidogo ili jambo hilo lisiende mbele zaidi. Ni jambo la kushangaza na kusikitisha!

Kwamba, wezi wanaachiwa waende kuwaibia watu wengine ili walipe fedha ambazo waliiba, ni utamaduni wa ajabu kabisa na mpya!

Wakati wahalifu hawa wakiendelea kutumia anuani ya barua pepe ya Padre Luhingo, walifanikiwa kufungua akaunti ya benki kwa jina la Parokia anayohudumu Padre huyo kwenye benki ya BOA iliyopo jijini Dar es Salaam. Baada ya kufungua waliomba mfadhili mmoja Ulaya kutuma Dola za Kimarekani 200,000 sawa na zaidi ya shilingi milioni 400 kwa ajili ya kusaidia ujenzi wa kanisa.

Kwa bahati nzuri, kabla mfadhili hajatuma fedha hizo, Padre Luhengo alishitukia na kuwaarifu Polisi ambao walifanikiwa kuzima jaribio hilo. Hata hivyo, suala la kufungua akaunti linaacha maswali mengi kuliko majibu.

Maswali hayo ni pamoja na je, wahalifu hao walitumia nyaraka halali au feki kufungulia akaunti? Je benki ilikuwa makini kukagua nyaraka na vielelezo hivyo kabla ya kukubali kufungua akaunti hiyo? Hapa tunapata picha kwamba benki zetu hazina umakini wa kutosha jambo ambalo kama halitafanyiwa kazi vitendo hivi vitaendelea Inaonekana vinasaidiwa na rushwa iliyotamalaki.

Polisi wahusishwa

Kwa mujibu wa Padre huyo, mmoja wa wahusika waliofungua akaunti hiyo alifanikiwa kukamatwa na Polisi na iligundulika kuwa ni mmiliki wa shule moja iliyopo Tabata jijini Dar es Salaam. Cha kushangaza ni kuwa, baada ya kuhojiwa na Polisi aliachiwa na Polisi walimwambia Padre kuwa jamaa huyo alisema yeye siyo mhusika na kwa hiyo wanafanya uchunguzi kuwakamata wahusika. Mpaka sasa hakuna aliyekamatwa. Ni kesi ya nyani kupelekwa kwa ngedere.

Katika hali ya kawaida, hili haliingii akilini na ngumu kumeza. Padre anasema alipewa mpaka picha ndogo (passport size) ya mhusika huyo ambaye ndiye aliyefungua akaunti, iweje tena Polisi waseme hakuwa mhusika? Na kama sio  yeye mhusika ni nani?

Kwa kuangalia sababu  nilizozielezea hapa tuhuma kuwa Polisi wanashirikiana na genge hili hatari la wahalifu zinabeba uzito.

Kama ambavyo nimewahi  kueleza, mamlaka zinazohusika kama hazitalifanyia kazi suala hili kwa nguvu ni wazi kuwa huko tunakoelekea mambo yanaweza kuwa mabaya zaidi.

Ni muhimu kwanza wahusika watafutwe na kuchukuliwa hatua kali na pia elimu kwa umma itolewe juu ya tatizo hili  linalojenga usugu na namna ya kujiepusha nalo. Mabenki nayo yanaonekana kukosa umakini jambo ambalo limetoa mwanya kwa wahalifu kutekeleza malengo yao. Au tuseme na wao wamo?

Hawa wahalifu waliokuwa walikitumia jina na Padre Luhengo kutapeli watu walikuwa wanatumia kitambulisho bandia cha mpiga kura chenye jina la Padre huyo kuchukua fedha zilizokuwa zinatumwa kwa njia ya Western Union kwa benki nne tofauti lakini benki hawakuweza kulinga’amua suala la uhalali wa kitambulisho.

Kw nchi kubwa na inayoendelea kwa haraka kama Tanzania na wananchi wake kukjosa vitambulisho vya taifa vya haja matokeo yake ni hayo ya aibu. Watu wa Mungu wanapohusishwa  na utapeli au makosa ya jinai sio kuntu na haipendezi !

 

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles