27.5 C
Dar es Salaam
Thursday, April 25, 2024

Contact us: [email protected]

Mtaka: Viwanda Simiyu bidhaa moja kijiji kimoja  

Na GRACE SHITUNDU, DAR ES SALAAM

KATIKA kuhamasisha ujenzi wa Uchumi wa Viwanda, Shirika la Kuhudumia Viwanda Vidogo (SIDO) limeanzisha Mkakati wa Wilaya Moja Bidhaa Moja (ODOP) ili kuchochea maendeleo ya Viwanda vidogo kwa lengo la kuongeza kipato na ajira kwa wananchi.

Dhamira ya Shirika hilo ni kuhakikisha kuwa kuna viwanda katika Halmashuri zote kwa kufuata mpango wa Wilaya moja Bidhaa moja.

Mkakati huu unakusudia kuibua na kuendeleza bidhaa moja kwa awamu katika Wilaya kwa kuzingatia rasilimali zilizopo katika Wilaya husika kwa kuhakikisha kuwa wadau wanachagua na kuwekeza katika viwanda vidogo na kuzalisha bidhaa ili kuweza kuharakisha maendeleo ya kiuchumi Vijijini.

Wakati utekelezaji wa mkakati huo ukiendelea, Mkoa wa Simiyu umedhamiria kwenda mbali zaidi kwa kuanza maandalizi ya utekelezaji dhana ya ‘bidhaa moja, kijiji kimoja’

MTANZANIA lilifanya mahojiano maalumu na Mkuu wa Mkoa huo Anthony Mtaka anayeelezea namna watakavyoitumia Sido kutekeleza mkakati huo.

Anasema moja ya ahadi alizoahidi wakati anateuliwa na Rais ni kuhakikisha kwamba anaubadilisha mkoa wa Simiyu kuwa mkoa mwingine kiuchumi.

Anaeleza kwamba wananchi walipata elimu na kujifunza mbinu na utaalamu wa aina mbalimbali katika kilimo, mifugo na uvuvi kwenye maonyesho ya Nanenane kwa muda wa siku 10 lengo ni kufanya kilimobiashara na kwenda kwenye uchumi wa viwanda.

“Sasa tuna maonyesho ya kitaifa ya Sido  yatakayofanyika katika viwanja vya Nyakabidi kuanzia Oktoba 23 hadi 28 mwaka huu, huko wananchi wataendelea kujifunza dhana ya mnyororo wa thamani ya mazao na utekelezaji wa uchumi wa viwanda.

“Sisi kwenye mkoa tunatekeleza ile dhana ya  bidhaa moja wilaya moja, na tunataka kwenda kwenye  bidhaa moja kijiji kimoja, hivyo maonyesho haya ndio maandalizi”

Anaongeza kusema, “Na tunaanza maandalizi kwasababu tunahitaji  mwaka 2019 kwa Simiyu uwe ni mwaka ambao Rais atazindua rasmi  utekelezaji wa dhana ya bidhaa moja wilaya moja,  bidhaa moja kijiji kimoja”

Anasema mkoa huo una vijiji 480 ndani ya wilaya tano hivyo ili kuufanya uchumi wa kila kijiji kuimarika ni kuileta Sido kwenye maisha ya wananchi.

“Namna ya kwenda kwenye utekelezaji huo wa bidhaa moja kijiji kimoja ni kuifanya Sido ije kwenye maisha ya wananchi wa Simiyu kwenye vijiji 480.

“Maana yake mnabainisha uchumi wa kijiji, kwa mfano kijiji hiki uimara wake ni zao la mpunga kwa hiyo tunahakikisha Sido inaleta teknolojia nzuri kwanza za uvunaji wa mpunga, wananchi wanatoka kwenye kupura mpunga chini unatoka na mawe na michanga,

“Lakini pili mnakwenda kwenye ukoboaji ambao unakuwa na grade la kwanza, pili na ya tatu, lakini pia pumba endapo kuna kitu mnapaswa kufanya mna kuwa na teknolojia ndogo ambayo itawasaidia kupata mkaa ambao unaweza kutokana na pumba za mpunga”.

Anaongeza kusema, ‘Lakini kama kijiji kingine uimara wake ni mahindi hivyo mnajua tutavuna mahindi, lakini tunakuwa na mashine ndogo za kusaidia kupukuchua badala ya watu kupukuchua kwa mikono, lakini yatakobolewa, mahindi yale yakikobolewa, mabaki yanayokobolewa na mabua yake kuhakikisha kuna mashine ya kuchakata chakula cha mifugo”.

Anasema kwa kufanya hivyo ina maana kwamba unaileta Sido kwenye maisha ya wananchi wa kawaida kwenye vijiji 480 ya mkoa wa Simiyu.

“Ile dhana ya mnyororo wa thamani ya mazao inatekelezeka kwa kuiweka Sido katika jamii ya wananchi wa kawaida”, anasema.

Anasema teknolojia za Sido zikiweza kutumiwa kwenye maeneo ya jamii za kitanzania, wananchi wataweza kuongeza thamani ya mazao yao ya kilimo, mazao ya mifugo.

Anasema kwa sababu kwa wananchi wa kawaida hutegemei kupata kiwanda kikubwa au teknolojia kubwa bali utakuta teknolojia ndogo.

“Huko utakuta teknolojia ambazo mwananchi atakamua mafuta yake ya alizeti atumie, atakoboa mpunga ataupa madaraja, huko utakuta viwanda vidogo vidogo vyenye teknolojia ya kutengeneza viatu, teknolojia ndogo za usindikaji wa maziwa, teknolojia ndogo za urinaji na ukamuaji wa asali na ufungashaji wake,”anasema.

Anasema ajenda ya Rais ni uchumi wa viwanda, na unapohusisha Sido inamaana ni viwanda vidogovidogo vinavyoweza kupatikaka katika jamii na rahisi kufanyia matengenezo na kuzitunza mashine hizo.

“Tutaitumia Sido kutekeleza dhana ya kuimarisha uchumi wa vijiji  480,  kwani malengo ni kutumia rasilimali ambazo ni malighafi, utaalamu, ujuzi zilizopo katika wilaya na sasa kijiji kimoja kimoja.

“Hii itasaidia kuwapa huduma wenye viwanda vidogo na wanaotaka kuanzisha viwanda kuongeza thamani mazao yanayolimwa katika kijiji  hadi kufikia bidhaa.

Anaongeza kusema, “itawajengea uwezo wa wajasiriamali vijijini katika mbinu za kibiashara na teknolojia ili kuwezesha kushindana katika soko la wilaya,  mkoa,  kitaifa na kimataifa.

Anasema baadhi ya nchi zimefanikiwa katika sekta ya viwanda kwa kutumia mfumo huo ambao umetekelezwa katika Taifa hadi ngazi ya Vijiji na kuchochea maendeleo.

“Wakati wote watu wamekuwa wakitupongeza Simiyu na kusema kwamba tunaweza kuwa manispaa lakini ninachoamini mimi ni kwamba Simiyu inaweza kuwa kanda rasmi ya serikali huko tunakoenda,”anasema.

“Kama leo tumepata hati ya ardhi hatuendi Mwanza, tumepata hospitali ya rufaa hatuendi Bugando, na tuna kanda ya kilimo, ni lazima Simiyu tubadilike pia katika uchumi,”anasema.

Aidha Mtaka anawakaribisha wadau mbalimbali wa teknolojia rahisi sambamba na wajasiriamali kushiriki Maonyesho ya SIDO kitaifa yatakayofanyika katika mkoa huo kwa mara ya kwanza

Anasema katika maonyesho hayo ya siku tano  kutakuwa na uonyeshaji wa teknolojia mbalimbali na  uhamasishaji wa kutumia teknolojia hizo za kisasa.

“Tumedhamiria  kufanikisha azma ya serikali ya awamu ya tano chini ya Rais Magufuli ya kujenga uchumi wa kati na viwanda ifikapo 2025,”anasema.

 “Maonyesho hayo ni fursa pekee ya wajasiriamali kuonyesha ubora wa bidhaa zao na pia ni nafasi mojawapo ya kutafuta masoko ya uhakika na kujitangaza.anasema

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles