25.7 C
Dar es Salaam
Friday, April 19, 2024

Contact us: [email protected]

MSHAMBA 14 YAFUTWA MOROGORO

Na Ashura Kazinja

-Morogoro

WAZIRI wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi, amesema Rais Dk. John Magufuli amefuta umiliki wa mashamba makubwa yenye ukubwa wa heka 14,341 yaliyokuwa yakimilikiwa na watu mbalimbali kwenye wilaya za Mvomero na Kilosa mkoani Morogoro.

Amesema hatua hiyo imetokana na wamiliki wa mashamba hayo kushindwa kuyaendeleza licha ya kutakiwa kufanya hivyo kwa muda mrefu, ikiwamo kuandikiwa barua kwa mujibu wa sheria.

Akizungumza jana mjini hapa na viongozi wa Mkoa wa Morogoro, Lukuvi alisema kuwa moja ya sababu ya kufutwa kwa umiliki huo, ni pamoja na wamiliki hao kushindwa kulipa kodi za Serikali kama inavyotakiwa kwa zaidi ya miaka mitatu.

Alisema miongoni mwa mashamba yaliyofutiwa umiliki huo ni pamoja na la Waziri Mkuu Mstaafu, Frederick Sumaye na mkewe Esther  lenye ukubwa wa ekari 473.

Mbali na hilo, pia lipo la Kampuni ya Noble Agriculture Enterprises Limited ambayo mmiliki wake anatambulika kwa jina la Gitu Patel anayemiliki mashamba manne yenye ukubwa wa ekari 2,661.

“Kwa maelekezo ya Rais, baada ya kufutwa mashamba hayo, ni wajibu wa Mkuu wa Mkoa na Wilaya kuhakikisha mashamba hayo yanasimamiwa vizuri katika ugawaji, hasa kwa kuzingatia watu wenye mahitaji ambao wapo jirani na mashamba hayo.

“…Rais pia ameonya viongozi wenye nia ya kujipenyeza kwa lengo la kuchukua maeneo kwenye mashamba hayo na kwamba wale watakaojipenyeza watajulikana na hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi yao,” alisema Lukuvi.

Alisema kuwa Serikali ya Awamu ya Nne ilifuta mashamba pori 16 yaliyopo katika Wilaya ya Kilosa na Mvomero, hata hivyo zipo taarifa kuwa baadhi ya mashamba hayo yanaendelea kushikiliwa na wajanja na alimtaka Mkuu wa Mkoa na Wilaya husika kuwasilisha taarifa sahihi za mashamba hayo.

“Hata hao wanaosema kuwa kulikuwa na kesi wanatakiwa kusema wamefungua mahakama gani badala ya kulalamika jumla. Na huu uamuzi ulichukuliwa si kwa kuangalia mtu ana rangi gani,” alisema.

Naye Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Dk. Stephen Kebwe, alisema kuwa awali mkoa ulifanya uchambuzi wa mashamba pori na kubaini kuwapo 223, huku Wilaya ya Kilosa ikiwa na mashamba pori 198.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles