27.1 C
Dar es Salaam
Friday, March 29, 2024

Contact us: [email protected]

Msamaha wa watuhumiwa EPA waibua utata

mwakyembeNA AZIZA MASOUD, DODOMA

MSAMAHA uliotolewa na Rais mstaafu Jakaya Kikwete kwa baadhi ya watuhumiwa wa Akaunti ya Madeni ya Nje (EPA), umezua utata baada ya Mbunge wa Konde, Khatib Said Haji (CUF) kuhoji mamlaka ya kiongozi huyo kikatiba.

Katika swali lake la msingi, Haji aliuliza; “Je, rais ana mamlaka kisheria kutoa msamaha kwa watuhumiwa wa uhalifu wa aina yoyote ambao mashauri yao yapo katika vyombo vya dola kwenye hatua za uchunguzi, upelelezi au mahakamani?”

Akijibu swali hilo, Waziri wa Katiba na Sheria, Dk. Harrison Mwakyembe alisema ibara ya 45(1) (a)-(d) inampa rais mamlaka ya kutoa msamaha kwa mtu yeyote aliyepatikana na hatia mbele ya mahakama.

Alisema kifungu cha (ii) cha ibara hiyo pia kinampa mamlaka rais kumwachia kabisa au kwa muda maalumu mtu yeyote aliyehuhumiwa, kuadhibiwa kwa ajili ya kosa lolote.

Dk. Mwakyembe alisema kifungu cha (iii) pia kinamruhusu rais kubadilisha adhabu yoyote aliyopewa mtu yeyote kwa kosa lolote iwe adhabu tahafifu wakati kifungu cha (iv) kinamruhusu rais kufuta adhabu yoyote au sehemu ya adhabu.

“Kwa kuzingatia masharti hayo ya Katiba, msamaha wa rais unatolewa kwa mtu aliyetiwa hatiani na kupewa adhabu na mahakama,” alisema Dk. Mwakyembe.

Alisema watuhumiwa wa uhalifu ambao mashauri yao yapo katika hatua ya upelelezi au uendeshaji mahakamani hawaguswi na masharti ya ibara hiyo.

“Kwa sababu hiyo, rais hawezi kisheria kutoa msamaha kwa watuhumiwa wa uhalifu wa aina yoyote ambao mashauri yao yapo katika vyombo vya dola kwenye hatua za uchunguzi, upelelezi au mahakamani,” alisema Dk. Mwakyembe.

Alisema kwa muda huo hatima ya watuhumiwa hao inakuwa bado ipo katika mamlaka husika za uchunguzi, mashtaka na mahakama.

Katika maswali yake mawili ya nyongeza, Haji alihoji: “Rais Kikwete alitoa msamaha kwa watuhumiwa wa EPA. Je, kutokana na kitendo hicho rais alivunja Katiba kwa kutumia madaraka yake vibaya

“Kwa mujibu wa majibu yako ya msingi, ni dhahiri watuhumiwa wa EPA bado wanastahili kupelekwa mahakamani kwa sababu msamaha walioupata ulikuwa kinyume na Katiba. Je, Serikali inatoa kauli gani juu ya kuhusu kuwafikisha watuhumiwa wale wa wizi wa EPA kujibu tuhuma zao.”

Dk. Mwakyembe akijibu, alisema swali hilo limeshaulizwa na ameshalijibu kwa mujibu wa katiba.

“Jibu langu ni la kikatiba na nililolisema ndiyo Katiba inavyosema, mimi sio tu mwanasheria bali ni mwalimu wa sheria, pia nasema chini ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ibara ya 45.

“Mheshimiwa rais madaraka yake yapo katika kumsamehe mtu ambaye tayari amehukumiwa na kupewa adhabu, naomba nieleweshe vizuri huu msamaha hana Rais wa Jamhuri ya Muungano tu, bali hata Rais wa Zanzibar chini ya ibara ya 59 ya Katiba ya Zanzibar ya 1984,” alisema Dk. Mwakyembe.

Alisema Rais wa Zanzibar anaruhusiwa kutoa msamaha huo kama kunakuwa na makosa.

Dk. Mwakyembe alisema kwa sababu hizo na taarifa alizonazo ni wazi Rais Kikwete hakutumia kifungu hicho cha Katiba kuwasamehe watuhumiwa hao.

Katika hatua nyingine, wabunge wa upinzani walitoka nje ya ukumbi wa Bunge kupinga kuapishwa kwa wabunge kutoka Baraza la Wawakilishi Zanzibar.

Kususia kwa kiapo hicho, ni mwendelezo wa msimamo wa wabunge wa upinzani kutotambua uchaguzi wa marudio uliofanyika Machi 20 mwaka huu visiwani humo uliomweka madarakani Rais Dk. Ally Mohammed Shein.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles