31.2 C
Dar es Salaam
Thursday, March 28, 2024

Contact us: [email protected]

Msajili: Pingamizi la Mbowe, matokeo ya kunipuuza

Freeman Mbowe
Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe

PATRICIA KIMELEMETA NA NORA DAMIAN, DAR ES SALAAM

SIKU moja baada ya Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Freeman Mbowe, kuwekewa pingamizi la kutogombea nafasi hiyo kwa awamu ya tatu, Msajili wa Vyama vya Siasa, Jaji Francis Mutungi, amesema kinachotokea kwenye chama hicho ni matokeo ya kupuuza ushauri wake.

Mbowe amewekewa pingamizi na aliyekuwa Mwenyekiti wa Chadema Mkoa wa Tabora, Kansa Mbarouk, ambaye pia ni mgombea wa nafasi hiyo, kwa madai ya kukiuka katiba ya chama hicho na maagizo ya msajili wa vyama vya siasa.

Akizungumza na MTANZANIA jijini Dar es Salaam jana, Jaji Mutungi alisema kuwa ofisi yake iliwashauri viongozi wa chama hicho kuhitisha mkutano wa Kamati Kuu ili waweze kufanya marekebisho ya Katiba yao kabla ya uchaguzi, lakini walipuuza ushauri wake.

Alisema kuwa baada ya ushauri wake huo kupuuzwa, Mbarouk ameona fursa hiyo na kuamua kuitumia.

“Tuliwashauri Chadema muda mrefu kuhitisha mkutano wa Kamati Kuu ili wafanye marekebisho ya Katiba yao, lakini walitupuuza na kuanza kutulaumu. Kinachotokea sasa ni matokeo ya kile ambacho tulijua kinaweza kutokea katika uchaguzi wao,” alisema Jaji Mutungi.

Alisema baada ya kuwaambia hayo, viongozi wa chama hicho waliishutumu ofisi ya msajili na kudai kuwa inatumika.

Jaji Mutungi alisema kutokana na hali hiyo, ofisi yake imeamua kukaa kimya na kuacha mchakato wa uchaguzi uendelee, lakini mwishowe wanatakiwa kuwasilisha taarifa zao katika ofisi hiyo.

“Tumeamua kuwaacha waendelee na mchakato wao, watavutana mwisho watachoka wakimaliza watatufuata,” alisema.

Mbarouk aliwasilisha taarifa yenye kumbukumbu namba Mbarouk/UCH/14 kwenda kwa Katibu Mkuu wa Chadema na Msajili wa Vyama vya Siasa ambayo inasema kuwa kufikia Septemba 14, siku ya uchaguzi mkuu wa chama hicho, Mbowe atakuwa ametumikia vipindi viwili katika nafasi ya mwenyekiti taifa.

Kulingana na Katiba ya Chadema kama ilivyothibitishwa na Msajili wa Vyama vya Siasa, hakuna mwanachama anayeruhusiwa kuchaguliwa kuongoza zaidi ya vipindi viwili katika cheo kimoja na ngazi moja.

Juni mwaka huu, msajili alidai kuwa Mbowe hawezi kuwania nafasi hiyo kutokana na Katiba yao kuwa na kipengele cha ukomo wa uongozi wa vipindi viwili.

Alisema ili aweze kuendelea na nafasi hiyo, alipaswa kuitisha mkutano wa Kamati Kuu ili waweze kufanya marekebisho katika Katiba yao ikiwa ni pamoja na kuondoa kipengele cha ukomo wa uongozi.

Katika hatua nyingine, chama hicho kimesema hakijapata taarifa za Mbowe kuwekewa pingamizi.

Akizungumza na waandishi wa habari katika ofisi za chama hicho jana, Mkurugenzi wa Kampeni na Uchaguzi, Singo Benson, alisema kulingana na Katiba ya chama hicho walioomba kuteuliwa kama wana pingamizi au malalamiko wanapaswa kupeleka ofisini, lakini hawajapokea hadi sasa.

“Sisi tumesoma tu kwenye magazeti, hatuna taarifa yoyote ya pingamizi hadi sasa. Huyo anayesema alileta je, alilileta kwa njia gani na kama ‘dispatch’ ipo, aseme nani alipokea na kusaini,” alisema Benson.

Alisema ofisi ya chama hicho iko wazi muda wote na kwamba kwa siku ya juzi alikuwapo ofisini hadi saa 5 usiku, lakini hakupokea pingamizi la aina yoyote.

Wakati huo huo, chama hicho jana kiliwatangaza washindi wa uchaguzi wa Baraza la Wazee Taifa.

Nafasi ya mwenyekiti ilichukuliwa na Hashim Juma Issa kutoka Zanzibar, Makamu Mwenyekiti Bara ni Suzan Lyimo na Makamu Mwenyekiti Zanzibar ni Omar Masoud Omar.

Wengine ni Rodrick Lutembeka ambaye alichaguliwa kuwa Katibu Mkuu na Erasto Gwota aliyechaguliwa kuwa Mweka Hazina.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles