23.9 C
Dar es Salaam
Wednesday, April 24, 2024

Contact us: [email protected]

MRADI WA LNG UTAKAVYONUFAISHA NCHI

Na Mwandishi Wetu             |                 


KWA miaka kadhaa iliyopita, kuna neno moja ambalo limetawala fikra za watu kuliko mengine yote nchini Tanzania: ‘ujenzi wa viwanda’. Nchi imekumbwa na wimbi la matumaini, kwa sehemu kubwa matumaini hayo yamesababishwa na dhamira ya Serikali ya kuweka vipaumbele katika maendeleo na ukuaji uchumi wa muda mrefu.

Maboresho yanayoendelea na ya kudumu si tu yataimarisha uchumi, lakini yatasaidia maeneo ambayo kwa sasa  yana maendeleo duni, ili yakue na kukomaa. Ukuaji wa viwanda unaweza tu kuchukuliwa kuwa umefanikiwa iwapo Tanzania yote itanufaika.  Mradi wa gesi asilia na gesi asilia iliyosindikwa Tanzania (LNG), utakuwa na wajibu mkubwa katika kufanikisha azma hiyo, ikiwa mradi utaendelea hadi utekelezaji.

Kuboresha miundombinu

Katika maeneo mengi nchini Tanzania, kuna miundombinu michache ya kisasa na hivyo kuna fursa chache sana za maendeleo. Hata hivyo, maeneo mengi ya Tanzania yaliyo na maendeleo duni yako njiani kupata maboresho makubwa ambayo yatapelekea ukuaji uchumi na kuboresha hali ya maisha kwa wananchi.

Mradi wa LNG ni msingi wa mabadiliko haya. Uwekezaji wa ukubwa huu na wenye matarajio kama haya, haujawahi kutokea nchini Tanzania na ikiwa utatekelezwa  kwa mafanikio utaleta matokeo mazuri  na chanya katika sehemu nyingi. Si tu Mradi wa LNG utatangaza uwezo wa Tanzania kukaribisha miradi ambayo ni mikubwa na yenye vipengele vingi, ambayo itazishawishi biashara nyingine duniani kuanzishwa nchini, bali utainua uchumi kwa kiwango ambacho pesa itapatikana kuweza kuendeleza na kukuza maeneo yasiyo na maendeleo.

Mabadiliko rahisi ambayo yatasaidia nchi kwa kiwango kikubwa, ni suala la kuondokana na matumizi ya mkaa kama chanzo cha nishati. Si tu matumizi ya mkaa yana madhara kwa mazingira, lakini ukataji miti mingi ni kisababishi kikubwa cha uharibifu wa misitu. Mara baada ya mradi wa LNG kuanza kufanya kazi, ukianzia na mijini, nishati yote inayotumika majumbani nchini Tanzania inaweza kutokana na gesi asilia, ambayo itakuwa chanzo cha nishati kilicho na ufanisi na rahisi zaidi kutumia. Uhakika wa upatikanaji wa nishati unaweza kuwa sababu kubwa itakayochangia kuvutia wawekezaji wa nje.

Uchumi thabiti na mkubwa lazima unufaishe nchi kwa ujumla na hicho ndicho ambacho Serikali inataka kuona na kile ambacho Mradi wa LNG unaweza kufanikisha. Hata hivyo, ili kufikia mafanikio yatakayodumu muda mrefu, lazima mradi utengeneze fursa za ajira kwa wananchi na hiyo ni sehemu muhimu sana katika azma ya ujenzi wa viwanda, azma ambayo Mradi wa LNG utaweza kufanikisha.

Kuimarisha elimu ya ufundi

Kujenga mradi wenye ukubwa wa Mradi wa LNG kutaambatana na fursa lukuki za biashara za ndani pamoja na kujitangaza kwenye baadhi ya mashirika makubwa duniani.

Wakati wabia wakuu katika mradi huu ambao ni Shell, Statoil, ExxonMobil, Ophir na Pavilion, watasimamia na kujenga kiwanda cha LNG na miundombinu yake, makandarasi na wasaidizi wao bila shaka watatoka Tanzania watahitajika kwa ajili ya ujenzi wa   mradi huu katika hatua mbalimbali.

Kwa makampuni na watu binafsi ambao tayari wana ujuzi na utaalamu  unaotakiwa, kutakuwa na fursa  nyingi za ajira. Na wale wanaotarajia kuja kufanya kazi katika hatua na sehemu mbalimbali za mgodi, bado kuna muda wa kutosha wa kujifunza na kupata ujuzi utakaohitajika.

Mafundi wenye utaalamu kwenye fani za kama vile kuchomea chuma, ufundi bomba, fundi seremala, uhandisi na kufunga mabomba watahitajika sana katika miaka ijayo na kama miradi mingi itakuja Tanzania kufuatilia kukamilika kwa Mradi wa LNG, basi mafundi hao watahitajika na watatumia ujuzi wao kwa muda mrefu zaidi.

Halafu kuna hii dhana ya “matokeo ya kujiongeza kiuchumi” ambayo tuliijadili katika makala zilizopita, ikimaanisha kwamba kwa kila ajira inayotengenezwa moja kwa moja katika sekta ya gesi, kuna ajira nyingine nyingi zinatengenezwa sehemu nyingine katika uchumi wa Tanzania.

Kwa kifupi, tunaweza kufikiria kwamba utekelezaji wa mradi huu ni kama vile unasababisha mawimbi yanayoanzia sehemu moja, halafu kuenea katika miduara inayofuatana kwenye dimbwi. Ukubwa wa mradi una maana kwamba utatengeneza mawimbi makubwa yenye urefu na upana wa kutosha kufikia dimbwi moja kubwa la maendeleo ya Tanzania.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles